Kenya, Tanzania zafungua ukurasa mpya wa ushirikiano Afrika Mashariki

May 5, 2021 1:13 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Bunge la Kenya lililo na mjumuiko wa wabunge wa Seneti na Bunge la Taifa wakati siku ya pili ya ziara yake.  Picha| Ikulu.


  • Amesema uhusiano huo unaendeshwa kwa undugu na mahusiano ya kiekolojia.
  • Amewataja wanaodhani Tanzania na Kenya ni nchi za mafarakano ni watu wenye “akili mbovu”.
  • Amesititiza nchi hizo mbili kuwa na tabia ya kukutana mara kwa mara.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uhusiano wa Tanzania na Kenya haupaswi kujengwa katika misingi ya ushindani na uhasama badala yake ujikite katika undugu, urafiki na ushirikiano unaowezesha ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili. 

Amesema nchi hizo mbili hazina uadui kama inavyodhaniwa na kuzushwa na baadhi ya watu kwa sababu umefungamanishwa na vitu vingi mbali ya mipaka ya ramani, ekolojia na undugu ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka 64 kwa sasa.

“Binafsi huwa nashangazwa sana na wale wanaodhani eti Kenya na Tanzania ni Washindani na hivyo uhusiano wetu unapaswa kuwa wakuhasimiana na kukamiana. Nawashangaa wanaodhani kuwa Kenya peke yake ama Tanzania peke yake inaweza kuendelea bila mwenzake,” amesema Rais Samia.

Rais Samia  amewaita watu hao kuwa ni wenye “mioyo ya choyo, maono mafupi na akili mbovu”.

Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 5, 2021 wakati akihutubia Bunge la Kenya lililo na mjumuiko wa wabunge wa Seneti na Bunge la Taifa wakati siku ya pili ya ziara yake.  

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema hiyo ni mitazamo hasi na mara nyingi inachangiwa na kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri kati ya nchi hizo yanayochangiwa na baadhi ya wanasiasa.

Ili kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi hizo mbili, Mama Samia amewasihi viongozi wa pande zote mbili kukutana na kufanya majadiliano ya mara kwa mara kwani ndugu wanaotembeleana ndiyo wanaoelewana huku wasiotembeleana husababisha mashaka miongoni mwao.

Aidha, amewasihi Wabunge wa nchini Kenya kuwa tayari kuwarekebisha viongozi wa nchi hizo mbili wanapoona mambo hayaendi sawa na pia kuyafanyia kazi yote ambayo wamekubaliana ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kimahusiano baina ya Kenya na Tanzania.

Amewakaribisha wawekezaji wa Kenya wenye mitaji kuja Tanzania kuwekeza kwa sababu nchi ina rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zitaweza kuboresha maisha ya pande mbili.

Hotuba aliyoitoa Rais Samia katika Bunge la Kenya inahitimisha ziara yake ya siku mbili iliyoifanya nchini humo ambayo imemkutanisha na wadau mbalimbali akiwemo mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta ambapo wamekubaliana mambo mbalimbali yenye manufaa kwa pande mbili. 


Soma zaidi:


Pia katika ziara hiyo, Rais alikutana na wafanyabiashara wa jukwaa la biashara la Tanzania na Kenya. Pia ameshiriki kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya; na dhifa maalum iliyoandaliwa na mwenyeji wake katika hoteli ya Serena jijini Nairobi. 

Enable Notifications OK No thanks