Rais Samia: Uamuzi wangu wa kuja Kenya si wa bahati mbaya
- Amesema hiyo ndiyo ziara yake ya kwanza tangua aingie madarakani Machi 19 mwaka huu.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara yake nchini Kenya iliyoifanya kwa siku mbili ndiyo ziara yake kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu.
Rais Samia amebainisha hayo leo Mei 5, 2021 jijini Nairobi wakati akihutubia kikao cha Bunge la Taifa na Seneti na kueleza kuwa alitembelea Uganda hivi karibuni lakini haikua ziara rasmi.
Rais Samia Suluhu Hassan: Hii ni ziara yangu ya kwanza rasmi tangu kushika wadhifa wa urais…Kenya ndio nchi ya kwanza kwa rais wa sita wa tanzania kufanya ziara rasmi..Nilikwenda Uganda kwa madhumini ya kutia saini mkataba, haikua ziara rasmi pic.twitter.com/u3SxHTUSQW
— Citizen TV Kenya (@citizentvkenya) May 5, 2021
“Uamuzi wangu wa kuja Kenya si wa bahati mbaya bali ni wa makusudi, busara inaelekeza kuwa ukiwa mpangaji mpya kwenye eneo ni lazima ujitambulishe kwa majirani, nilipata mialiko mingi lakini nikasema nianze hapa,” amesema Rais Samia na kubainisha kuwa Kenya na Tanzania ni ndugu na zina ushirikiano wa muda mrefu ambao hauwezi kuyumbishwa na mtu yeyote.
Amesema Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kenya huku akizitaka nchi hizo mbili kuziona kama ndugu na siyo washindani ambao wanaishi kwa kuhasimiana.