Corona ilivyopunguza abiria wa ndege Tanzania

May 18, 2021 1:47 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imepungua kwa asilimia 43.5  hadi abiria milioni 2.5 katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Aprili, 2021.
  • Sababu kubwa ni athari za janga la COVID-19 kwenye sekta ya anga.

Dar es Salaam. Janga la Corona siyo tu limeathiri uchumi na afya za watu duniani, bali athari zake zimeenda mbali na kuathiri sekta ya anga nchini Tanzania, jambo lliloshusha idadi ya watu wanaotumia usafiri wa ndege na kupunguza mapato katika sekta hiyo.

Idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga yaani ndege imepungua kwa asilimia 43.5  hadi abiria milioni 2.5 katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Aprili, 2021.

Idadi hiyo ni sawa na upungufu wa abiria milioni 1.9 ikilinganishwa na abiria milioni 4.5 waliotumia usafiri huo mwaka 2019/20. 

“Sababu za kupungua kwa abiria wanaosafiri ndani na nje ya nchi ni mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 ambapo nchi nyingi zilifunga na kuzuia safari za anga,” amesema Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Dk Leonard Chamuriho katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2021/22.

Janga hilo limechangia kupungua kwa abiria wa ndani na nje ya nchi wanaotumia usafiri wa ndege. 

Dk Chamuriho amesema idadi ya abiria wanaosafiri kwenda na kutoka nje ya nchi imepungua kutoka abiria milioni 2.1 hadi kufikia abiria 819,272 huku wasafiri wa nje wakipungua kutoka

“Aidha, idadi ya Abiria wanaosafiri ndani ya nchi imepungua hadi abiria milioni 1.6 ikilinganishwa na Abiria milioni 2.4 waliosafiri katika kipindi kama hicho mwaka 2019/2020,” amesema. 

Idadi hiyo ya abiria wa ndani na wale wanaokwenda nje ya nchi inajumuisha idadi ya abiria wote waliokuwa wanatumia usafiri wa anga katika kipindi kilichotajwa.


 Soma zaidi:


Kupungua kwa safari za ndege pia kumesababisha kupungua watalii wanaokuja nchini na shughuli za biashara hasa zinazofanyika kimataifa na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi. 

Waziri huyo amesema Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya anga ili kuimarisha sekta hiyo na kuvutia watu wengi kutumia usafiri huo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za kibiashara na utalii.


Bajeti ya wizara hiyo yashuka

Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/22 wizara hiyo inatarajia kutumia Sh3.7 trilioni ambapo kati ya fedha hizo, Sh2.2 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi.

Shughuli ambazo zitatekelezwa katika sekta ya uchukuzi ambayo imechukua zaidi ya nusu au asilimia 56.5 ya bajeti wizara hiyo ni pamoja na miradi mbalimbali ya usafiri wa majini na nchi kavu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa meli zinazotumiwa katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ili kuwarahishia wananchi usafiri.

Pia ukaratbati na ujenzi wa viwanja vya ndege na uboreshaji wa miundombinu ya bandari. 

Hata hivyo, bajeti hiyo ya mwaka 2021/22 imeshuka kutoka Sh4.78 trilioni iliyopangwa mwaka 2020/2021.

Enable Notifications OK No thanks