Hatari inayowakabili wavutaji sigara wasio wa hiari Tanzania

May 27, 2021 9:10 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya watu hujikuta wakivuta sigara bila hiari katika shughuli zao za kila siku.
  • Watu hao wako katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya ikiwemo saratani ya mapafu.
  • Wataalam wa masuala ya afya wameeleza kuwa zuio la uvutaji wa sigara maeneo ya umma uwekewe msisitizo.

Dar es Salaam. Unaweza kusema wewe siyo mvutaji wa sigara lakini huenda unahitaji kutafakari mara mbili kama uko sahihi.

Katika shughuli za kila siku, watu hujikuta wakivuta sigara kwa lazima katika maeneo tofauti ikiwemo sokoni, ofisini, vituo vya daladala, kwenye hata kwenye foleni za usafiri wa vyombo vya moto.

Hata katika maeneo ambayo baadhi ya watu huamua kwenda kutembea binafsi, na watoto wao, au familia, pia wanajikuta wakiwa wahanga wa uvutaji sigara bila hiari yao baada ya kuvuta moshi wa bidhaa hiyo ya tumbaku kutoka kwa watu waliopo katika maeneo hayo.

Tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika kuhusu uvutaji wa sigara ikiwemo tafiti kutoka Kituo cha kuzuia na kupambana na Magonjwa (CDC) cha Marekani zinaonyesha kuwa kuvuta sigara bila ridhaa hutokea baada ya mtu ambaye siyo mvutaji kuvuta moshi unaotokana na bidhaa za tumbaku.

Hali hiyo inaweza kuwa kutoka kwenye sigara yenyewe au hata moshi ambao anaupuliza mtu ambaye anavuta sigara.

CDC inaeleza kuwa, kwenye moshi wa bidhaa za tumbaku kuna kemikali zaidi ya 7,000 ambapo kati ya hizo, mamia yake ni kemikali mbaya na takriban kemikali 70 zimetajwa kuwa visababishi vya saratani.

Hali hiyo humweka mtu ambaye anafikiwa na moshi huo katika hatari ile ile kama ya mtu anayevuta sigara ikiwemo kupata ugonjwa wa saratani na changamoto zingine za kiafya.

Jamii bado iko gizani

Licha ya madhara yanayoambatana na uvutaji wa sigara usio wa hiari, bado watu wengi hawafahamu namna uvutaji huyo unavyochangia kuziweka afya zao matatani.

Mkazi wa Majumba Sita jijini Dar es Salaam, Amina Sued ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kama kuvuta sigara basi anavuta bidhaa hiyo kila siku na hana njia za kuepuka.

“Sigara watu wanavuta kila mahali jamani niwe stendi, nitavuta moshi wa sigara, muda mwingine unaweza ukawa hata kwenye daladala ukifika kwenye foleni kuna mtu pembeni yenu anavuta sigara kwenye gari yake. Kumsema huwezi, kumpiga huwezi,” amesema Sued.

Binti huyo amesema, hata akiwa katika ofisi yake, watu mbalimbali wazee kwa vijana hupita wakivuta sigara na mara zote hizo, moshi humfikia.

“Sipendi sigara lakini kwa jinsi nilivyozungukwa na wavuta sigara, naona na mimi ni mvutaji tu tena ukute navuta mara nyingi kuliko mvutaji kabisa,” amesema Sued.

Licha ya kuwa uvutaji wa sigara unazuiliwa katika maeneo ya wazi, bado badhi ya watu huvuta sigara katika maeneo hayo na kuwaletea madhara wasiohusika. Picha| AP.

Uvutaji wa sigara katika maeneo ya wazi haukubaliki

Sheria ya Usimamizi wa Bidhaa za Tumbaku, Sura ya 121 TL ya mwaka 2003, kipengele cha 12(1) ambacho kinakataza matumizi ya bidhaa hiyo katika maeneo ya umma ili kuilinda jamii kutokana na madhara yatokanayo na moshi wa sigara.

Sababu kubwa zuia uvutaji sigara maeneo ya umma ni kuwa uvutaji sigara ni hiari lakini kuvuta hewa safi ni lazima, hivyo mtu anayetumia kilevi hicho hana budi kukaa mbali ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa kama ya moyo na saratani kwa wasiotumia bidhaa hizo. 

Licha ya msimamo wa sheria bado utekelezaji wake una changamoto kwa sababu baadhi ya watu bado wanavuta sigara katika maeneo ya umma. 

Pia ukosefu wa elimu nao unasababisha watu kutozingatia sheria na hivyo kuongeza idadi ya watu wanaothirika na uvutaji wa sigara nchini. 

Kuonjaonja kulivyojenga tabia ya uvutaji

Licha ya kuwa wengine huishia kuvuta moshi wa sigara kutoka kwa wavutaji, kwa baadhi ya watu, hali hiyo ndiyo ilikuwa mwanzo wa historia yao ya uvutaji wa sigara na kuwafanya kuwa wavutaji wa sigara waliokubuhu.

Kwa mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, Masenyi Benjamini, uvutaji wake wa sigara ulianza kama ilivyo udadisi wa paka anayetafuta kujua ndani ya mtungi kuna nini.

Benjamin amesema, katika kibanda chake ambacho huuza sigara na bidhaa nyingine za kila siku, watu mbalimbali huenda kununua sigara na kuvutia pale pale. Hali hiyo ilimsababisha kutaka kujua starehe wanaoyoipata kwani kuvuta moshi pekee hakukumtosha.

“Walikuwa wanakuja kununua nawaona wanavuta, moshi wanapuliza hadi kwangu na mimi nikaona nivute nione wanachosikia,” amesema Benjamini.


Soma zaidi


Adhabu bila hatia

Wakati shughuli za maisha zinazowafanya watu kufikiwa na moshi wa tumbaku bila kupenda zikiendelea,  uvutaji huo huwasababishia watu wengi madhira ya kiafya mbali na saratani ambayo inajulikana kuwa adhabu ya matumizi ya tumbaku.

Kwa mujibu wa Daktari kutoka Zahanati ya Sarib iliyopo Kinyerezi Dar es Salaam, Dk Ambilikile Malango, mtu ambaye anavuta moshi wa sigara kutoka kwa mtumiaji wa tumbaku yupo kwenye hatari ya kuathirika zaidi ya hata yule ambaye anavuta bidhaa za tumbaku moja kwa moja.

Athari hizo ni pamoja na kuwashwa, kichefuchefu, uchovu na kukosa hamu ya chakula.

“Moshi wa sigara unapoingia mwilini unaenda kwenye mapafu na mfumo wa damu hiyo itasababisha saratani ya moyo, changamoto ya macho, na kwa ambao hawana watoto, ni chanzo cha ugumba,” amesema Dk Malango.

Zaidi, hali huwa mbaya zaidi kwa wajawazito na watoto ambapo Dk Malango amesema kuvuta moshi wa tumbaku kunaweza kumfanya mama mjamzito kupoteza mtoto wake na hata akijifungua, mtoto anaweza kuwa na magonjwa kama pumu.

“Watoto wengi kwa sasa wanazaliwa kabla ya wakati na wengi wao wanalia mara moja tu ukichunguza, wanakuwa na changamoto ya mapafu,” amesema Dk Malango.

Nini kifanyike?

Mtaalamu huyo wa afya ameshauri endapo utakaa na mtu ambaye anavuta sigara au bidhaa ya tumbaku inayotoa moshi, mwambie aende mbali na wewe kabla hata hajaiwasha bidhaa hiyo.

“Siyo sigara tu moshi wowote una madhara kwa binadamu hata ule unaotokana na kuchoma taka taka za nyumbani,” amesema Dk Malango.

Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani kwa upande wa Tanzania (GATS) imeainisha mikakati mbalimbali ambayo inaweza kutumia kupunguza matumizi ya sigara ikiwemo yasiyo ya hiari kwa kuzuia matangazo ya sigara na kuongeza bei ya bidhaa hiyo.

Utafiti huo umependekeza kuwa katika maeneo ya wazi ikiwemo migahawa na sehemu za kazi, uvutaji wa sigara uzuiliwe kabisa na kusiwe na hali yoyote ya kuruhusu vitendo hivyo kufanyika hata kama kuna mifumo mizuri ya kupitisha hewa. 

Enable Notifications OK No thanks