Zingatia haya kabla haujaamua kujichora “tatoo”

June 3, 2021 7:18 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Zingatia ukubwa wa tatoo na sehemu takayoichora mwilini.
  • Jiandae kisaikolojia kutokupokelewa baadhi ya sehemu.
  • Fahamu kwa uwazi dhumuni lako na mtu anayekuchora tatoo.

Dar es Salaam. Uchoraji wa “tatoo” ni kitu maarufu miongoni mwa vijana na watu wazima kote ulimwenguni. Watu huchora sanaa hizo kwenye ngozi wakiwa na madhumuni mbalimbali ikiwemo kumbukumbu na urembo.

Mapokeo ya kitendo hicho katika jamii yanatofautiana kutoka mtu na mtu hadi jamii na jamii. Kwa baadhi, tatoo huenda mbali zaidi ya urembo na kuhusishwa na tabia za mtu au imani huku wengine ikiwa ni urembo tu.

Mkazi wa Dar es Salaam Godlisten Godson amesema kuchora tatooo ni kati ya vitu ambavyo anajutia maishani mwake kwani kila kukicha, anakutana na kikwazo kipya.

“Nilikuwa kijana hivyo kwangu niliona niko sawa. Kwa sasa imenikwamisha mambo mengi sana na kwa baadhi wanashindwa hata kunichukulia kama mtu ninayeweza kuwa na mawazo mazuri au ushauri,” amesema Godson.

Kwa kijana huyo, tatoo yake imemkwamisha kupata ajira na imemlazimisha kuvalia mavazi yanayofunika mwili wake hasa anapoenda katika ofisi mbalimbali.

“Shida siyo tatoo, shida ni ilipochorwa na usanifu wa mchoraji,” amesema kijana huyo ambaye alichora picha ya nyoka katika mkono wake wa kulia na picha ya kitu kinachofanana na mwewe katika mkono wa kushoto.

Tangu kuchorwa tatoo hiyo imekuwa kikwazo kwake na ilifika kipindi hata baadhi ya rafiki zake walianza kumnenea mambo mabaya.

“Sijui ni kwanini, lakini nahisi picha ya nyoka ndiyo iliwafanya wahisi nimeanza kuabudu mashetani. Hata wazazi wangu hawakuwa na amani na tatoo zangu,” amesema Godson.

Kuna mishawasha mingi inayoambatana na ujana ya kutaka kujaribu kila kitu kilichopo duniani ikiwemo pombe, madawa ya kulevya na mambo mengine ikiwemo kuchora tatooo. 

Hata hivyo, kwa baadhi, maamuzi yao huwatokea puani mbeleni kujikuta watu waliojaa majuto. Kuepukana na changamoto kama yake, haya ni mambo ya kuzingatia unapoamua kuchora tatoo.

Kabla ya kuchora tatoo, fikiria kazi ambayo utahitaji kuifanya mbeleni kama inakubaliana na tatoo. Picha| Improb

Dhumuni la kuchora

Wapo ambao huandika majina ya watu wao wa karibu ikiwemo wazazi, wapenzi na marafiki. Kabla ya kuchora, unashauriwa kuwa na uhakika kuwa hakuna ambacho kitakuja kati yako wewe na unayeandika jina lake mwilini mwako.

Neema Swai, mfanyabiashara mkoani Kilimanjaro, tatoo haina shida ilimradi aliyenayo akiwa na amani na alichokifanya.

“Unakuta mtu amechora tatoo isiyofutika ya jina la mpenzi wake ambae wameshaachana au walichora tatoo fulani pamoja. Sasa haifutiki na analazimika kubaki na kumbukumbu inayomuumiza,” amesema Swai.

Binti huyo ameshauri kuwa pale mtu anapoamua kuchora tatoo hasa ya maandishi ni heri akaandika kitu ambacho hautojutia mfano majina ya wazazi, mtoto na mahusiano mengine ambayo ni ya kudumu.

Usanifu wa mchoraji

Unaweza ukawa na picha nzuri kichwani jinsi tatoo yako unapenda iwe na ionekane mwilini mwako lakini utakachopewa na msanifu wako ikawa ni tofauti kabisa na matarajio.

Inashauriwa ili kuepuka majuto, hakikisha unaona baadhi ya kazi ambazo mchoraji uliyemchagua amefanya awali kabla ya kumkabidhi ngozi yako aifanyie sanaa ambayo itadumu na mwili wako.

Hilo litakuepushia kuwa na tatoo ambayo imekosewa na ulazima wa kutumia gharama kubwa kuirekebisha au kuifuta.


Soma zaidi:


Sehemu unayochora tatoo yako

Wapo wanaochora tatoo mikononi, mapajani, miguuni na sehemu zingine za mwili ikiwemo usoni. Chaguo la wapi uchore tatoo yako linatoa nafasi ya kuonyesha tatoo hiyo kwa watu wengine au laa.

Kwa baadhi ya watu, tatoo zimekuwa kikwazo kwao kupata ajira katika ofisi mbalimbali hasa ambazo zimechorwa katika sehemu zinazoonekana.

Meneja Rasilimali Watu kutoka moja ya kampuni jijini Dar es Salaam, Elvira Cyprian amesema kupata ajira kwa mtu mwenye tatoo zinazoonekana inategemea na utamaduni na dhima ya kampuni.

Kwa makampuni ya kimataifa, mengi hayajali muonekano wala mavazi ya mtu ilimradi anafikia lengo na kutimiza majukumu yake.

“Unaweza kuweka rangi yoyote kwenye nywele, kuvaa nguo fup, ndefu na hata ukawa na tatoo na wasijali. Kwa kampuni za nyumbani, lazima wakufikirie mara mbili,” amesema Cyprian.

Mtaalamu huyo amesema waajiri huwaza kama kijana huyo atapokelewa vyema na watu ambao kampuni inawahudumia kwani huwa ni watu wa rika, tamaduni na imani tofauti.

Ukubwa wa tatoo unayochora

Vijana husema “mwili ni wangu usinipange matumizi” na hivyo huamua kufanya wakitakacho ikiwemo kuchora tatoo katika sehemu kubwa ya mwili. Lakini maneno hayo huyeyuka pale majuto yanapoanza. 

Mtaalam wa rasilimali watu kutoka kampuni ya TopTarget, Victoria Mabuba amesema ukubwa wa tatoo wanazochora watu mwilini unaweza pia kuwanyima ajira vijana katika baadhi ya fani.

Kwake kama afisa mwajiri, amesema tatoo haina neno ilimradi siyo ya mwili mzima au kuchukua sehemu kubwa ya mwili japo kwa Tanzania, mtu mwenye tatoo huchukuliwa kwa dhana tofauti hasa maofisini.

“Inaweza kumsababisha mtu kukosa ajira. Watu wenye tatoo huchukuliwa kama watu ambao hawapo sawa,” amesema Mabuba. 

Baadhi ya vijana wamekosa fursa za ajira kutokana na ukubwa wa tatoo walizochora. Picha| Adrenaline tatoo.

Jiandae kisaikolojia 

Kabla ya kuamua  kujichora, unatakiwa kujiandaa kisaikolojia kuwa zipo baadhi ya fursa ambazo utazikosa na baadhi zitakuwa upande wako.

Mkufunzi wa waajiriwa na waajiri, Moses Samora amesema, unatakiwa kuwa tayari kuonekana mtu wa tofauti na changamoto zingine nyingi. 

Amesema mtu anatakiwa kujua kuwa maamuzi yake yanaambatana na faida na hasara zake kwani licha ya kuwa na furaha kwa kutimiza adhma yake, ajue kuna mahala hatokaribishwa.

“Ningemshauri asubiri asijichore kwa sasa. Kama ni lazima basi achore yenye kuweza kufutika,” ameshauri Samora.

Mbali na hayo yote, ni muhimu kufahamu kuwa, kuchora tatoo ni vile saikolojia ya mtu inavyomtuma na hakuna uhusiano wa tatoo ya mtu na uwezo wake wa kufanya kazi au imani yake. 

Hata hivyo, vijana wanashauriwa kuzingatia picha wanazozichora na maana zake.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW