Rais Samia: Chukueni tahadhari Covid-19 isipukutishe Tanzania
- Rais Samia ashangaa kuona watu wachache katika mkutano wake wakiwa wamevaa barakoa.
- Asema wimbi la tatu la Uviko-19 lipo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha hadi Dodoma.
Dar es Salaam. Katika jitihada za kuendelea kuokoa maisha dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19), Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kutopuuza tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya ili kuzuia janga hilo “lisipukutishe” watu nchini.
Rais Samia amewaambia wakazi wa Kibaigwa mkoani Dodoma kuwa ameona watu wengi waliokuwa wamehudhuria mkutano wake hawajavaa barakoa ili hali wameshaambiwa na wataalamu wa afya kufanya hivyo katika mikusanyiko.
“Nimetizama hapa ninaowaona wameziba midomo na pua ni kidogo sana, nataka niwaambie tuchukue tahadhari zote dhidi ya maradhi ya corona,” amesema Rais Samia ambaye ameingia mkoani Morogoro katika ziara ya kikazi ya siku mbili. Huu ni mkoa wa pili kwa kiongozi huyo kufanya ziara rasmi ya kikazi tangu aingie madarakani Machi 2021 baada ya kuzuru Mwanza mwezi uliopita.
“Hili wimbi la tatu lipo kwenye nchi yetu na hakuna la kuficha tayari tuna wagonjwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, na mikoa mingine. Hata Dodoma kwa kiasi kidogo sana lakini wapo,” ameongeza Rais Samia ambaye miezi mitatu ya hivi karibuni ameimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Nawasalimia: Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wakazi wa Morogoro mjini waliojitokeza kumpokea Julai 7, 2020 ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo. Picha|Ikulu.
Kiongozi huyo wa juu wa nchi amewasihi Watanzania kufuata tahadhari zote zinazoshauriwa na mabwana afya “ili wimbi la tatu linalopukutisha kwa wenzetu lisije kupukutisha hapa kwetu.”
“Niwaombe sana tuchukue hadhari kwa sababu gonjwa hili likianza kutuangusha linakuwa halina kusimama linapukutisha tu. Kwa hiyo tujikinge na balaa hiyo,” amesema Rais Samia.
Tangu aingie madarakani baada ya kifo cha Rais John Magufuli Machi 17 mwaka huu, Rais Samia amefanya mabadiliko makubwa katika sera za kukabiliana na janga la Uviko-19 ikiwemo kuunda kamati ya wataalamu wa afya kushauri namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mapema juma lililopita aliwaeleza wahariri wa habari jijini Dar es Salaam kuwa tayari kulikuwa na wagonjwa zaidi ya 100 wa Uviko-19 huku 70 kati yao wakipata matibabu ya gesi ya oksjeni, ikiwa ni mara ya kwanza kutangazwa kwa takwimu mpya za wagonjwa tangu Mei, 2020.
Hadi Julai 7, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Uviko-19 ulikuwa umeshagharimu maisha ya watu zaidi ya milioni 3.9 huku visa zaidi ya milioni 184.1 vikiripotiwa ulimwenguni kote.
Licha ya Rais Samia kutangaza wagonjwa 100 wapya wiki iliyopita, takwimu za Uviko-19 za Tanzania katika tovuti ya WHO zinaonyesha kuwa bado kuna visa 509 na vifo 21, kiwango ambacho hakijabadilika tangu Mei mwaka jana.
Latest
