Netflix yatambulisha kifurushi kipya cha chini ya Sh10,000
- Mpango huo utanufaisha zaidi watu wenye simu janja za mkononi na wenye uchumi wa chini.
- Gharama yake ipo chini ya Sh10,000.
Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za filamu mtandaoni ya Marekani ya Netflix imetangaza mpango mpya kwa ajili ya watu wanaotumia simu janja kuangalizia filamu utakaoshuhudia ongezeko la kifurushi kipya kitachotoza chini ya Sh10,000 kwa mwezi.
Kifurushi hicho kipya cha nne kinachojulikana kama “Mobile Plan” kitakuwa na gharama ya chini zaidi kuliko vifurushi vingine.
Kifurushi kipya cha Mobile Plan kinagharimu Dola 3.88 ambayo ni sawa na Sh9,250 na hivyo huenda ikaongeza watumiaji wa mtandao wa Netflix wenye kipato cha chini kutokana na unafuu wa gharama ikilinganishwa na gharama za vifurushi vilivyokuwepo awali.
Kabla ya Mobile Plan, mtumiaji wa Netflix alihitaji walau kianzio cha Sh18,530 kuwa na akaunti katika mtandao huo ambapo kwa gharama hiyo alikuwa na uwezo wa kutazama filamu kwenye simu au kompyuta na televisheni.
Gharama hiyo (Sh18,530) ni ya kifurushi kilichokuwa cha chini zaidi kinachojulikana kama “Basic”. Kifurushi hicho pia kiliruhusu kutazama filamu kwenye skrini moja.
Vifurushi vingine ni ‘Standard’ ambayo gharama yake ni Sh23,170 ambacho mtumiaji wake anaweza kutumia akaunti hiyo kwenye skrini mbili iwe simu, kompyuta au televisheni.
Kifurushi cha juu zaidi ni ‘Premium’ ambayo mtumiaji wake anaweza kuangalia filamu kwenye skrini nne kwa gharama ya Sh27,800.
Kifurushi kipya kinafanyakazi kwenye simu janja pekee. Picha| Africa Inc.
Kwa Mtumiaji wa mtandao wa Netflix, Caroline Kabogo amesema kuanzishwa kwa kifurushi hicho ni ahueni kwa kuwa zamani ujumbe wa kuwa amekatwa zaidi ya Sh10,000 ulikuwa unamfikirisha kufunga akaunti yake.
Kwa mpango mpya ambao gharama zake ni nafuu, Kabogo amesema atahamia kwenye mpango huo.
“Kama ni chini ya Sh10,000 ni afadhali kwa kweli. Nlikuwa sijui hata naona nitahamia hicho,” amesema Kabogo.
Hata hivyo, chungu ya kifurushi cha Mobile Plan ni kuwa kinatumika kwenye simu tu na ni kwenye skrini moja.
Ujio wa kasi wa Netflix unazidi kutoa ushidani kwa huduma za filamu za maudhui ya Tanzania mtandaoni hususan Bongo Movie ikizingatiwa kuwa hadi sasa hakuna filamu ya Kiswahili au iliyoanzia Tanzania ambayo imefanikiwa kupenyeza mtandaoni humo.
Wewe unadhani Mobile Plan itakunufaisha? Acha maoni yako kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii kupitia @NuktaTanzania
Latest