BoT yatangaza hatua tano kukuza mikopo, kupunguza riba Tanzania

July 27, 2021 9:54 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • BOT imeziweka hadharani hatua zilizochukuliwa ili kukuza sekta binafsi nchini.
  • Hatua hizo ni pamoja na kupunguza kiasi cha riba na ukomo wa uzoefu wa kibiashara kwa wanaohitaji uwakala wa kibenki.
  • Zimelenga kuchochea urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi ili kukuza uchumi.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imechukua hatua tano za kisera kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kupunguza riba ikiwemo kuanzisha mfuko wa Sh1 trilioni kwa ajili ya kukopesha benki na taasisi za fedha kwa riba ya asilimia 3. 

Hatua hizo za BoT ni sehemu ya jitihada za Serikali kukuza uchumi baada ya kuathiriwa na ugonjwa wa virusi vya korona (Uviko-19). 

Gavana wa BOT, Prof Florens Luoga amewaambia wanahabari jijini Dodoma kuwa hatua ya kwanza iliyochukuliwa kuanzia leo Julai 27 ni kupunguza kiwango cha sehemu ya amana za mabenki kinachotakiwa kuwekwa BoT.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Prof Luoga, nafuu hiyo siyo kwa benki zote bali zile ambazo zitatoa mikopo kwa sekta ya kilimo kulingana na kiasi cha mkopo kitakachotolewa.

“Benki itakayonufaika itatakiwa kutoa mikopo kwa sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka,” amesema Prof Luoga huku lengo la hatua hiyo ikiwa ni kuongeza mikopo katika sekta ya kilimo na kupunguza riba katika mikopo itakayotolewa.

Mbali na hatua hiyo, BoT imeanzisha mfuko maalum wa kukopesha benki na taasisi za fedha ili ziweze kukopesha sekta binafsi wenye thamani ya Sh1 trilioni ambao utatumika kuzikopesha taasisi hizo kwa riba ya asilimia 3. 

“Benki au taasisi ya fedha itakayofaidika na mfuko huu itatakiwa kukopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hatua hii itaongeza ukwasi na kupunguza riba za mikopo kwa sekta binafsi,” amesema Prof Luoga. 

Gavana wa BOT, Prof Florens Luoga amewaambia wanahabari jijini Dodoma kuwa hatua hizo zinalenga kuchochea urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi ili kukuza uchumi. Picha| BOT.

Hatua nyingine iliyochukuliwa ni kulegeza masharti ya usajili wa mawakala wa benki ambapo sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa uwakala limeondolewa. 

Kwa mujibu wa BoT,  hali hiyo itachochea uwepo wa mawakala wengi wa benki na hivyo kurahisisha huduma za kibenki kwa wananchi. 

Hata hivyo, ili mtu awe wakala, sharti lililowekwa kwa sasa ni kuwa na kitambulisho au namba ya kitambulisho cha taifa.

Mbali na hilo, ukomo wa riba kwenye akaunti za kampuni ya watoa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi umewekwa ukilingana na ule wa benki husika. 

“Riba itakayotolewa kwenye akaunti hizi haitazidi riba itolewayo na benki husika katika amana za akiba (savings deposit rate),” amesema Prof Luoga. 

Kwa mujibu wa Prof Luoga, hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za upatikanaji wa fedha kwa benki zinazotumika kukopesha, hivyo kuchangia kupunguza riba za mikopo.

Katika hatua ya tano,  BOT imepunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo ikilenga kusaidia benki za biashara kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi kuliko ilivyokuwa awali.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa mbalimbali ulimwenguni ambayo uchumi wake uliathiriwa na Uviko-19 kiasi cha kushusha kasi ya ukuaji wake uliokuwa umedumu kwa wastani wa asilimia 7 kwa zaidi ya muongo mmoja. 

Uviko-19 ulichangia kasi ya ukuaji wa uchumi Tanzania kushuka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2019 hadi asilimia 4.8 mwaka 2020, kiwango cha chini kurekodiwa katika kipindi hicho. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW