Mifuko kutoboka: Mfumuko wa bei wapanda kwa miezi miwili mfululizo
- Umepanda tangu mwaka unaoishia Juni mwaka huu.
- Umepanda hadi kufikia asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia Julai 2021 kutoka asilimia 3.6 iliyorekodiwa Juni mwaka huu.
- Umechangiwa zaidi na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma Tanzania imepanda hadi kufikia asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia Julai 2021 kutoka asilimia 3.6 iliyorekodiwa Juni mwaka huu, ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Kasi hiyo imechangiwa zaidi na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula ikiwemo unga wa ngano.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa Agosti 8, 2021, baadhi ya bei za vyakula ambazo zimepanda ni pamoja na ngano kwa asilimia 6.5, unga wa ngano (asilimia 6.1) na nyama kwa asilimia 3.7.
Bidhaa zingine za vyakula ambazo zimepanda bei ni viazi mviringo kwa asilimia 7.9, viazi vitamu (asilimia 8.4) na mihogo mibichi kwa asilimia 6.4.
“Kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupanda kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nguo za wanawake kwa asilimia 6.4, viatu vya wanaume kwa asilimia 7.1, viatu vya watoto kwa asilimia 6.4 na kodi ya pango kwa asilimia 4.9,” inaeleza taarifa ya NBS iliyotolewa leo Agosti 9, 2021.
Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2021 umeongezeka hadi asilimia 5.1 kutoka kwa asilimia 4.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021.
Huenda ikawa ni maumivu kwa watumiaji wa bidhaa nchini ikizingatiwa kuwa mfumuko wa bei umepanda mfululizo kwa miezi miwili mfululiz, jambo linalowafanya kutoboa zaidi mifuko yao ili kuzipata.
Kwa mujibu wa NBS, kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2021ilipanda hadi kufikia asilimia 3.6 kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2021.
Kasi hiyo ilichangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula vikiwemo vitambaa vya nguo na mavazi ya wanawake.
Latest
