Mafuriko yalivyorudisha nyuma vita ya kufuta ujinga Kigoma
- Shule iliyowahi kuandikisha hadi wanafunzi 240 yazingirwa na maji kwa zaidi ya mwaka.
- Wanafunzi wahamishiwa kwenye shule ya dharura ili kuendeleza masomo yao.
Kigoma. Walikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa elimu ya msingi Tanzania waliokuwa na shule yenye majengo mazuri, imara yenye milango na madirisha madhubuti.
Walioanza masomo katika shule hiyo wakati wote walikuwa na uhakika wa kumalizia elimu yao hapo ili wapate tiketi ya kujiunga na sekondari.
Ndani ya mwaka mmoja tu mambo yamebadilika. Wanafunzi hawa wa Shule ya Msingi Mgumile katika Manispaa ya Kigogo Ujiji hawasomi tena katika majengo yenye kuta imara za matofali, zilizosakafiwa na kuwekwa milango.
Shule yao iliyokuwa mita 10 tu kando kando mwa Ziwa Tanganyika haifai tena. Kwa sasa ni sehemu ya makazi ya muda ya baadhi ya wavuvi baada ya sehemu ya kijiji chao kuzingirwa na maji kutokana kuongezeka kwa kina cha maji cha ziwa hilo lilipo Magharibi mwa Tanzania.
“Bado naikumbuka shule yetu,” anasema Magreth Leonard (11) mwanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo iliyopo kata ya Kagera.
“Maji yalianza kuingia darasani kwetu…shuleni tulienda kwa muda mfupi tu wakasema tuhame,” anasema binti huyo huku akionyesha uelekeo ilipokuwepo shule yao.
Baadhi ya rafiki zake ambao wazazi wao wana uwezo, kwa mujibu wa Magreth, walihamishwa kutokana na changamoto hiyo.
Kwa sasa ili ufike shule aliyokuwa anasoma Magreth unahitaji mtumbwi utakaokusaidia kuvuka maji yaliyovamia sehemu ya mtaa huo kwa takriban dakika 25 kwa kupita pembezoni mwa michikichi na makazi ya watu yaliyozungukwa na maji.
Madarasa ya Shule ya Msingi ya Mgumile ambayo imeathiriwa na mafuriko na sasa haitumiwi tena na wanafunzi kwa sababu imezingirwa na maji. Picha| Gift Mijoe.
Rasilimali zote za umma zilizokuwa karibu na shule hiyo zikiwemo nyumba mbili za walimu na zahanati zote zimezingirwa na maji.
Julius Robert, mjumbe wa Serikali za mtaa hufanya doria kila wiki na mtumbwi wake kuhakikisha mali hizo yakiwemo mabati, madirisha ya vioo na milango haviibwi.
Mratibu wa Elimu wa Kata ya Kagera, Salvatory Meshack anasema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2003 ilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 300.
Baada ya maji kuzingira sehemu ya eneo la mtaa huo uliopo nje kidogo ya mji, Manispaa ya Kigoma/Ujiji ilijenga shule ya dharura katika eneo ambalo lipo juu kidogo.
Shule hiyo mpya yenye madarasa tisa na ofisi moja imejengwa kwa kuzungushiwa mabati yaliyopigwa kwa urefu wa mita moja hivi. Madarasa haya hayana milango na ndani hayajipigwa sakafu zaidi ya kuwa na ubao tu wa kufundishia.
Licha ya kuwa Serikali imejenga shule hiyo kwa dharura, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Sikulama Jumanne anasema wakati wa mvua maji huingia katika darasa hilo na kufanya wanafunzi wengi kukimbilia madarasa mengine.
Changamoto kama hizo, Sikulama anasema, kuna wakati zinapunguza muda wa masomo yao hasa nyakati za upepo mkali na mvua.
“Hapa tunapata shida sana ya maji kwa ajili ya matumizi ya shule, tunayachota mbali tunatembea hadi dakika 15 kwenda kisimani,” anasema Jumanne huku akibainisha kuwa kazi ya kuchota maji hufanywa kwa zamu.
Mbali na ukosefu wa maji unaoukumba mtaa mzima, Mwenyekiti Msaidizi wa kamati ya Shule ya Mgumile, Julius Robert anasema mabati yaliyotumika kujenga shule hiyo yameanza kuwa tishio la kiusalama kwa wanafunzi baada ya kumjeruhi mmojawapo siku za nyuma na kuwahishwa Ujiji kwa ajili ya matibabu.
“Haya mabati kwa sasa ni ajali hususan kwa watoto wadogo ambao ni watundu sana,” anasema Robert. “Tunaomba wabadilishe kuokoa maisha yao.”
Mbali na malighafi zilizotumika kujengea kuwa tishio kwa usalama, Robert anasema vyoo vilivyojengwa ni vya muda mfupi na hakuna nyumba za walimu jambo linalowafanya watumishi hao kusafiri kila siku za wiki kutoka mitaa mingine ya Kigoma/Ujiji walipopanga kuja Mgumile.
Shule ya dharura ya Mgumile ambayo inatumiwa na wanafunzi baada ya awali kufurikwa na mafuriko. Picha| Gift Mijoe.
Tofauti na mitaa mingine ya kata za manispaa hiyo, Mgumile umejitenga na unahitaji ufike kwa ama kwa kutembea kwa miguu au kwa kutumia bodaboda kwa kuwa hakuna barabara zinazowezesha magari kuingia kwa urahisi.
Kabla ya kufika huko kwa bodaboda, mwalimu atahitaji kulipa Sh200 kwa siku kuvuka Mto Rwiche na mtumbwi. Wenyeji wanasema mto huo una mamba na viboko.
Nauli ya bodaboda kutoka makao makuu ya kata ya Kagera hadi Mgumile, kwa mujibu wa Kandege Suleiman dereva wa bodaboda, ni Sh7,000 wakati wa kiangazi na Sh10,000 wakati wa masika. Ni mwendo usiozidi nusu saa lakini katika njia nyembamba yenye matope na inayoweza kupitisha watu na bodaboda pekee.
Watoto na walimu hao wanaendelea kutaabika kwa takriban mwaka sasa tangu shule hiyo ya muda ilipotengenezwa licha ya wakazi wa mtaa wa Mgumile kueleza kuwa wapo tayari kuchangia kujenga shule hiyo na sehemu nyingine kumaliziwa na Serikali.
Ofisa Mtendaji wa kata ya Kagera Nuru Isote ameiambia Nukta Habari kuwa hakuna matumaini kuwa maji yaliyofunika sehemu ya mtaa huo yakatoweka na kuifanya shule hiyo kuanza kutumika tena.
Ili shule ya kudumu ijengwe katika eneo hilo, Serikali itahitaji kumalizana na mwenye eneo aliyejitolea ardhi wakati wa janga hilo ili wanafunzi angalau waendelee na masomo.
Serikali inaeleza kuwa inafahamu hali inayoikumba Shule ya Msingi Mgumile na huduma nyingine za kijamii na kwamba ilishaanza jitihada za kuboresha hali hiyo ili watoto wasome katika maeneo tulivu.
“Muda wote ambao watoto walikuwa wakitaka kwenda shuleni walikuwa lazima wapite kwenye maji na kule kuna mamba na viboko na wadudu wengine hatarishi kwa watoto wetu…tulitafuta eneo katika mtaa huo ambalo lipo juu tukajenga vyumba vya muda tisa na kuhakikisha tumewahamisha watoto wetu ili waendelee na masomo,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Frednand Fillimbi.
Mtendaji huyo wa manispaa anasema baadhi ya walimu waliokuwa na nyumba katika eneo lililofurika walitafutiwa nafasi kijijini hapo ili waweze kuendelea kutoa huduma ya kufindisha watoto.
“Mbali na hatua za dharura tumeshaiandikia Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Maafa kuomba msaada namna ya kupata fungu la kujenga shule ya kudumu kwa sababu itahitaji gharama kubwa na bajeti ya halmashauri kwa mwaka husika haikutengwa kwa ajili ya ujenzi mpya,” anasema Fillimbi.
Kwa sasa, anasema, ngazi za juu zinafanyia kazi suala la shule hiyo ya Mgumile ili kujenga shule ya kudumu nje ya eneo lililofunikwa na maji.
Latest
