Manahodha wakwepa mamba wanaoipiga jeki elimu Tanzania

December 13, 2021 3:31 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni watoa huduma ya usafirishaji watu na mizigo kwa kutumia mitumbwi mkoani Kigoma.
  • Wanawavusha bure wanafunzi katika Mto Ruchwe kwenda kupata elimu.
  • Wenyewe wasema kazi hiyo ni huduma ya kujitolea licha ya kuwa mto wanaofanyia kazi kuwa na mamba, viboko.

Kigoma. Akiwa na miaka 22 tu, Ally Ramadhan alijitosa kuanza kutoa huduma ya usafirishaji kwa kutumia mtumbwi katika Mto Rwiche uliopo pembezoni mwa Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Tofauti na wenzie wa Ziwa Tanganyika wanaofanya safari ndefu za zaidi ya kilomita moja, yeye safari yake haizidi umbali wa mita 15.

Lakini safari ya Ramadhan mkazi wa Kasimbu katika manispaa hii si rahisi kihivyo. Mto huo ambao amekuwa akitoa huduma ya kuvusha watu na mizigo kwa miaka 25 sasa, unasifika kwa kuwa na mamba na viboko.  

Licha ya vihatarishi vya kazi yake, Ramadhan na wavushaji wenzie ni miongoni mwa watoa huduma za usafirishaji katika kivuko cha Kabogo ambao wanapendwa na kusifiwa na wakazi wa manispaa hii kwa “huruma yao”.

Tofauti na daladala ambao si rahisi kusafirisha abiria wakiwemo wanafunzi bila nauli, kwa Ramadhan na wenzie kazi yao ni huduma ambayo hailengi kujipatia fedha pekee.

‘Kazi ya kujitolea’

“Hii ni kazi ya kujitolea tu, huwezi kumwacha binadamu mwenzio asivuke kwa kuwa hana pesa,” anasema Ramadhan huku akisogeza mtumbwi wake nchi kavu kwa ajili ya mahojiano bila ya kuvaa mavazi ya kujiokoa (Life jacket).  

Ally Ramadhan akiwa katika majukumu yake ya kuvusha abiria na mizigo katika kivuko cha Kabogo katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji. Kazi hiyo ameifanya kwa miaka 25 sasa. 

Kwa kawaida abiria yeyote anayetaka kuvuka katika eneo hilo kutoka Mtaa wa Mgumile kwenda Ujiji anatakiwa kulipa Sh100 kwa safari moja huku pikipiki zikitozwa Sh1,000 na dereva wake kwenda na kurudi.

Hata hivyo, ni kawaida tu kwa wakazi wa maeneo haya kwenda kivukoni bila fedha na wakapata huduma ya kwenda na kurudi.

Miongoni mwa abiria walionufaika kwa muda mrefu ni wanafunzi wanaosoma ama katika Shule ya Msingi Mgumile ama shule nyingine katika manispaa hiyo.

Pamoja na kuwa shule zilikuwa zimefungwa mwishoni mwa Juni, kutokana na mazoea ya kusafiri bure, watoto watatu tunakutana nao pembezoni mwa mto wakisubiri kuvuka kwenda Mgumile bila ya kuwa na nauli huku wakiwa na mizigo yao kichwani.

Wasafiri bila nauli

“Naenda shamba lakini leo hatuna hela…huwa tukiwa hatuna tunasubiria wanatuita na kutuvusha bure,” anasema Esther Elia, mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Azimio.  

Kutokana na hali duni ya maisha katika baadhi ya familia, siyo rahisi kwa mzazi kumpatia mwanafunzi Sh200 kwa ajili ya usafiri wa mtumbwi kila siku kabla ya gharama za chakula.

Mkoa wa Kigoma ni mkoa wa pili kwa umaskini Tanzania ukiwa nyuma ya Kagera, kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Takwimu za awali  zilizotolewa na NBS hivi karibuni kwenye kitabu cha takwimu muhimu mwaka 2020 (Tanzania in Figures 2020)  zinabainisha kuwa wastani wa pato la mtu kwa mwaka Kigoma mwaka 2020 ulikuwa Sh1.48 milioni ukiwa juu kidogo ya nusu ya wastani wa kitaifa wa Sh2.65 milioni.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mgumile, Pius Saboya aliiambia Nukta kuwa familia nyingi haziwezi kumudu gharama za kila siku kuvusha watoto na mtumbwi kwa kuwa hakuna daraja.

“Baada ya shule yetu kuzingirwa na maji baadhi ya watoto walihamishiwa shule nyingine za manispaa na kutakiwa kuvuka mto. Ule mto una mamba na viboko…tuliongea na manispaa kuhusu hili na mkurugenzi sasa anawalipia wanafunzi wote nauli za kuvuka na mitumbwi,” anasema.

Mapato hayaendani na uzito wa kazi

Pamoja na wanakijiji kujua kuwa Serikali inawalipia watoto wao kuvuka mto huo, ukweli ni kuwa kiwango wanachopata wavushaji hao hakiendani na kazi kubwa ya wanaofanya ambao kwa sasa wanafikia 21.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji Frednand Filimbi anasema baada ya kubaini shida wanayopata wanafunzi hao walianza kuwalipa wamiliki wa mitumbwi Sh3,000 kwa mwezi kwa kila mwanachama kuwachangia gharama za usafiri.

Kwa kuwa wamiliki nao ni wazazi, Fillimbi anasema, walikubaliana kuendelea kutoa huduma kwa kiwango hicho anachokiri kuwa hakiendani na thamani ya utoaji wa huduma husika.

“Nawashukuru wamiliki wa mitumbwi, kile tunachowalipa si kweli kwamba ndiyo gharama zenyewe kwa hiyo sehemu kubwa ni mchango wao wananchi wa eneo lile,” anasema Filimbi.

Waendesha pikipiki ni moja ya wateja wakuu wa manahodha hawa wa mitumbwi katika manispaa hii. 

‘Tuliwahi kuwasubirisha wanafunzi’

Licha ya kuwa wapo tayari kujitolea kuvusha wanafunzi, Ramadhan anakiri kuwa kuna wakati walikuwa hawawapi kipaumbele wanafunzi hao ili kupata fedha kidogo kutoka kwa abiria jambo lililokuwa likiwachelewesha masomo.

“Tumefanya kazi hii ya kujitolea kwa miaka mingi, tunashukuru angalau mkurugenzi ametukumbuka,” anasema Ally.

Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa mitumbwi katika kivuko cha Kabogo Hillary Ninga anasema wamekuwa wakitoa huduma kwa wanafunzi hao tangu ianzishwe Shule ya Msingi Mgumile zaidi ya miaka 15 iliyopita.

“Tuna matumaini wanafunzi watasoma, watapata mafanikio ya kielimu kama watapata ajira au wajiajiri, hiyo ni kwao. Sisi tunachotaka wasome vema, wafaulu na wanafanikiwe zaidi maishani,” anasema Ninga huku akijisifu kuwa kazi yao itawaletea maendeleo vijana wengi wa eneo hilo.

Kwa sasa kwa mujibu wa kiongozi huyo, wanawavusha wanafunzi watano wa Sekondari.  Uongozi wa kata ya Kagera unasema kuna zaidi ya wanafunzi 30 wa elimu ya msingi wanaopatiwa usafiri wa mtumbwi kila siku.

“Hapa tunajitolea na tunafanya shughuli nyingine za kilimo ambazo tukipata mazao yanatusaidia kupata fedha nyingine za kijikimu na maisha,” anasema Ninga, akieleza kuwa ni vigumu kujua wastani wa kipato anachopata kwa mwezi kutoka katika kazi hiyo.

Ni shughuli ya kuwakwepa mamba, viboko

Ninga na wanachama wenzie pamoja na kutoa huduma wana kazi ya ziada kuhakikisha wanajilinda na kuwalinda wateja wao dhidi ya mamba na viboko ambao kuna wakati hufika hadi kwenye kivuko chao.

“Mwaka 2006 mama mjamzito akiwa amebeba mtoto alichukuliwa na mamba na mwanaye. Tangu hapo hatujapata kadhia ya mamba kwa kuwa sehemu kubwa wapo katika eneo la mtu unapomwaga maji ziwani,” anasema na kuongeza;

“Hii kazi ni hatari”.

Baadhi ya abiria wakivushwa na mtumbwi katika kivuko cha Kabogo katika Mto Rwiche. Abiria hao hutakiwa kulipa Sh200 kwenda na kurudi. Picha zote|Nuzulack Dausen/Nukta. 

Licha ya kuwa kazi hiyo inachangia kuwaingizia kipato, wamiliki wa mitumbwi hao wanasema ni vyema Serikali ikajenga daraja ili kuwawezesha wanafunzi na wakazi wa eneo hilo kuvuka na kufanya shughuli bila changamoto za usafiri.

Daraja kumaliza tatizo

Ujenzi wa daraja katika kivuko hicho, utaihitaji Serikali kutengeneza barabara kutoka Kagera ilipoishia lami hadi kufika eneo hilo na kuendelea Mgumile.

Sehemu kubwa ya wakazi wa Mgumile ni wakulima wa mpunga na michikichi na wavuvi katika Ziwa Tanganyika na Mto Rwiche ambao ni wa pili kwa ukubwa mkoani humo.

Serikali inasema kuwa kwa sasa mpango uliopo ni kujenga barabara ya lami na daraja ikiwa ni sehemu ya miradi ya Tactic itakayotekelezwa mkoani humo kuanzia mwaka wa fedha 2021/22.

“Daraja litajengwa eneo la Mto Rwiche na barabara itaendelea kuingia Mgumile ili kuhakikisha mazao yanayozalishwa huko na wananchi wanapata usafiri wa uhakika,” anasema Filimbi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW