Mabadiliko ya tabianchi: Simulizi ya mtaa unaomezwa na Ziwa Tanganyika

August 17, 2021 6:40 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mtaa wa Mgumile ambao sehemu yake imefurikwa na maji.
  • Miundombinu ya shule, zahanati na maji nayo yaharibiwa.

Kigoma. Miaka 51 iliyopita Almas Rashid alivuka Mto Rwiche na kuingia katika Kijiji cha Mgumile mkoani Kigoma ili kuanza maisha na kufanya kilimo kama shughuli yake kuu ya kiuchumi. 

Wakati huo akiwa na miaka 36 tu eneo kubwa la kijiji hicho, ambacho kwa sasa ni moja ya mitaa ya 68 ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, lilikuwa ni pori. Ni watu wachache sana waliishi katika mtaa huo ambao ulikuwa kijijini.

Mto Rwiche, ambao ni wa pili kwa ukubwa mkoani Kigoma, wakati huo ulikuwa na maji mengi na Ziwa Tanganyika lilikuwa na kina cha maji ya kawaida kisichofurika. 

Eneo la ardhi la kijiji chao lilikuwa na rutuba safi huku kukiwa na maeneo machache oevu yaliyowavutia wengi kufanya kilimo cha mpunga na michikichi. 

Kwa miaka zaidi ya 61 aliyoishi Mgumile, Rashid mwenye umri wa miaka 98 anaeleza hakuwahi kushuhudia mafuriko makubwa yaliyodumu kwa zaidi ya mwezi. 

Haijawahi kutokea

Sehemu kubwa ya mafuriko, anasema, yalikuwa ni madogo yaliyotokana na Mto Rwiche kufurika wakati wa masika na baada ya muda mfupi wa wiki tatu ama nne hivi maji yalikauka. Mafuriko hayo pia yaliathiri eneo dogo tu la kijiji chao.

Miaka 60 baadaye rasilimali nyingi alizokuwa ameziwekeza katika mtaa huo wa Mgumile zimeharibiwa na maji baada ya mafuriko ambayo hajawahi kuyashuhudia maishani mwake. 

Mafuriko hayo, yaliyotokea mwanzoni mwaka 2020, yametokana na kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kuongezeka na kufunika sehemu ya mtaa. 

“Nyumba yangu ilikuwa hapo, imezama,” anasema Mzee Rashid akionyesha ilipokuwa nyumba yake kubwa ya bati. 

Makazi ya watu katika Kijiji cha Mgumile mkoani Kigoma yaliyofunikwa na maji baada ya kuongezeka kwa kina cha Ziwa Tanganyika. Picha| Gift Mijoe.

Kila kitu chatoweka

“Mashamba yote yameharibika, hatuna namna…tunaisubiria Serikali itusaidie. Tumebaki hivi hivi, tumebaki uchi kiuchumi kama tulivyozaliwa,” Rashid anaongeza. 

Kama walivyo wakazi wengine wa mtaa huu wenye watu zaidi ya 2,000, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgumile Pius Saboya, Rashid hafahamu chanzo cha mafuriko hayo yaliyodumu kwa zaidi ya mwaka sasa kuwa ni mabadiliko ya tabianchi. 

Mabadiliko ya tabianchi husababishwa na uchafuzi wa mazingira ikiwemo ukataji miti na shughuli nyingine za kibinadamu vikiwemo viwanda. Shughuli hizo huchochea ongezeko la joto na kina cha maji baharini na ziwani.

“Suala la ziwa kujaa kwa maji kwa msimu wa 2020/21 na hata msimu uliopita lilikumba maeneo mengi hapa nchini, kutokana na mabadiliko ya tabianchi basi maeneo mengi ya ziwa yamefurikwa zaidi,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Frednand Filimbi. 

Maji hayo ya ziwa yalianza kuingia taratibu msimu wa mwaka 2019/20 lakini Aprili 2020 yalizidi zaidi na kufunika sehemu ya mtaa karibu na ziwa. 

                         

Mabadiliko ya tabianchi yaangamiza mtaa

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) liliambia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) Juni mwaka jana kuwa kina cha Ziwa Tanganyika kilikua kimeongezeka kwa mita tatu toka kiwango cha awali kutokana kuongezeka kwa joto kunakotokana na mabadiliko ya tabianchi. 

Eneo la mtaa lililofunikwa na maji tayari lilikuwa na huduma muhimu za kijamii kama shule, zahanati iliyokuwa imeshafikia hatua za mwisho za ujenzi ili ianze kutoa huduma, mradi wa huduma za maji na nyumba ya walimu. 

Mgumile ni moja ya maeneo mengi kando mwa Ziwa Tanganyika yaliyofurikwa na maji nchini Tanzania.

Ukiachana na huduma hizo, wakazi wengi waliokuwepo eneo hilo wamepoteza makazi yao na mashamba ya michikichi. 

Rukia Saidi, (65) yeye amepoteza nyumba nne zilizokuwepo karibu na msikiti wakati mzee Rashid akipoteza takriban ekari 10 za mashamba ya michikichi, mpunga na maharage. 

Kutembelea eneo lililokuwa sehemu ya mtaa kwa sasa inakuhitaji ukodi mtumbwi ambao mwendeshaji wake anatakiwa kuwa mzoefu kwa kuwa baadhi ya maeneo anapopita ni vyoo au visiki vya mashamba. 

Itakuchukua dakika 25 hivi kwa mtumbwi kutoka eneo la nchi kavu ili kufika ilipokuwa Shule ya Msingi Mgumile. Katika safari hiyo si ajabu kukutana na wakulima ambao wanavuna michikichi yao kwenye makazi hayo yaliyofurika. 

“Bado tunaendelea kuvuna michikichi, watu wengi wanaingia na mitumbwi wanapanda kwenye “migazi” (michikichi) na kuivuna,” anasema Saidi ambaye pia ni mjumbe wa mtaa wa Mgumile. Kufurika kwa maji kumefanya hata huduma nyingine za upatikanaji wa maji na huduma za afya kama ujenzi wa choo kuwa mgumu.

Rasilimali nyingi katika mtaa huo wa Mgumile zimeharibiwa na maji baada ya mafuriko ambayo wakazi wake hajawahi kuyashuhudia katika maisha yao. Shule ya Msingi Mgumile nayo imeathirika na mafuriko hayo. Picha| Gift Mijoe. 

‘Hakufai hata kuchimba choo cha kudumu’

Chausiku Chimeze (50) mkazi wa mtaa huo anasema vyoo vingi vya kisasa wanavyochimba vinatitia au kubomolewa na maji ya mafuriko kiasi cha kuwafanya wachimbe vya muda mfupi ambavyo ni hatari kwa afya yao. 

Wakati akihaha kuboresha huduma za maliwato, katika eneo hilo kwa sasa ni shida kupata maji safi na salama. Wakazi wa eneo hili wanapata maji ama ziwani, mtoni au kwenye visima vidogo vilivyo mtaani kwao ambavyo si safi na salama.

Kukwepa magonjwa ya tumbo, Chausiku yeye hununua maji safi na salama kutoka mtaa jirani wa Kitale ambako huuziwa dumu la lita 20 kwa Sh1,000. 

Kwa matumizi ya wiki tatu, hulazimika kutumia Sh5,000 kwa kuwa muda mwingi anakaa pekee yake. Kwa wenye familia, gharama ni kubwa zaidi ya hapo. 

“Hapa nipo barabarani watu wakija wanaomba maji nawapatia na maji yakiisha huwa nauza kuku nawaagiza wenye baiskeli waniletee, wasipokuwepo huwa nayanunua dukani,” anasema Chausiku. 

Mabadiliko hayo ya tabianchi yamerudisha nyuma mtaa huu ambao kwa sehemu kubwa unakaliwa na wakazi wanaojishughulisha na kilimo cha michikichi, mpunga, maharage na shughuli za uvuvi. 

Wakazi wa mtaa huu kwa kushirikiana na Serikali na waraghabibishi walikuwa wamehamasishana na kujenga huduma nyingi za kijamii na nyingine walikuwa wakiendelea kujenga. Baada ya mafuriko, sasa maisha yao yamerudi nyuma. 

‘Tumekuwa kama yatima’

Wakati naingia kwenye mtaa huu Juni 29 mwaka huu, Saboya alikuwa na wajumbe wake wanne wakijadiliana agenda za mkutano wa mtaa ambapo pamoja na mambo mengine walipanga kujadili upatikanaji wa eneo la kujenga zahanati na kuisisitiza Serikali ijenge shule ya msingi ya kudumu.

“Tumekuwa kama yatima wakati na sisi tupo ndani ya manispaa, Serikali imekaa kimya,” anasema Saboya.

“Hapa maradhi ya mlipuko yanaweza kutokea. Hatuna usafiri wa uhakika hata kwenda kupata matibabu…alitokea mama aliyekuwa anataka kujifungua ilitulazimu tumbebe kwenye machela.”

Serikali inasema mafuriko hayo yaliyotokea Mgumile na maeneo mengine ya ukanda wa ziwa ni janga na kwamba inaendelea kuboresha huduma za kijamii ili angalau wananchi hao warejee kwenye maisha yao ya awali. 

Wakazi wa kijiji cha Mgumile ambacho kimezungukwa na maji hulazimika kutumia usafiri wa mitumbwi kukatiza katika maeneo yao. Picha| Gift Mijoe.

Serikali yaanza upya kurejesha huduma

“Tuliuelekeza uongozi wa mtaa utafute eneo la kujenga zahanati, wakishalipata watoe taarifa kwa mkurugenzi ili tuanze ujenzi wa zahanati kwa sababu zahanati iliyokuwa katika hatua za mwisho za ujenzi nayo imefurikwa na maji,” anasema Filimbi akibainisha kuwa mtaa upo kwenye mazungumzo na wamiliki wa ardhi. 

Kuhusu maji, Filimbi aliiambia Nukta Habari kuwa kwa sasa wapo mbioni kupeleka huduma za maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Kigoma (Kuwasa) ambayo itatoa maji kutoka mjini kwenda Mgumile ili kuwapunguzia hatari za kiafya kutokana na ukosefu wa maji safi na salama. 

Awali Serikali ilikuwa imeshajenga vituo vya kuchotea maji na kusambaza mabomba katika mtaa huo kabla ya mafuriko. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW