Benki ya Dunia yaungana na Tanzania mapambano ya Uviko-19

September 22, 2021 5:53 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass (kushoto) akizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan jana Septemba 21, 2021 pembeni ya mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA76), New York nchini Marekani. Picha| Ikulu.


  • Imesema itasaidia juhudu za upatikanaji wa chanjo.
  • Kuendelea kuisaidia Tanzania kuinua uchumi wake.
  • Tanzania nayo yakaribisha ushirikiano huo.

Dar es Salaam. Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass ameihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa itaisaidia kukabiliana na athari za Corona (Uviko-19) na kukuza uchumi kupitia mabadiliko ya kidijitali kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Malpass ametoa ahadi hiyo alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan jana Septemba 21, 2021 pembeni ya mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA76), New York nchini Marekani.

Kigogo huyo wa Benki ya Dunia amesema benki yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika mapambano dhidi ya athari za Uviko-19 na manunuzi, utoaji na usambazaji wa chanjo. 

Aidha, Rais huyo wa Benki ya Dunia ameihimiza Tanzania kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ili kuwezesha sekta binafsi kukua kupitia mabadiliko sheria na sera.

“Rais Malpass ameelezea umuhimu upatikanaji wa umeme, nyumba za bei nafuu na miundombinu ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na kutengeneza masoko yenye ushindani,” imeeleza taarifa ya benki hiyo iliyotolewa mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo.

Pia Rais Malpass amesisitiza umuhimu wa uwazi wa madeni na uchaguzi mzuri wa programu za uwekezaji na vyanzo vyake vya mapato. 

Naye Rais Samia ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake kwa Tanzania katika huduma za jamii pamoja na mapambano dhidi ya Uviko-19.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo ili kuwaletea Watanzania maendeleo.

Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania ambapo imekuwa ikiipatia mikopo na misaada ili kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.

Mathalan, Mwaka 2019, Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ziliingia makubaliano ya kuongeza kasi ya usambazaji maji vijijini kwa kutumia mifumo ya umemejua.

Makubaliano hayo yalitokana na kusainiwa kwa mkataba ulioipatia Tanzania Dola za Marekani 4.5 milioni sawa na Sh10.3 bilioni ili kuwawezesha wananchi kutoka katika mifumo duni ya upatikanaji na usambazaji maji na kuwaletea mifumo rafiki  inayotumia pampu zinazoendeshwa na nishati ya umemejua.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV