Mwalimu Nyerere: Funzo la uongozi kwa wanawake Tanzania
- Amewafanya waongoze kwa unyenyekevu na uwajibikaji.
- Kujitathmini kama viongozi na kukubali makosa huku ukijifunza.
- Ni lama za barabara katika e safari ya uongozi kwa vijana.
Dar es Salaam. Yapo mengi ambayo Baba wa Taifa la Tanzania, alituachia mambo mengi mazuri ikiwemo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Licha ya kuacha vitu mbalimbali ambavyo kama Taifa tunajivunia kutaja jina lake, Mwalimu Julius Nyerere ni chachu ya maendeleo mbalimbali miongoni mwa vijana wakiwemo wanawake.
Wakati leo Oktoba 14 tunakumbuka kifo chake, yapo mengi ya kujifunza kutoka kwake hasa katika nyanja ya uongozi ambao ni msingi wa maendeleo kwa Taifa.
Baba wa Taifa kwa wengi ni mfano wa kuigwa na uongozi wake ni barabara ambayo baadhi ya vijana wa Kitanzania wameamua kuifuata wakiamini ni njia ya kuelekea kwenye mafanikio katika tasnia ya uongozi.
Kwa viongozi wanawake, Mwalimu Nyerere atakumbukwa kwa uwezo wake ikiwemo kusimamia ukweli, haki na kuwa kiongozi anayesikiliza Watanzania.
Licha ya kuwaaga Watanzania na dunia Oktoba 14, 1999, Mwalimu Nyerere anasherehekewa na viongozi wanawake wanaoongoza katika nyanja mbalimbali nchini Tanzania kwa namna mbalimbali.
Ni miaka 22 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Picha| The Conversation.
Unyeyekevu katika uongozi
Baadhi ya watu huuchukulia uongozi kama nguvu. Uwezo wa kufaya maamuzi na kutoa amri kwa watu ambao wanaowaongoza.
Hata hivyo, hilo halikuwa katika hulka ya uongozi wa Baba wa Taifa na badala yake, aliongoza kwa unyenyekevu huku historia yake ikiwafundisha wengine kuwa uongozi hauhusiani na uwezo wa kifedha, historia ya kiuchumi ya familia bali busara.
Balozi wa Vijana katika Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Jessica Mshama anasema Mwalimu Nyerere ni kioo cha unyenyekevu katika uongozi.
“Mwalimu Nyerere alikuwa hafanyi tu maamuzi. Alikuwa anawaita watu na kuwashirikisha. Sera zake za uongozi zinanifundisha kuongoza kwa busara na siyo kwa mabavu,” amesema Mshama ambaye pia ni mjasiriamali.
Kujiamini na kuongoza kwa misingi ya amani
Mwalimu Nyerere aliyezaliwa mwaka 1922 hakuongoza kwa ubaguzi. Awaye yeyote ilimradi ni Mtanzania, Mwafrika na binadamu, kwake alikuwa na haki sawa.
Ni jambo ambalo Mwakilishi wa Viti Maalam katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Hudhaima Mbarak Tahir amekuwa akiishi nalo katika uongozi wake.
Kwa Tahir, uwezo wa kusafiri kutoka Zanzibar na kwenda bara na kuishi na watu wa bara kwa amani bila kujali itikadi za kisiasa wala kidini ni jambo ambalo atamkumbuka daima Mwalimu Nyerere.
“Kanifundisha kuwa kiongozi mwenye unyenyekevu lakini usiopita kiasi. Nimejifunza kama kiongozi, usinyenyekee sana kiasi cha kujidhalilisha,” amesema Tahir anayeamini fursa zinazogusa maendeleo ya watu zinahitaji watu walio tayari kuzifanya.
Pale mtu anapopewa fursa ya kuongoza Watanzania na kuonyesha ulegevu, basi nafasi hiyo imfikie mtu mwenye utayari na malengo mazuri na Tanzania.
Kati ya alama kuu alizoacha Mwalimu Nyerere ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Picha| YouTube.
Kusimamia unachokiamini
Uongozi haimaanishi kila kitu unachokisema watu watakubaliana nacho. Wapo ambao watakipinga licha ya wewe kuona uwezekano wa mafanikio na maendeleo.
Sera kama za muungano, ujamaa na nyinginezo ni hamasa kwa Afisa Programu wa taasisi ya Segal Family Foundation, Carolyn Kandusi ambaye anamuenzi Mwalimu Nyerere kwa kusimamia anachokiamini.
Kandusi amesema maisha ya Mwalimu Nyerere yamemfundisha kujitathmini kama kiongozi na kufahamu kile wanachofikiria anaowaongoza kuhusu uongozi wake.
Zaidi ni kusherehekea mafanikio na kuyakubali mapungufu ambayo kama kiogozi anaweza kuwa nayo.
“Mwalimu amenifunza kuanza kila kitu kwa msingi. Katika kila ninachofanya huhakikisha nimeweka msingi mzuri kwani kama msingi wa nyumba siyo imara, ni lazima itetereke,” amesema Kandusi.
Misingi ya umoja, amani na utu vilivyowekwa na Mwalimu Nyerere ni vitu vinavyomfanya ajihisi na kujivunia kuwa Mtanzania popote alipo licha ya Mwalimu kutokuwa naye lakini anaishi katika mioyo ya watu.
Wewe unamkumbuka kwa lipi Mwalimu Nyerere?
Latest
