Rais Samia: Chanjo ya Uviko-19 inapunguza gharama za matibabu, vifo
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi kampeni ya Taifa ya chanjo ya Covid-19 Julai 28 mwaka huu na kuwa wa kwanza kuchanjwa akinuwia kuuhakikishia umma kuwa chanjo hiyo ni salama. Picha| Ikulu.
- Ni zile zinazotumiwa na Serikali kutibu wagonjwa wa Uviko-19.
- Pia inaokoa nguvu kazi ya Taifa inayopotea kwa watu kuugua na kufariki.
- Awataka Watanzania kujitokeza kuchanjwa ili kujikinga.
Dar es Salaam. Rais Samia ameeleza faida mbalimbali ikiwa Watanzania watakubali kuchanjwa chanjo ya Corona (Uviko-19) ikiwemo kupunguza gharama za matibabu inazotumia Serikali na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Oktoba 15, 2021, Tanzania ilikuwa imeripoti visa 26,034 vya Uviko-19 na vifo vya watu 724 tangu ugonjwa huo uingie nchini Machi 2020.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza jana katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro amesema kama watu wasipochanja chanjo hiyo inaongeza hasara kwa kutumia gharama kubwa za matibabu ili kuokoa maisha ya watu hasa kutumia mitungi ya gesi kwa ajili ya kupumua kwa wagonjwa.
Pia hasara nyingine inayoweza kujitokeza ni watu kupoteza maisha ambapo hali hiyo inaweza kupungua au kuepukwa kama idadi kubwa ya wananchi kukubali kuchanjwa.
“Tukikaa bila kuchanja, maradhi yale yakiingia yanaingia kwa kasi sana, yanaingia kwa maumivu makali sana. Tunajitahidi lakini tunapoteza watu,” amesema Rais Samia katika uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi.
“Kuchanja kunatupunguzia gharama sana. Kunatupunguzia gharama za matibabu lakini kunatupunguzia gaharama za kupoteza watu wetu, nguvu kazi ndani ya nchi yetu,” amesisitiza Rais Samia.
Aidha, ameupongeza Mkoa wa Kilimanjaro kwa kufanikiwa kuchanja chanjo zote ilizopokea katika awamu ya kwanza, jambo linalotoa uhakika wa watu wake kujikinga na ugonjwa huo.
Agosti mwaka huu, Kilimanjaro ilikabidhiwa dozi 60,000 za chanjo aina ya Johnson&Johnson kati ya milioni 1.05 ambazo Tanzania ilipokea kama msaada kutoka Marekani kupitia mpango wa utoaji chanjo wa Umoja wa Mataifa wa COVAX.
“Tumeletewa dozi 49,000(dozi zingine za Johnson&Johnson na sasa zenyewe zipo katika harakati za kuisha,” amesema Mkuu wa Mkoa wa Kilamanjaro, Steven Kigaigai na kuongeza kuwa tayari wamepokea dozi zingine 36,864 za chanjo aina ya Sinopharm.
Mapema mwezi huu wa Oktoba, Tanzania ilipokea dozi 576,558 za chanjo aina ya Sinopharm kutoka China na kufanya jumla ya chanjo zilizopokelewa hadi sasa kufikia milioni 1.06.
Zoezi la uchanjanji linaendelea katika maeneo mbalimbali nchini huku Serikali ikihamasisha watu kujitokeza na kusisitiza kuwa zoezi hilo ni hiari.
Oktoba 7 mwaka WHO ilizindua mkakati wa kufikisha chanjo ya Uviko-19 kwa asilimia 70 ya wakazi wa dunia ifikapo katikati ya mwaka 2022 ikiwa na lengo la kumaliza mwenendo hafifu wa utoaji chanjo hizo duniani.
Lengo la awali la Shirika hilo, lilikuwa ni kuona asilimia 10 ya wakazi wa kila nchi wawe wamechanjwa chanjo ya Uviko-19 katikati ya mwezi wa Septemba mwaka huu, lakini nchi 56 hazikufikia lengo hilo, huku nyingi zikiwemo barani Afrika na Mashariki ya mbali.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest