Wafanyabiashara wasota na soko liloungua miaka saba Dar
- Ni soko la Mchikichini lililoungua mwaka 2014.
- Wafanyabiashara wajenga vibanda lakini miundombinu siyo rafiki.
- Serikali yasema italijenga upya kulingana upatikanaji wa fedha.
Dar es Salaam. “Lilivyowaka moto soko la Kariakoo walinitonesha kidonda, niliumia… ikanirudisha kwenye maumivu yetu ya nyuma tulivyounguliwa soko letu,” ni maneno ya Eva Kakobe, mfanyabiashara wa kanga na vitenge katika soko la Mchikichini, Halmashauri ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Eva ambaye amekuwa mfanyabiashara kwa takriban miaka 15 katika soko anasema liliungua Juni 11, 2014 na miundombinu na bidhaa zote ziliteketea kwa moto.
Ilikuwa ni huzuni na simanzi kwa waliowekeza mitaji yao sokoni hapo, hata hivyo hakuna aliyewafuta machozi licha ya ahadi ya kujengewa upya soko lao.
“Mizigo yetu iliteketea yote. Mfano, mimi nilikua na cherehani ziliteketea zote,” anasema Rogathe Shayo (60), mfanyabiashara wa kanga na vitenge katika soko hilo lilipo karibu kabisa na machinjio ya Mchikichini.
Zaidi ya miaka saba tangu ajali hiyo itokee, soko hilo halijakarabatiwa. Wafanyabiashara wameamua kujenga vibanda kutumia mbao na mabati chakavu ili waweze kuendelea na shughuli zao katika soko hilo ukizingatia ni moja ya masoko ‘bize bize’ mjini hapo.
Uchakavu wa miundombinu katika soko hilo, umekua kero kwa wafanyabiashara wanawake hasa wakati wa mvua kubwa kwa sababu maji hujaa kwenye mitalo na barabarani na hivyo kulazimika kuhamisha vitu vyao ili visiharibike na maji.
“Sasa hivi mvua ikinyesha, tunakushanya nguo zote zikiwa zimeloa,” anasema Rogathe, mama akionekana mwenye masikitiko kwa sababu hali hiyo inamkosesha wateja wa uhakika.
Hadi kufikia Julai, 2021, wafanyabiashara 2,300 walikuwa wanaendesha shughuli zao sokoni hapo huku asilimia 35 wakiwa ni wanawake, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa soko hilo, Jumanne Kongogo.
Wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao sokoni Mchikichini. Picha | Gift Mijoe
Mazingira ya soko siyo rafiki
Mazingira yasiyoridhisha sokoni hapo yamesababisha baadhi ya wafanyabishara akiwemo mkaanga chipsi, Hamis Abdallah kukosa wateja wa kudumu katika biashara zake ili kukuza mtaji wa kuongeza kipato cha kuhudumia familia yake.
Ubovu wa miundombinu katika masoko umekuwa ukiwaathiri zaidi wanawake ambao ndiyo wamekuwa wakijuhusisha zaidi na uuzaji wa bidhaa, jambo linaloweza kuchelewa ukombozi wa mwanamke kiuchumi kwenye jamii.
“Hali hii imesababisha wale watu wanaokula huku ni wale wale wa humu. Mtu hawezi kutoka huko nje akafikia kula huku kutokana na mazingira yenyewe yalivyo.” anasema Abdallah.
Kwa mujibu wa uongozi wa soko hilo, lilianza kujengwa upya lakini ujenzi ulipofikia asilimia 30 ndipo likaungua na tangu hapo Serikali haijafanya maboresho yoyote licha miundombinu iliyopo kuwa chakavu.

Mara kadhaa, wafanyabiashara wakishirikiana na viongozi wao wamekuwa wakipeleka maombo serikalini ili kujengewa upya soko hilo lakini majibu yamekuwa hayaridhishi licha ya kuahidiwa kuwa kero yao itamalizwa.
“Tumekuwa tukipeleka barua mara kwa mara juu ya malalamiko yetu na vilio vyetu kwa mkurugenzi ila hatukuwahi kupata majawabu. Mara nyingine tunaambiwa wanakuja watu na wataalamu wanajaribu kupima na kuna ujenzi utakuja ila baadaye tunashangaa kimya,” anasema Jumanne akionyesha kukata tamaa juu ya uboreshwaji wa soko hilo.
Mbali na ubovu wa miundombinu katika soko hilo, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika juu ya tozo wanazolipa kutokuleta mabadiliko yoyote licha ya kuungua miaka saba iliyopita.
“Hapa nilipo mimi kila siku nalipa Sh1,000 ya Manispaa kwa ajili ya ushuru na haina sikukuu. Hata usipokuwepo unalipa,” anasema Eva Paschal.
Sheria ndogo ya ushuru wa masoko yaliyopo Manispaa ya Ilala zinaeleza kuwa mfanyabiashara anapaswa kulipa ushuru kwa siku zote ndani ya mwezi mpaka pale soko litakapofungwa.
Sehemu ya soko la Mchikichini ambalo wafanyabiashara wamejenga vibanda wakisubiri Serikali ijenge soko jipya baada la awali kuungua. Picha| Gift Mijoe.
‘Serikali kumaliza mfupa’
Serikali imesema imeweka mipango ya uendelezaji wa masoko ndani ya Manispaa ya Ilala, soko la Mchikichini likiwa mojawapo.
“Serikali kwa maana ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka mipango ya uendelezaji wa masoko hayo, ni masoko yaliyojengwa muda mrefu.
“Kwahiyo Halmashauri imeweka mpango ya kuyaendeleza sasa kuwa katika ukubwa na ubora utakaoendana na idadi ya wafanyabiashara,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu.
Mtendaji huyo amesema masoko hayo hayajasahaulika, yako kwenye mipango ya Serikali kwani masoko hayo ni moja ya chanzo cha mapato kwa Manispaa.
“Mipango ipo, si kwamba masoko hayo yameachwa tu, kwa sababu sisi kwetu masoko haya ni pamoja na kuwa chanzo cha mapato, hivyo iko katika mipango ya muda mrefu,” anasema Shaibu.
Latest