Majukwaa ya mtandaoni yanavyoboresha elimu ya wanafunzi walemavu Tanzania
- Kuwawezeka miundombinu ya kidijitali kuwawezesha kupata elimu.
- Majukwaa hayo yamewasaidia kupata elimu wakati wa Corona
- Maboresho yanahitajika zaidi kukidhi mahitaji yao.
Dodoma. Haikutarajiwa. Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walikuwa mwezi wa tatu tangu kuanza muhula mpya wa masomo katika darasa jipya.
Kwa wanachuo, baadhi walikuwa wakihesabu miezi michache tu hadi kukamiilisha mwaka wa masomo na kusubiria kuvaa majoho.
Hata hivyo, Machi 17, 2020 ilikuwa ni siku yenye mshtuko kwa wengi baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutangaza kufunga shule, kusitisha ligi, matamasha kukoma na sherehe kuahirishwa.
Kwa wanafunzi, ilimaanisha masomo kusimama kwa kipindi kipindi cha siku 30. Ni mwezi mzima wa kukaa nyumbani bila kusoma.
Uamuzi huo ulikuwa ni hatua ya Tanzania kuungana na mataifa mengine duniani kuchakua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19).
Hata hivyo, ilikuwa fursa kwa wabunifu kubuni mifumo ya kidijitali kuwawezesha wanafunzi kusoma mtandaoni wakiwa nyumbani. Majukwaa mbalimbali ya mtandaoni likiwemo la Shule Direct, walitengeneza mifumo rahisi kuwawezesha wanafunzi kuendelea kujisomea kwa kutumia simu na kompyuta.
Ujifunzaji huo bila mwalimu ulihusisha kufanya mazoezi, mitihani, kusoma notsi za masomo, video za mafunzo na mijadala ya wanafunzi.
Mbali na kutoa huduma hiyo, Shule Direct haikuwasahau wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwepo wenye changamoto za kusikia na kuongea.
Kupitia jukwaa la Shule Direct, Mwanafunzi anaweza kujifunza kwa mitihani, majadiliano na notsi za kujisomea. Picha| Shule Direct.
Shule Direct na wanafunzi wenye mahitaji maalum
Kutokana na ukweli kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kuhitaji uangalizi wa karibu wa mwalimu na vifaa vya kujifunzia vinavyoendana na hali zao, jukwaa hilo liliboresha mfumo wake wa kutoa elimu kukidhi mahitaji ya kundi hilo.
Pia lilitumia fursa hiyo kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kwa watu wanafunzi wenye mahitaji maalum ili wasiachwe nyuma.
Meneja Mawasiliano wa Shule Direct, Narindwa Msongole ameiambia Nukta habari (www.nukta.co.tz) kuwa waliwasiliana na mwalimu aliyetengeneza video ambayo ililenga kutoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kuiweka video hiyo kwenye jukwaa la Shule Direct ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
“Tulipakia video ambayo ilihusisha mwalimu anayetumia lugha ya alama kwa ajili ya kuwaelimisha watoto juu ya mbinu za kujihadhari na ugonjwa wa Corona na kuwajengea uelewa wa ugonjwa huo,” amesema Msongole.
Msongole amesema kuwa waliigia ubia na mwalimu huyo ili kutumia maudhui yake.
Video hiyo iliwasaidia wanafunzi hao kuelewa kinachoendelea.
Soma zaidi
- Kilimo kinavyosaidia kuokoa kivutio maarufu cha utalii Tanzania
- Namna ya kuwanusuru wafanyakazi wa ndani na madhara ya Corona
- Wafanyabiashara wasota na soko liloungua miaka saba Dar
Wazazi watayarishe mazingira
Siyo kila mzazi ambaye ana mtoto mwenye mahitaji maalumu anafahamu jinsi ya kumsaidia mtoto kujifunza akiwa nyumbani.
Wapo ambao walau wanaweza hata kuwasiliana na watoto wao lakini wapo ambao wanashindwa kabisa na kuhitaji mtaalamu wa kuwaelewesha.
Jukwaa la Shule Direct liliandaa makala za kuwafundisha wazazi jinsi ya kutayarisha mazingira kwa ajili ya watoto wao kujisomea.
“Makala hizo zimewafundisha mbinu za kuondoa vikwazo vya kujisomea na mazingira yaweje ili wanafunzi waelewe kinachofundishwa,” anaeleza Msongole.
Shule Direct bila haja ya bando
Kwa kawaida, kuingia kwenye tovuti ya Shule Direct unahitaji kuwa na intaneti. Katika kipindi cha Uviko-19, Shule Direct iliingia makubaliano na baadhi ya kampuni za simu nchini ili intaneti isiwe kikwazo cha wanafunzi kujisomea.
“Tulionea na Vodacom na Tigo ili wanafunzi waweze kupata masomo bure,” amesema Msongole.
Hali hiyo iliwawezesha wanafunzi kupata masomo hata kama hawana bando la kuingia katika mtandao huo na hivyo kujisomea.
Licha ya kuwafikia wanafunzi ambao hawawezi kusikia na kusema, Shule Direct haikuwafikia wanafunzi wenye changamoto ya uoni.
Kwa mujibu wa Msongole, juhudi zilizopo ni kuhakikisha zana zote zilizopo kwenye jukwaa hilo zinapatikana pia kwa njia ya sauti ambazo hata mwanafunzi asiyeweza kuona anufaike.
“Ambacho tunakifanyia kazi ni kuboresha majukwaa yetu kua jumuishi hasa kwa watoto wenye changamoto katika kujifunza yaani (learning disabilities) na tutakua tayari mwazoni mwa 2022,” amesema Msongole.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).
Latest