Mwekezaji asota miaka sita kuzindua kiwanda cha nyaya Tanzania
Kiwanda cha nyaya za mawasiliano cha Raddy Fibre Manufacturing kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa Ramadhan Mlanzi kimezinduliwa leo Desemba 2, 2021 na Rais Samia. Picha| Ikulu.
- Ni mmliki wa kiwanda cha nyaya cha Raddy Fibre Manufacturing.
- Asoteshwa miaka sita kupata kibali kutoka TIC.
- Rais Samia akemea tabia ya urasimu kwa wawekezaji wazawa.
Dar es Salaam. Licha ya Rais Samia kuzindua kiwanda cha nyaya za mawasiliano kilichopo Wilaya ya Mkurunga mkoani Pwani, amesema mwekezaji wa kiwanda hicho amesota miaka sita kupata kibali cha ujenzi, jambo ambalo siyo zuri kwa maendeleo ya uwekezaji Tanzania.
Kiwanda hicho cha Raddy Fibre Manufacturing kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa Ramadhan Mlanzi kimezinduliwa leo Desemba 2, 2021 na Rais Samia huku akionyesha masikitiko yake kwa mamlaka husika kuchelewa kumpatia kibali cha kuanzisha kiwanda hicho kwa wakati.
Nyaya za kiwanda hicho ni kwa ajili ya mkongo wa Taifa ambao unawezesha upatikanaji wa huduma ya intaneti nchini na hivyo kurahisisha maisha.
“Mwekezaji huyu amekuja na wazo lake mwaka 2016, leo tuko 2021 ni miaka sita, ni hakika amekumbana na misukosuko mbalimbali,” amesema Rais Samia na kubainisha kuwa waliomkwamisha kuanzisha kiwanda hicho mapema ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
“Bahati nzuri aliyekuwa anaongoza hicho kitengo tunaye hapa ambaye leo ni waziri (Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Geofrey Mwambe) ni yeye aliyemchelewesha, ni yeye anayefungua kiwanda.
“Na nadhani yale aliyoyafanya akiwa TIC sasa atakwenda kuyasimamia yarekebishwe ili wawekezaji wapite haraka haraka,” amesema Rais.
Hata hivyo, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema Mlanzi hakukata tamaa kutimiza ndoto yake ya kuwa na kiwanda kikubwa cha kutengeneza nyaya nchini.
“Wakati anakuja na wazo hili 2016, jina Ramadhan Hassan Mlanzi bila shaka pale TIC walimtizama mara tatu tatu pengine walimuona ni tapeli, dalali, mwongo kwa sababu ya jina tu na kwamba ni Mtanzania, kumbe wangekwenda naye haraka haraka ufunguzi wa kiwanda hiki ungefanyika miaka minne mitano nyuma,” amesema Rais.
Amesema ucheleweshwaji aliofanyiwa Milanzi huenda umetokana na mtazamo hasi juu ya wawekezaji wazawa, jambo ambalo siyo jema kwa maendeleo ya viwanda Tanzania.
“Kwa sababu ya jina Ramadhan Hassan Mlanzi basi unaanza kudharau tu labda lingekuja jina Johnson Blonson labda ndiyo mngeona mwekezaji wa maana.
“Kwa hiyo ndugu yangu nikupe pole ya mabonde ya milima lakini nikupongeze kwa hatua uliyofikia,” amesema Rais.
Kiwanda hicho kinatajwa kuwa ni cha nne kwa ukubwa Afrika na kitakuwa mkombozi kwa Watanzania kwa sababu kinatoa fursa za ajira na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha kilomita 24,000 za nyaya kwa mwaka na hivyo kurahisisha upatikanaji wana kinatarajiwa kutoa ajira zipatazo 670 pindi kitakapomalizika.
“Urasimu kwenye Serikali yangu hauna nafasi”
Aidha, Rais Samia amekemea tabia ya baadhi ya watendaji kuwadharau na kuwabagua wawekezaji wazawa badala yake amewataka watoe huduma kwa haki bila upendeleo.
“Mheshimiwa waziri (Mwambe) naomba muache hizo kasumba, kuna Watanzania wengi ambao wameshatembea, wameshaona, wamepata mitaji wanataka kuja nyumbani kuwekeza na watuletee faida zilizoletwa na kiwanda hiki naomba muwakumbatie,” amesisitiza Rais.
Amezitaka taasisi zinazosimamia uwekezaji kuacha urasimu kwa sababu Tanzania inahitaji wawekezaji kuliko Watanzania wanavyowahitaji.
Amesema wana wajibu wa kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kadiri inavyowezekana na kurahisisha michakato ya utoaji vibali ili nchi ifaidike.
“Tunapochelewesha muwekezaji tunachelewesha ajira kwa vijana wetu, unachelewesha kodi, unadumaza uchumi wa Taifa letu,” amesema Rais Samia.
Latest