Mwanzo mpya: Wakulima kufaidika kilimo cha viungo Tanzania
- Ni baada ya kongamano la viungo litakalofanyika Zanzibar wiki hii.
- Litawakutanisha wadau wa kilimo kujadili namna ya kulifikia soko la viungo.
- Huenda ikawa ni njia sahihi ya kuwapatia tija wakulima wa viungo.
Dar es Salaam. Huenda wakulima na wafanyabiashara wakaanza kufaidika kikamilifu na soko la kimataifa la viungo baada ya wadau wa kilimo kuandaa kongamano la siku mbili kujadili namna ya kuongeza uzalishaji na kutanua wigo wa soko la bidhaa hizo ili kuleta tija Tanzania.
Tanzania inazalisha zaidi ya aina 30 za viungo ikiwemo karafuu, pilipili kali, tangawizi, mdalasini, pilipili manga, iliki, mchaichai na vanila. Viungo hivi vina faida nyingi zikiwemo za kuimarisha afya na pia vinatumika kama dawa mbadala.
Hata hivyo, bado wakulima hawajafaidika inavyotakiwa na kilimo cha viungo kwa sababu ya njia duni za uzalishaji na kushindwa kulitumia vizuri soko la kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo, mwaka 2015, Tanzania ilizalisha tani 8,609 za viungo, kati ya hizo, tani 396 (asilimia 4.29) ziliuzwa nje ya nchi.
Pia mwaka 2019 uwiano wa mauzo ya nje ulipungua hadi asilimia 1.23 huku tani 478 kati ya tani 38,987 za viungo zilisafirishwa nje ya nchi.
Ingawa hivi karibuni, uzalishaji halisi wa viungo umeongezeka, kiasi cha viungo kinachouzwa nje ya nchi kinashuka huku karafuu pekee ikichangia zaidi ya asilimia 90 ya mauzo yote ya viungo nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, programu ya AGRI-CONNECT inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), itafanya kongamano la kitaifa Desemba 7 na 8, 2021 Mkoa wa Kaskazini, Pemba ili kujadili kwa kina namna ya kuongeza uzalishaji na kuyafikia masoko ya kimataifa.
“Washiriki watatoka Tanzania bara na visiwa vya Zanzibar, wakiwemo viongozi wa serikali, maafisa wa serikali, washirika wa maendeleo, wataalamu na wadau wanaojihusisha na sekta ya viungo wakiwemo wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara na wakufunzi,” imeeleza taarifa ya AGRI-CONNECT iliyotolewa Desemba 4, 2021.
Zinazohusiana:
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Wakulima kuwezeshwa kuuza pamba kwa bei wanayotaka
- Karafuu yachangia kushuka kwa mauzo ya nje Zanzibar
Kongamano hilo linalenga kuibua na kujadili hoja na masuluhisho yatakayoimarisha biashara ya viungo kwa kuzingatia kuwezesha na kuongeza uzalishaji mali na ustawi wa pamoja.
Pia litajikita kuangazia historia na matarajio ya tasnia ya viungo nchini Tanzania, vipaumbele vya kisekta na uboreshaji wa mazingira ya biashara kwa tasnia ya viungo na kuongeza thamani baada ya mavuno.
Washiriki watajadili namna ya kukuza uzalishaji bora na wenyebtija wa viungo hususan kwa kuzingatia matumizi ya chapa ya viungo ya Tanzania na viwango vya kimataifa vya ubora.
“Iwapo wadau watatumia chapa ya viungo ya Tanzania na kukidhi viwango vya ubora vya kimataifa, pamoja na uzalishaji endelevu na kwa kuongeza tija, wakulima wanaweza kuwa na uhakika wa masoko yenye thamani ya juu, na hivyo kutengeneza fursa za ajira kwa makumi ya maelfu ya Watanzania,” imeeleza taarifa ya programu hiyo.
AGRI-CONNECT ni programu iliyo chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo (Tanzania Bara) na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Zanzibar.
Programu imeanza kufanya kazi mwaka 2020 na inatarajiwa kufikia mwisho mwaka 2024 ikiwa na lengo la kuchangia ukuaji wa uchumi shirikishi, kukuza maendeleo ya sekta binafsi na kuongeza ajira katika sekta ya kilimo na inalenga kuongeza uhakika wa chakula na lishe bora nchini Tanzania.
Latest
