Ndugai ajiuzulu baada ya wiki ya kukosolewa, shinikizo kujiuzulu

January 6, 2022 2:24 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema uamuzi huo ni wa hiari na amefanya hivyo kwa maslahi mapana ya Taifa, Serikali na CCM.

Dar es Salaam. Spika wa Bunge Job Ndugai amejiuzulu nafasi yake wiki moja baada ya kuwepo shinikizo kubwa kutoka kwa watu mbalimbali la kumtaka kujiuzulu kutokana na kauli yake iliyokosoa uamuzi wa Serikali kukopa zaidi mikopo kugharamia miradi ya maendeleo.

Spika Ndugai katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo Januari 6, 2022 ameeleza kuwa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kujiuzulu nafasi hiyo ya kuliongoza Bunge ambayo ameishikiria kwa zaidi ya miaka sita sasa.

“Uamuzi huu ni binafsi na hiari na nimeufanya kwa kuzingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya Taifa langu, Serikali na chama changu cha CCM,” amesema Ndugai.

Katika taarifa hiyo, Ndugai ameeleza kuwa tayari ameshawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Katibu wa Bunge kwa ajili ya hatua stahili kwa mujibu wa Katiba na sheria nyingine ili kuwezesha kuanza mchakato wa kumpata Spika mwingine.

Kujiuzulu huko kwa Ndugai kunafuata baada ya kukosolewa vikali kwa zaidi ya wiki moja kufuatia kusambaa kwa video inayoonyesha hotuba yake aliyoitoa Jijini Dodoma Desemba 26, 2021 iliyokuwa ikikosoa hatua ya Serikali kuendelea kukopa zaidi mikopo ukiwemo wa hivi karibuni wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Video hizo zimezua mjadala mkubwa hasa katika mitandao ya kijamii na kusabanisha Spika huyo kuitisha mkutano na wanahabari mapema wiki hiyo akieleza kuwa kuna “mambo yalikatwakatwa”.

Tangu Ndugai atoa kauli hizo Rais Samia Suluhu Hassan ameonekana akijibu mapigo mara mbili katika hotuba zake ikiwemo ya Jumanne hii aliyoendelea kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kukopa na kwamba hakutegemea kiongozi wa muhimili angesema maneno yale.

Mbali na kukosolewa na Rais Samia licha ya kuomba msamaha, Ndugai amekuwa akishinikizwa na makada wa CCM kujiuzuru huku shinikizo hilo likipaa zaidi kuanzia mapema wiki ikiwemo kutoka kwa vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Kujiuzulu kwa Ndugai kunamaliza safari yake ya miaka sita ya kuliongoza Bunge hilo lenye makao yake jijini Dodoma. Ndugai alichaguliwa kuliongoza Bunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na mwishoni mwaka jana tena baada ya Uchaguzi Mkuu alichaguliwa kwa kipindi kingine hadi leo alipojiuzulu.

Kutokana na hatua hiyo, Ndugai atarudi kuwa mbunge wa kawaida akiwatumikia wananchi wa Kongwa huku akiacha mchakato wa kumpata Spika mwingine atakayemalizia kipindi cha miaka minne iliyosalia.

Spika Job Ndugai akiwa kwenye majukumu yake bungeni. Picha|Mwananchi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW