OnePlus 10 Pro: Simu janja itakayokata utepe mwaka 2022
- Inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwanzo wa mwezi Januari.
- Muonekano umebadilika kidogo, “selfie camera” uwezo umeongezwa.
- Gharama na lini itavuka masoko ya India bado kitendawili.
Ni wiki ya kwanza ya mwaka 2022 na wadau wa teknolojia za simu tayari wanaukaribisha mwaka na bidhaa mpya sokoni.
Januari 11, 2022 kampuni ya bidhaa za kielektroniki ya China, OnePlus inatarajia kuzindua aina mpya ya simu ijulikanayo kama OnePlus 10 Pro.
Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi mwenza wa kampuni hiyo Pete Lau amesema simu hiyo mpya itakuwa bora kuliko matoleo yaliyopita.
Lau kaeleza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa, “OnePlus 10 Pro ni zaidi ya mkusanyiko wa sehemu za simu”
Picha za awali za simu hiyo tarajiwa, zinaonyesha kuwa kuna mambo mengi yanayoitofautisha na mtangulizi wake, 9 Pro ikiwemo uwezo na muonekano wa kamera.
Tofauti kubwa inayoonekana ni muundo wa kamera. Picha| Tom’s Guide.
Hodi hodi sokoni
Ikiwa ni simu ya kwanza itakayoingia sokoni kwa mwaka 2022, One plus inaambatana na maboresho huku mambo mengine yakiwa ni sawa na OnePlus9 Pro ya 2021. Mfano, kamera ya 10 Pro imebadilika kimuundo na kutaka kufanana kiasi na kamera ya iPhone 13.
OnePlus haijataka kufuja uhondo wote wa simu hiyo mpya kwa kuacha baadhi ya taarifa muhimu ikiwemo bei zake, uwezo wa uhifadhi na lini simu hiyo itapatikana kwenye masoko ya kimataifa nje ya China.
Hata hivyo, Haya ni mambo ambayo OnePlus imeweka bayana juu ya 10 Pro ya Januari 11.
Macho matatu kwenye mraba
Imezoeleka Oneplus kuingiza sokoni simu ambazo kamera zake zipo kwenye mstatiri. Kwa simu ya 2022, kamera zake zinakuja kwenye mraba kama ilivyo kwenye iPhone 13.
Kamera za nyuma zipo tatu lakini uwezo wake ni kama ule wa OnePlus 9 Pro. Tofauti kubwa iliyopo ni umbo na ukubwa wa kamera za simu hiyo.
OnePlus 10 Pro itaambatana na kamera zenye uwezo wa MP8, 48 na 50 mtawalia ambazo ni sawa sawa na zilizopo kwenye 9 Pro iliyotolewa mwaka jana.
Kamera kuu (Main camera) ina uwezo wa “Megapixel” (MP) 48, kamera ya picha pana (telephoto) ina MP50, na kamera ya kupiga vitu vya mbali (telephoto) yenye ina MP8.
Walichoongeza OnePlus kwenye toleo hilo jipya ni uwezo wa kamera ya mbele ambayo kwa 10 Pro itakuwa ya MP32 kutoka 16 ya 9 Pro.
Soma zaidi
- Unavyoweza kuitumia simu yako kama rimoti
- Unayohitaji kufahamu kuhusu simu mpya za Google
- Simu inavyoweza kuimarisha ulinzi nyumbani, ofisini
Hewani zaidi
Furaha ya kila mtu anayetumia simu ni kuwa na kifaa kinachokaa na chaji kwa muda mrefu. Kutoka battery lenye uwezo wa mAh 4,500 kwenye 9 Pro, simu ya OnePlus 10 Pro itaongezewa uwezo wa betri kwa mAh 500 hivyo kufikia uwezo wa mAh 5,000.
Uwezo huo ni sawa na baadhi ya simu zilizopo sokoni ikiwemo Samsung Galaxy S21 Ultra, Xiaomi Mi 11 na Redmi Note 10 Pro Max.
Katika uwezo wa betri, tulitegemea OnePlus wafanye vyema zaidi kwani zipo simu ambazo betri lake lina hadi mAh 6,000 tayari kama Asus Rog Phone 5.
Kuwa na betri lenye uwezo mkubwa pamoja na mfumo wa kuchaji kwa haraka, huenda ni kati ya mambo ambayo OnePlus imefanya “poa” kwa simu hiyo japo siyo kwa kiwango kikubwa kama nyingine.
Pamoja na hayo, 10 Pro itatumia mfumo endeshi wa Android iliyotengenezwa na kampuni ya simu za Oppo huku teknolojia ya chaja zake za kuchaji haraka, zikitokea kwenye kampuni hiyo.
Licha ya kuwa bado OnePlus haijatoa bei ya simu hiyo, wadau mbalimbali wa teknolojia wakiwemo wa nchini India wametabiri huenda ikauzwa kwa Dola za Kimarekani 852 ambayo ni sawa na takriban Sh2 milioni kabla ya kodi.
Nini kingine kitakuwa kipya? Endelea kufuatilia habari za Nukta kupitia Nukta Habari na Nukta TV.
Latest



