Rais awatolea uvivu mawaziri, manaibu mawaziri
Rais Samia aliyetoa maagizo hayo leo Januari 13, 2022 alipokuwa akifanya mazungumzo na mawaziri na naibu mawaziri katika ukumbi wa Hazina uliopo jijini Dodoma amesema viongozi hao wanatakiwa kwenda na mabadiliko ya sasa ili kutofanya kazi kwa mazoea. Picha| Wilson Malima.
- Awataka kuwa wabunifu katika utendaji na kuacha kufanya kazi kwa mazoea
- Awaonya kutokufanyiana ubabe na kufumbiana macho.
- Agusia pia ajira za kindugu na kirafiki kuwa mwiba kwa taasisi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri na naibu mawaziri kubadilika kulingana na wakati lakini, kuongeza ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Rais Samia aliyetoa maagizo hayo leo Januari 13, 2022 alipokuwa akifanya mazungumzo na mawaziri na naibu mawaziri katika ukumbi wa Hazina uliopo jijini Dodoma amesema viongozi hao wanatakiwa kwenda na mabadiliko ya sasa ili kutofanya kazi kwa mazoea.
“Tuupdate (tusasishe) kwenye kubadilika, kubadilika jinsi muda unavyokwenda, kubadilika jinsi uchumi unavyotuambia, kubadilika jinsi utambuzi wa watu unavyokuja.
“Ukiingia huko kwenye maeneo ambayo watu wanasema unakuta wanasema mengi mengine yana maana kuliko tunayoyafanya huku ndani, kwa hiyo tuwe (dynamic) wenye kubadilika,” amesema Rais Samia.
Pia amewataka kuwa wabunifu katika utendaji wao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuleta tija kwa wananchi.
“Kuna swala la kuwa wabunifu na kuweza kutatua changamoto zetu na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea. Kazi zinavyoendeshwa ni hivyo hivyo tunatakiwa kuwa wabunifu,” amesema Rais Samia.
Kikao cha mawaziri na manaibu mawaziri waliokuwa na mazungumzoa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Januari 13, 2021 jijini Dodoma. Picha| Wilson Malima.
Aidha, amewataka mawaziri kutokufumbiana macho kwa makosa na kasoro zao huku akiwahimiza kuonyana kistaarabu ili kuondoa migogoro na migongano baina yao.
“Sasa kule kutokutaka kuaambizana, kutokutaka kuchukuliana hatua kuwa (reserved) kutunziana, kutokutaka kuonesha au kutokutaka kumkera mtu kwa kumwambia kasoro yake huo ni muhali. Kwa hiyo mnakokwenda huko kama mwenzio ana tatizo itaneni kistaarabu si kutukanana,” amesisitiza Rais.
Maradhi yanayozitesa wizara
Pia katika mazungumzo hayo, Rais Samia amebainisha maradhi makubwa mawili yanayozitafuna wizara za Tanzania ikiwemo kuwepo kwa migogoro na kutokuelewana kwa sabau ya maslahi binafsi na si ya wananchi.
”Suala lingine ni kutoelewana baina yenu, sijui mna maradhi gani ndugu zangu, waziri na manaibu waziri hawaelewani, waziri na katibu mkuu hawaelewani, hili mimi silielewi kwa sababu kila mtu yuko pale ameonekana anaaminika na anaweza kufanya hiyo kazi.
Soma zaidi:
- Ni panga, pangua: Rais Samia afumua baraza la mawaziri Tanzania
- Rais Samia awapangia kazi mpya Profesa Kabudi, Lukuvi
“Wakati mwingine mnachogombania sio haki zenu, ni kwa haki za wananchi mnazozi-grab (mnazozinyakua) lakini huko kwa sababu mgawo hauendi sawa mnagongana,” amesema Rais Samia.
Pia amegusia suala la mawaziri kupeana ajira au nafasi kindugu na kwa kuzingatia urafiki ambapo amesema ni jambo linaloharibu taasisi.
“Lingine linaloharibu taasisi ni ajira za kirafiki, ajira za kindugu, unaweza kuvuta r afiki zako ukijua hawa ni team players (washirika wangu), nikiwa na fulani na fulani tutachapa kazi vizuri unaweza kuwa nao lakini unawavuta tu kwa sababu ni rafiki zangu tumekua pamoja waje niwe nao hapa, mtaua taasisi zenu, naomba mkayazingatie hayo,” amesema Samia.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Samia alifanya mabadili madogo ya Baraza la Mawaziri na kulisuka upya baraza ikiwa ni hatua ya kuboresha utendaji kazi na kuchagua watu ambao anaamini watamsaidia kutimiza majukumu ya kuwaleta wananchi maendeleo.
Mabadiliko hayo yalihusisha kuteua mawaziri wapya watano, kufanya mabadiliko katika wizara tisa kwa kuwabadilisha mawaziri, kuigawa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kuwapumzisha mawaziri wanne akiwemo Profesa Palamagamba Kabudi wa Katiba na Sheria.
Latest