Mwandishi Nukta Africa kinara tuzo za corona Afrika Mashariki
- Ni Tulinagwe Malopa aliyeshinda tuzo ya kuripoti kwa usahihi habari za Corona.
- Tuzo hizo zimetolewa na shirika la Merk Foundation ya nchini Ujerumani.
- Ameibuka mshindi wa tatu katika kipengele cha vyombo vya habari vya mtandaoni.
Dar es Salaam. Mwandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Afrika, Tulinagwe Malopa amepata tuzo ya kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) kwa mwaka 2021.
Tuzo hizo zilizopewa jina la “Mask Up With Care” zimetolewa na shirika la Merk Foundation ya nchini Ujerumani kwa waandishi wa habari katika nchi mbalimbali duniani ambao walikuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya kujikinga na Uviko-19 ikiwemo uvaaji sahihi wa barakoa.
Malopa ambaye amekuwa akiripoti habari zake katika tovuti ya habari ya Nukta (www.nukta.co.tz) na Nukta TV ameibuka mshindi wa tatu kwa upande wa waandishi wa habari wa Afrika Mashariki katika kipengele cha vyombo vya habari vya mtandaoni (Online category).
Habari iliyompa ushindi huo mwanahabari huyo ilikuwa inahusu nama utupaji hovyo wa barakoa zilizotumika unavyowaweka watu katika hatari ya kupata maradhi ya Uviko-19 huku akibainisha njia sahihi za kuhifadhi barakoa hizo.
Mshindi wa kwanza katika kipengele cha vyombo vya habari vya mtandaoni ni Nelson Mandela, wa tovuti ya PML Daily ya Uganda huku Dorcas Wangir, wa Citizen TV ya Kenya na Delphine Maombi wa newtimes.co.rw, ya Rwanda wakiibuka katika nafasi ya pili kila mmoja.
Soma zaidi:
-
Waandishi Nukta Africa vinara tuzo za umahiri wa habari Tanzania
-
Waandishi wa Nukta Africa wateuliwa kuwania tuzo EJAT 2020
Akihojiwa na Nukta Habari Malopa ameeleza kuwa amejisikia mwenye furaha sana kupata tuzo hiyo na kuiwakilisha vema Tanzania kimataifa hasa katika kutambuliwa kuripoti kwa usahihi kuhusu Uviko-19.
“Kama mwanahabari najiskia furaha kuipeperusha vema bendera ya Tanzania katika tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zinazohusu ugonjwa wa Uviko-19, Barani Afrika,” amesema Malopa na kubainisha kuwa tuzo hiyo imemuongezea nguvu ya kufanya kazi kwa bidii.
“Katika safari yangu ya uandishi, tuzo hii inanipa motisha kuendelea kuelimisha jamii na kuwapa taarifa sahihi zenye matokeo chanya hasa katika kipindi ambacho dunia inafanya kila jitihada kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19,” amesema Malopa.
Shirika hilo kwa kushirikiana na Wanawake wa Marais wa Afrika walitangaza walitoa tuzo hizo kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu virusi vya Corona barani Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Merck Foundation, Dk. Rasha Kelej, amesema anaamini kuwa vyombo vya habari vina jukumu muhimu sana katika kukuza ufahamu, kuelimisha jamii na kuwasilisha taarifa muhimu na sahihi kwenye jamii.
“Katika wakati huu wa janga la kimataifa la Uviko-19, vyombo vya habari vimekuwa na jukumu la kipekee katika kueneza habari kuhusu janga hilo, kutenganisha uzushi na ukweli katika viwango vyote,” amesema Dk Kejeli hivi karibu baada ya kutoa orodha ya washindi.
Septemba 2021, Waandishi wengine wa Nukta Africa, Rodgers George na Daniel Samson walitangazwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2020 zilizotolewa na Baraza la habari Tanzania (MCT).
Latest
