Rais Samia ataja sababu mbili Serikali kushirikiana na machifu
- Asema ni kwa ajili ya kuhifadhi mila, desturi na mazingira.
- Agusia kauli za watu wanaotilia shaka ushirikiano huo.
- Machifu kusajiliwa kwenye kanzidata maalum.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ufafanuzi kuhusu Serikali kuendelea kushirikiana na machifu na wazee wa kimila kuwa ni ili kuhifadhi mila, desturi na mazingira kwa ajili ya maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Rais Samia ametoa kauli hiyo baada ya kuwepo mijadala mbalimbali kuhusu uchifu nchini huku baadhi ya watu wakihuusisha na ukabila na ukanda, jambo ambalo linaloweza kuleta changamoto katika ujenzi wa mshikamano wa kitaifa.
Wengine wameeleza kuwa ushirikiano huo hauna tatizo kwa sababu unasaidia kudumisha na kurithisha mila na desturi za Tanzania kwa vizazi vijavyo.
Rais Samia akitolewa ufanunuzi suala hilo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na machifu na wazee wa kimila kwa sababu ni viongozi muhimu katika jamii kuendeleza mila na desturi na kuhifadhi mazingira ya Tanzania.
“Kumekuwa na maneno mengi ndani ya Tanzania kuhusu Serikali kushirikiana na uchifu. Nataka niseme tumeamua kuwa na jukwaa la pamoja baina ya Serikali, machifu, wazee wa kimila ili macifu na wazee wa kimila kama nguvu muhimu ya kuhifadhi mila na desturi zetu na katika kuhifadhi maeneo mbalimbali yaliyotunzwa kama njia ya kuhifadhi mazingira ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan (Chifu Hangaya) leo Januari 22, 2022 baada ya kuvalishwa vazi maalum la Chifu Mkuu wa kabila la Wachanga mkoani Kilimanjaro. Picha| Swahili Times.
Rais Samia ametoa msimamo huo leo Januari 22, 2022 wakati akizindua tamasha la utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro katika viwanja vya ushirika mjini Moshi.
Amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na machifu kote nchini katika kulinda mazingira ambapo wanazuia wananchi wasiyasogelee na kuyaharibu.
“Serikali itashirikiana na viongozi hawa wa kimila ili kuendelea kudumisha mila zetu lakini kubwa zaidi ni katika kuhifadhi mazingira, “amesema Rais Samia.
Ili kuimarisha ushirikiano huo wa faida, amesema Serikali itaendelea kuongeza bajeti katika Wizara ya Sanaa, Michezo na Utamaduni ili iweze kuandaa matamasha ya utamaduni katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitolea mfano tamasha la kitaifa litakalofanyika Mei mwaka huu, Rais Samia ameiagiza Wizara hiyo kuhakikisha inashirikisha taasisi zote wakiwemo machifu na watemi wa kila mkoa pamoja na kuwaalika mabalozi wanaowakilisha nchi mbalimbali nchi kuhudhuria ili waweze kulitangaza tamasha hilo lakini pia kutangaza tamaduni na mila zetu.
Rais Samia amesema yapo matamasha kama hayo yanayogusa mila za watu yanayofanywa na nchi mbalimbali ikiwemo Brazil na kwa Zanzibar tamasha la Sauti za Busara ambalo hukutanisha watu wa ndani na nje ya nchi.
“Na kwa hapa Tanzania kuna matamasha ya kitaifa ambayo hajatangazwa vizuri mfano tamasha la Bagamoyo, ni vema nguvu na mikakati ikawekwa katika kulitangaza ili liweze kutangaza nchi na fursa za kitalii katika nchi yetu, ” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:
Ajibu maombi ya machifu
Kuhusu maombi muhimu matano waliyoyatoa machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro kwenye risala yao, amesema Serikali tayar imeanza kuyafanyia kazi ikiwemo kuanzisha kanzidata ya kuwatambua machifu kote nchini ambapo hadi kufikia Januari 20, 2022 tayari machifu 92 wameshasajiliwa wakingozwa na yeye chifu Hangaya huku zoezi la kuwasajili wengine likiendelea.
Amesema tayari Serikali imeanza kufanyia kazi suala la kutambua michango ya machifu waliopambania uhuru wa Tanzania Bara huku suala la mapango likifanyiwa kazi ambapo hadi sasa mapango 36 yanayotumiwa kwa shughuli za kimila yametambuliwa.
Amewaagiza Watanzania kuendelea kuhifadhi na kuhifadhi maeneo na majengo yaliyotumiwa na machifu ili yaweze kutumiwa katika utalii na sasa ni majengo 200 pekee ndiyo yametambuliwa.
Hata Hivyo amesema Serikali bado inafanyia kazi suala la kurejesha mafuvu ya machifu waliouawa na wakoloni na taratibu zikikamilika yatarudishwa nchini.
Latest