Waziri Nape ayafungulia magazeti manne yaliyofungiwa
- Ni magazeti ya Tanzania Daima, Mseto, Mawio na Mwanahalisi ambayo yalikuwa yamefungiwa.
- Yalifungiwa kwa madai kuwa yalikiuka maadili ya uandishi wa habari na sheria.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari na Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametangaza kutoa leseni ili kuruhusu kuanza kuchapishwa kwa magazeti ya Tanzania Daima, Mseto, Mawio na Mwanahalisi ambayo yalikuwa yamefungiwa.
Waziri Nape ametoa leseni hizo leo Februari 10, 2022 wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza vyombo vilivyofungiwa vifunguliwe na agizo lake ni sheria inayopaswa kutekelezwa.
Kutokana agizo hilo, Waziri Nape amesema “agizo la Rais ni sheria na inapaswa kutekelezwa, leo nitatoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima.
Amesema kufunguliwa kwa magazeti hayo ni kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa Serikali na vyombo vya habari ambao miaka kadhaa iliyopita ulikuwa siyo wa kuridhisha.
“Ni vizuri kuondoka kwenye maneno tufanye vitendo hivyo tuanze na ukurasa upya sasa mwenye maneno yake aseme mwenyewe, kifungo kimetosha kikubwa kazi iendelee,” amesema.
Hata hivyo, Nape amesema ilikuwa siyo rahisi kufanya uamuzi huo na kuvitaka vyombo vya habari kutumia vizuri imani na nia njema ya Serikali kwa sababu kila mmoja ana wajibu wa kuijenga Tanzania tuitakayo.
“Wizara ninayoingoza itafungua milango na madirisha wakati wowote, ukiona umeenda kutafuta habari ukanyimwa simu yangu iko wazi masaa 24,” amesema Nape.
Magazeti hayo yalifungiwa kwa nyakati tofauti kwa madai ya kukiuka Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na maadili ya vyombo vya habari ikiwemo kuchapisha habari za uchochezi na zinazohatarisha amani ya nchi.
Aidha, Waziri Nape ameongeza muda wa mwaka mmoja kwa waandishi wa habari ambao bado hawajapa elimu ya stashahada (diploma) kufanya hivyo ili kukidhi matakwa ya sheria yanayowataka kuwa na kiwango hicho cha elimu ili kufanya kazi za uandishi wa habari.
“Mimi nikiwa waziri, nilisimamia ile sheria ya huduma ya vyombo vya habari, mazingira ya wakati ule na sasa ni tofauti, mwaka 2016 na 2022 ni tofauti. Hili la elimu tutoe mwaka mmoja ili tuone nini cha kufanya huko mbele,” amesisitiza.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers, Said Kubenea akizungumza mara baada ya kupokea leseni ya Mwanahalisi ameishukuru Serikali kwa kuyafungulia magazeti hayo.
“Sisi tumefarijika kupata leseni. Tunakumbuka kwamba magazeti karibu yote haya hasa ya kwetu sisi yalimaliza adhabu zaidi ya miaka miwili iliyopita au mitatu. Lakini pia yalishinda kesi mahakamani, hata hivyo magazeti hayakuweza kurudi mtaani,” amesema Kubenea na kuongeza kuwa,
“Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kwa maana bila yeye pengine bila yeye haya magazeti yasingeweza kufunguliwa.”
Haya hivyo, amesema wamepata leseni ya kuanza kuchapisha tena magazeti hayo lakini yanaweza yasionekane mtaani kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayovikabili vyombo vya habari.
“Tumepata leseni lakini inawezekana haya magazeti usiyaone mtaani, hali ya uchumi ni mbaya sana. Magazeti yapo ambayo hayakufungiwa lakini yamejifunga yenyewe kutokana na hali za uchumi. Serikali namna ambavyo inaweza ikatoa ruzuku kwa vyombo vya habari binafsi,” amesema Kubenea.
Awali, Waziri Nape ameagiza taasisi za Serikali kutoa fursa za matangazo kwa vyombo vyote vya habari bila ubaguzi ili vijipatie mapato ya kujiendesha.