Redio bado zipo zipo sana Tanzania

February 12, 2022 10:20 am ยท Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Redio kesho Februari 13, 2022, redio ni chombo muhimu ambacho Watanzania wana kitumia kupata habari zinazowawezesha kufanya maamuzi katika maisha yao ya kila siku.

Licha ya kuongezeka kwa changamoto za kifedha zinazoendelea kuvikabili vyombo mbalimbali vya habari duniani, idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza katika ripoti mpya ya mawasilino ya robo ya mwisho ya mwaka 2021 kuwa hadi Desemba mwaka jana kulikuwa na vituo 210 vya redio nchini kutoka vituo 193 mwaka 2020.

Uchambuzi wa mwenendo wa takwimu za vituo vya redio uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) unaonyesha kuwa vituo vingi vya redio vilizaliwa mwaka 2016 baada ya vituo 42 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.

Hata hivyo, mwaka 2018 ndiyo mwaka ambao vituo vichache zaidi vilianzishwa ndani ya mwaka mmoja kutokana na kuongezeka kwa vituo viwili tu vya redio kutoka 156 mwaka 2017 hadi 158 mwaka 2018.

Hata hivyo, takwimu hizo hazihusishi vituo vya redio vya mtandaoni na haziweki bayana aina ya vituo hivyo katika makundi kama vya kijamii, kidini au kitaifa.

Redio ni moja ya aina ya vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi zaidi nchini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za hivi karibuni.

Ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Repoa wa Afrobarometer wa mwaka 2017 inabainisha kuwa redio ndiyo chanzo maarufu cha habari miongoni mwa Watanzania baada ya matokeo kubainisha watu 45 kati 100 hupata habari kupitia redio kila siku.

Licha ya utafiti kueleza kuwa sehemu kubwa ya watu Tanzania hupata habari kutoka redioni, Kitabu cha ubora wa habari cha mwaka 2017 (Yearbook in Media Quality in Tanzania 2017: What do we know?) kinabainisha kuwa habari za redioni bado zina ubora hafifu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW