Tanzania kutumia miradi ya kimkakati kuimarisha uhusiano wa kimataifa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, mkutano wa 10 wa wakuu wa nchi wa Serikali zinazohusika na mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini DRC na kwenye ukanda wa maziwa makuu unaofanyika leo, Februari 24, 2022 jijini Kinshasa, DRC. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa na bomba la mafuta.
- Yasisitiza kuendelea kushamirisha amani na utulivu Afrika.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa mengine ili kuhakikisha amani, ushirikiano, ustawi wa kijamii na kiuchumi unaendelea kushamiri katika nchi zote za bara la Afrika.
Majaliwa amesema kuwa tangu enzi za uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania imeshiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi barani Afrika, kutoa hifadhi kwa wakimbizi pamoja na kushiriki katika kazi ya kulinda amani.
Amesema katika kuhakikisha inashiriki katika ukuzaji wa ustawi wa kiuchumi barani Afrika, Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kutoka uvinza (Tanzania)- Gitega (Burundi) hadi Kindu (DRC).
“Pia tunajenga SGR kutoka Isaka (Tanzania) hadi Kigali (Rwanda),” amesema Majaliwa na kubainisha kuwa mradi mwingine unaolenga kukuza uchumi wa Afrika ni pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani (Tanzania).
Kiongozi huyo mkuu wa shughuli za Serikali ametoa kauli hiyo Februari 24, 2022 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)
Aidha, amependekeza kuwa katika mikutano mingine ya nchi wanachama wa Makubaliano ya Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC na Ukanda wa Maziwa Makuu, lugha ya Kiswahili iongezwe kama mojawapo ya lugha rasmi ya mikutano hiyo.
“Ni heshima kubwa sana kwa lugha yetu ambayo kwa sasa imepata idhini kutumika Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema.
Soma zaidi:
- Rais Samia ataja virusi vitatu vinavyotafuna maendeleo ya Mara
- Tanzania itakavyofaidika ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa, Ubelgiji
- Msimamo wa Tanzania kuhusu diplomasia ya uchumi kimataifa
Mkutano wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali umepitisha taarifa ya pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu na pamoja na maazimio yake.
Mkutano huo umeongozwa na Rais Félix Tshisekedi wa Congo DRC baada ya kukabidhiwa uenyekiti na Mwenyekiti wa sasa Yoweri Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ulizinduliwa nchini Ethiopia Februari 24, 2013 baada ya Wakuu wa Nchi 11 kusaini mkataba ulioanzisha mpango huo.
Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Angola, Afrika Kusini, Burundi, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kongo, Uganda, Zambia, Kenya na Sudan.
Mpango huo unalenga kusitisha mapigano Mashariki mwa DRC na maeneo mengine ya Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na kutoa majukumu kwa DRC kuimarisha usalama, nchi jirani kutoingilia masuala ya ndani ya DRC na kutounga mkono makundi ya waasi nchini humo.