Rais Samia ataja virusi vitatu vinavyotafuna maendeleo ya Mara

February 7, 2022 11:57 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni uzembe, ufujaji fedha na mivutano ya watendaji.
  • Aagiza Takukuru, wakaguzi kuingili kati utekelezaji wa miradi.
  • Awataka wananchi wa Mara kupambani maendeleo yao.

Dar es Salaam. Wakati Rais Samia akihitimisha ziara yake katika Mkoa wa Mara leo, amesema maendeleo ya wananchi katika mkoa huo uliopo Kanda ya Ziwa yanachelewa kwa sababu kuu tatu ikiwemo uzembe na ufujaji wa pesa uliokithiri miongoni mwa watendaji wa Serikali.

Rais Samia amehitimisha ziara yake ya siku nne mkoani humo leo Februari 7, 2022 kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu  maji mji wa Bunda ambapo shughuli nyingine iliyompeleka ilikuwa ni maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi mkoani humo inachelewa sana katika utekelezaji wake licha ya “fedha nyingi ambazo Serikali inamimina ndani ya mkoa.”

Amesema kuchelewa kwa miradi hiyo ambako kunawaathiri wananchi kunatokana na mambo makuu matatu: uzembe ambayo ameagiza yafanyiwe kazi ili kasi ya maendeleo ianze kuonekana.

“Moja kwa sababu tu ya uzembe lakini pili pia kuna ufujaji wa fedha lakini tatu kuna mivutano mingi sana ndani ya mkoa huu. Mivutano ya mradi uende wapi, mwingine anavuta kwake kwa ubinafsi bila kujua upande ambao ulitarajia huduma ziende ni upande wa wananchi wengi.

“Niwaombe sana muache mivutano, siasa ziende vizuri ili miradi iweze kutekelezwa vizuri,” amesema Rais.


Soma zaidi:


Suluhu ya kuharakisha maendeleo

Ili kukabiliana na tatizo la ufujaji wa fedha zinazotolewa na Serikali, amewataka wakaguzi wa ndani kutimiza wajibu wao kikamilifu kukagua fedha za miradi tangu zinapoanza kutumika na kuacha kuwa sehemu ya kuhujumu fedha za Serikali.

“Wakaguzi wa ndani ambao mko kila halmashauri naomba mfanye kazi zenu kwa sababu mtakapofanya nyinyi vizuri, wakaguzi wa hesabu wale wakubwa wa Serikali hawatakua na kazi kubwa kwa ajili ya halmashauri zenu,” amesisitiza huku akiwataka kutoa taarifa mapema ili hatua zichukuliwe.

Aidhaa, amewataka mawaziri wanaohusika na Idara ya Ukaguzi, kuwabadilisha vituo wakaguzi wa halmashauri ili kupunguza mazoe na watendaji wengine wabadhirifu.

“Lakini wengine maafisa Takukuru, mko katika maeneo haya kupambana na vitendo vya rushwa msisubiri ubadhirifu wa fedha umeshatokea ndiyo unakwenda kukagua na kutoa taarifa. Mimi naomba mfanye kazi yenu wakati miradi imeingia mnafuata hatua kwa hatua kupambana, kuzuia vitendo vya rushwa,” amesema Rais Samia akitoa maagizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitoa kitambaa kuweka jiwe la msingi mradi wa miundombinu ya kusafisha na kutibu maji pamoja katika viwanja vya Shule ya Msingi Miembeni wilaya ya Bunda mkoani Mara leo tarehe 07 Februari, 2022.

Pia ameagiza halmashauri zote nchini zitumie washauri elekezi wa miradi na kununua vifaa vyenye ubora ili kuepusha miradi kujengwa chini ya viwango.

Aidha, Rais Samia amewataka wananchi wa Mkoa wa Mara kutoka usingizini na kuanza kuwasimamia viongozi wao kuhakikisha wanawajibika na kuwa wawazi katika rasilimali zao.

“Wana Mara mkeni miradi inayoletwa huku ni yenu fuatilieni, fanyeni, semeni. Maendeleo ni yenu si yangu,” amesisitiza Rais Samia.

Enable Notifications OK No thanks