Mvua za masika: Wakulima watakavyoongeza uzalishaji wa mazao

March 7, 2022 8:00 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wanalima mazao yanayostahimili mvua nyingi ikiwemo mpunga na viazi.
  • Mvua hizo zimeanza kunyesha katika mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

Mwanza. Baada ya kupita katika kipindi cha ukame, wakulima wamesema wana matumaini makubwa ya kuongeza uzalishaji na kupata tija zaidi kutokana na kuwepo kwa mvua za kutosha za masika zilizoanza kunyesha wiki ya tatu ya mwezi Februari.

Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021 wakulima hawakufaidika kikamilifu na mvua za vuli kwa sababu zilikuwa chache na maeneo mengi kuwa na vipindi virefu vya ukavu, hivyo kuathiri shughuli za kilimo na ufugaji.

Wakulima hao wametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri uwepo wa mvua za kutosha ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwaletea tija wakulima katika shughuli zao.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliyekuwa akitoa utabiri wa mwelekeo za mvua msimu wa masika za Machi hadi Mei 2022 jijini Dar es Salaam Februari 17, 2022 alisema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

“Ongezeko la mvua linatarajiwa hususan katika kipindi cha mwezi Machi 2022 katika maeneo ya pwani ya kaskazini na mwezi Aprili 2022 kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki,” alisema Dk Kijazi.

Msimu wa mvua za masika ni mahususi katika Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Pia mvua hizo hunyesha katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

Wakulima walivyojipanga

Baadhi ya wakulima waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wamesema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa mvua za kutosha kutoka kwa TMA watazitumia vizuri ili kupunguza maumivu waliyoyapata mwaka jana.

“Msimu wa mvua uliopita tulitumia kupanda mazao yanayostahimili ukame: mahindi, mtama na pamba, mwaka huu watu wengi wamelima pamba na inastawi vizuri,” amesema Petro Pendo, mkulima kata ya Usagara mkoani Mwanza.

Hata hivyo, Pendo amesema kwa kuwa hivi sasa mvua zimeanza kunyesha watazitumia kupanda zao la mpunga ambalo linastawi  kwenye mvua nyingi.

“Mpunga unahitaji mvua nyingi hivyo tutamia mvua hizi ili kupanda kuongeza mazao ya chakula nyumbani ambapo kwa msimu wa mahindi hayakuwa mengi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” amesema Pendo.

Mkulima mwingine mkoani Mwanza, Maria Shadrack amesema kutokana upungufu wa chakula walionao watazitumia kuongeza uzalishaji ikiwemo kulima viazi vitamu ili kujitosheleza kwa mwaka mzima wa 2022.

Amesema hali ya upatikanaji wa vyakula kwa sasa imekuwa mgumu kwa kuwa wakulima hawakupanda mahindi ya kutosha kutokana na msimu wa mvua za vuli kusua sua.

“Hivi sasa tunalazimika kununua sado la mahindi kwa Sh2,800 na mhogo, kisado Sh2,500 huku mchele kilo moja ikipanda kutoka Sh1,000 mwezi Novemba na kufikia Sh1,800 mwezi huu,” amesema Maria.


Soma zaidi: 


Licha ya kuwa wakulima watafaidika na ujio wa mvua hizo za masika, pia zinaweza kusababisha madhara katika shughuli zao ikiwemo kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi na mazao jamii ya mikunde.

Aidha, TMA imewashauri kuimarisha miundombinu ya kilimo na kudhibiti visumbufu vya mimea hasa magonjwa ya kuvu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

“Wakulima wanahimizwa kufanya palizi kwa wakati, kutafuta na kutumia ushauri wa wataalam wa kilimo katika maeneo yao,” alisema Dk Kijazi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Idetemya katika kata ya Usagara, Juma Nyanda amewataka wakulima kuzitumia mvua hizo kupanda mazao yanayostahimili mvua nyingi ili kuepuka hasara huku wakifuata ushauri wa wataalam wa kilimo katika maeneo yao.

Kutokana na mvua za masika zilizoanza kunyesha, shughuli za kibiashara zinazohusisha hali ya hewa kama vile kilimobiashara zinaweza kunufaika kutokana na ongezeko katika uzalishaji. 

Jackson Mwima, mkulima wa Chalinze mkoani Pwani amesema itazitumia mvua hizo kuongeza uzalishaji katika kilimo cha korosho na miwa ili kujipatia faida ambayo hakuipatia msimu uliopita.

“Nimejipanga vizuri nimeanza kulima tayari, mvua hizi hazitanipita bure lazima nipate fedha,” amesema Mwima. 

/
No matches found for this filter
30 May, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
30 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
30 May, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

Nukta TV

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

Nukta TV

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

Nukta TV