Wiki ya Maji: Wadau wanavyookoa mazingira ya Ziwa Victoria

March 23, 2022 5:46 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Baadhi ya wafanyakazi kiwanda cha TBL mkoani Mwanza wakishiriki kuondoa taka ngumu kando ya Ziwa victoria ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Maji. Picha|Mariam John.


  • Washiriki kufanya usafi kando ya ziwa hilo.
  • Washauri elimu itolewe zaidi kwa wananchi.

Mwanza. Wakati leo ni Kilele cha Wiki ya Maji, wananchi wametakiwa kutunza chanzo cha maji ya Ziwa Victoria kwa kutotupa taka ngumu katika ziwa hilo ili kuepusha athari mbalimbali ikiwemo vifo kwa viumbe hai na mazingira ya ziwa hilo.

Utupaji taka hovyo ikiwemo za plastiki imekuwa ni changamoto kubwa duniani ambayo imekuwa ikihatarisha viumbe vya baharini na afya ya binadamu kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya chupa za plastiki.

Meneja wa kiwanda cha kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Mkoa wa Mwanza kinachozalisha kinywaji, Godwin Fabian amesema wametumia kilele cha Wiki ya Maji iliyofanyika kati ya Machi 16 na 22 mwaka huu kuondoa taka ngumu zinazotupwa ndani na kando kando ya Ziwa Victoria.

Fabian amesema wameamua kuondoa uchafu huo ziwani kwa kuwa asilimia 95 hadi 99 ya bidhaa zikiwemo bia zinazozalishwa kiwandani hapo zinatumia maji ambayo yanatoka ndani ya Ziwa Victoria.

“Tumeamua kufanya usafi ili kuondoa taka zote ngumu zinazoweza kuharibu maji ambayo tunayatumia katika kutengenezea bidhaa zetu, hivyo ni jukumu letu kuwalinda watumiaji wa bidhaa zetu kufurahia zikiwa kwenye ubora ,” amesema Fabian.

Amesema pamoja na kufanya usafi pia wanashiriki kutoa elimu kwa wananchi hasa wanaozunguka Ziwa Victoria kuhakikisha wanazikusanya taka zote ngumu na kwenda kuzichoma na si kuzitupa ndani ya ziwa hilo.


Soma zaidi:


Kwa mujibu wa Programu ya mazingira ya Umoja wa kimataifa (UNEP), chupa za plastiki milioni 1 zinanunuliwa kila dakika duniani, huku tani milioni 300 za taka za plastiki zikizalishwa kila mwaka, kiasi ambacho kina karibia uzito wa watu wote duniani.

Hali hiyo imesababisha taka za plastiki kutapakaa kwenye mazingira na ufukweni mwa bahari na maziwa, jambo ambalo linazidisha athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na ongezeko la joto.

Meneja Usalama wa Mazingira wa kiwanda hicho, Method Marko amesema pamoja na kufanya usafi lakini ipo mitambo inayotumika kusafisha maji yanayotumika kiwandani hapo kabla hayajarudishwa ziwani.

Baadhi ya wananchi  wanaozunguka ziwa hilo wamekiri kuwepo kwa taka ngumu kando ya ziwa ambazo nyingi zinatoka ndani ya maji na hivyo kusababisha athari za kimazingira na uchafuzi wa maji.

“Uchafu mwingi unatoka ndani ya Ziwa Victoria na hii ni kufuatia wasafiri kutupa taka hizo ndani ya ziwa kama makopo ya plastiki, karatasi za nailoni, hali hiyo inasababisha mawimbi yanapovuma huzisukuma taka hizo kuja nchi kavu,” amesema Juma Mugusi, mkazi wa Bwiru mkoani Mwanza

Mugusi amekiomba kiwanda cha TBL kwa kushirikiana na wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi mara kwa mara ndani ya ziwa hilo na si kusubiri siku za maadhimisho pekee.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW