Profesa Ngowi: Mtaalamu wa uchumi anayeliliwa na wengi Tanzania

March 28, 2022 12:28 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amefariki dunia leo kwa ajali ya gari mkoani Pwani.
  • Alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam.
  • Wasomi, Watanzania wasema alikuwa mtu muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Dar es Salaam. Nyota imezimika na wengi wanaililia. 

Saa chache baada ya habari za kifo chake, Watanzania wakiwemo viongozi wameungana na wana jumuiya ya Chuo Kikuu cha Mzumbe kumlilia Profesa mashuhuri wa uchumi Tanzania Honest Ngowi aliyefariki dunia leo katika jali ya gari mkoani Pwani.

Prof Ngowi, aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam na dereva wake Innocent Mringi, wamefariki baada ya gari aina ya Land Cruiser waliyokuwa wakisafiria kuangukiwa na lori katika eneo la Mlandizi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Lughano Kusiluka katika taarifa iliyotolewa na chuo hicho leo Machi 28, 2022 amesema ajali hiyo imetokea wakiwa njiani kuelekea kampasi kuu, Morogoro kwa shughuli za kikazi.

Prof Kusiluka amesema Ngowi alikuwa mhimili muhimu katika menejimenti ya chuo hususani katika usimamizi wa shughuli za kitaaluma Ndaki ya Dar es Salaam, mbunifu, na msimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo, utafiti, machapisho na elimu kwa umma.

“Daima tutawakumbuka na kuuenzi mchango wao mkubwa kwa kipindi chote cha utumishi wao katika kuendeleza Chuo Kikuu Mzumbe,” amesema Prof Kusiluka.

Taarifa ya kifo cha Prof Ngowi aliyekuwa amebobea katika masuala ya uchumi kimewashtua wengi ikizingatiwa kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. 

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema ni pigo kubwa kwa taifa kumpoteza Prof Ngowi ambaye wakati wote alikuwa tayari kutoa elimu ya masuala ya uchumi kwa manufaa ya umma.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo katika salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Prof Ngowi amesema anamshukuru Mungu kwa maisha ya nguli huyo wa uchumi.

“Tabasamu limeondoka. Hakika na mengi kichwani yamepotea. Asante sana Mungu kwa maisha ya Prof Honest. Ulimfanya awe zaidi ya wengi ili kuwafanya  watabasamu kupitia yeye. Leo hatunaye. Pumzika Honest. Pumzika Profesa. Taifa limejifunza mengi kwa ulivyoishi. Nenda salama,” ameandika Chongolo katika ukurasa wake wa Instagram. 

Kifo cha Prof Ngowi kimeamsha upya mjadala juu ya usalama barabarani nchini hasa baada ya kufululiza kwa ajali kubwa siku za hivi karibuni  ikiwemo iliyoua watu 23 katika eneo la Melela mkoani Morogoro.

Mtumiaji wa Twitter, Manace (@Manace50164839) amesema kifo cha mwanazuoni huyo wa uchumi kitumike katika kutafakari kuhusu usalama barabarani huku akisema ameumia sana kuhusu kifo chake.

“Profesa Honest Ngowi. Mungu aliyeamua kukuita kwake wakati huu wa mfungo mtukufu wa Kwaresma, akurehemu. Na pia atupe sisi neema na akili za kuanzisha mjadala mkubwa kuhusu usalama barabarani. Nimeumia sana moyoni kwa kifo chako.??,” amesema Manace.

Dickson Kamala (@ItsKamala), amesema Prof Ngowi alikuwa mstari wa mbele kuwasaidia vijana hasa kuwatia moyo katika mambo yanayolenga kuboresha maisha yao na jamii.

“Prof Ngowi @NgowiTv siku akikutana na kijana akakuta ana kitu fulani ama initiative alijitahidi kuhakikisha inafika mbali. Amekuwa rafiki na mzazi kwangu last time (muda uliopita) akasema dogo oa mie ntakuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi, upumzike mzee wangu vijana wako tutakukumbuka,” amesema Kamala katika ukurasa wa Twitter.


Soma zaidi: 


Safari ya kitaaluma ya Prof Ngowi

Kwa mujibu wa Chuo Kikuu Mzumbe, marehemu Prof Ngowi aliajiriwa na hicho  mwaka 1994 kama Mkufunzi Msaidizi, baada ya kuhitimu Stashahada ya Juu ya Mipango ya Uchumi.

Baadaye alijiendeleza na kupata Shahada ya Kwanza, Shahada ya Umahiri katika Biashara na Uchumi, na baadae mwaka 2014 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uchumi. 

Mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Profesa Mshiriki, na kuongoza Idara mbalimbali za Chuo Kikuu Mzumbe kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam hadi umauti ulipomkuta.

Mbali na kushika nafasi za uongozi Prof Ngowi amekuwa mjumbe wa bodi mbalimbali za taasisi za umma na binafsi, bodi za kitaaluma, mshauri na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, mtafiti, mshauri na Mwandishi wa Makala mbalimbali za uchumi, na mtoa mada katika makongamano ya kitaifa na kimataifa. 

“Amefanya utafiti, ameshauriana, ametoa mihadhara na kuchapisha kwa upana (zaidi ya machapisho 100 ya kitaaluma, ripoti zaidi ya 80 za utafiti na ushauri na zaidi ya nakala 2000 za magazeti na majarida katika uchumi, biashara na maeneo yanayohusiana,” inaeleza sehemu ya wasifu wake katika tovuti ya Chuo Kikuu Mzumbe.


Rafiki wa wanahabari

Prof Ngowi mbali na shughuli za kitaaluma amekuwa akishiriki katika mijadala mbalimbali ya uchumi nchini na amekuwa akiandakia safu katika vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo magazeti ya Mwananchi na The Citizen.  

Ni moja ya wataalamu wa uchumi waliowasilisha masuala ya kiuchumi kwa rahisi ambayo ingemsaidia mtu kuelewa kinachoendelea katika nyanja hizo hasa kupitia makongamano na vyombo vya habari. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Limited, Bakari Machumu amesema hana maneno ya kusema kuhusu kifo hicho, zaidi ya kusema “Kinara wa kugawa maarifa, mchumi, mjasiriamali, mwalimu, mpambanaji kwa vitendo kweli kweli.”

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW