Rais Samia awalilia 19 waliofariki ajalini Iringa

June 10, 2022 12:20 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ajali iliyohusisha lori na basi aina ya Coaster katika mji wa Mafinga.
  •  Madereva watakiwa  kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga  kutokana na ajali iliyotokea katika Mji wa Mafinga mkoani Iringa na kuua watu 19.

Rais Samia katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu leo Juni 10, 2022 amesema anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi, basi dogo la abiria aina ya Coaster lililokuwa likisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Iringa liligonga lori lililokuwa limeharibika katika eneo Milo wilayani Mufindi mkoani humo.

Wakati majeruhi wakiwa wanaokolewa lilitokea lori lingine lililopoteza uelekeo na kugonga tena Coaster hiyo pamoja na majeruhi waliokuwa wanaokolewa na mtoto mmoja wa kike.


Soma zaidi: Zaidi ya watu 57 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kuwaka moto Morogoro


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Mafinga, Dk Peter Msafiri amethibitisha kupokea miili ya watu 17 na majeruhi tisa lakini wawili walifariki wakati wanaendelea kupata matibabu na kufanya jumla ya vifo kufikia 19. 

Dk Msafiri amesema majeruhi wengine wanaendelea vizuri na wale ambao hali zao siyo nzuri unaandaliwa utaratibu wa kuwapeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

“Majeruhi wengine hali zao zinaendelea vizuri wanaendelea kupata matibabu na wale ambao hali zao siyo nzuri tunaandaa utaratibu wa kuwapeleka hospitali ya rufaa ya Iringa kwa matibabu zaidi,” amesema Dk Msafiri.

Ajali za barabarani zimekuwa zikisababisha majeraha, ulemavu na vifo na hivyo kupunguza nguvukazi ya Taifa, licha ya Serikali na wadau wa usalama barabarani kuendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti ajali hizo.

Rais Samia ametoa wito kwa vyombo vinavyosimamia usalama wa barabarani kuendelea kutoa elimu kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali hizo.

“Rais Samia pia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Mungu azilaze roho za marehentu wote mahali pema peponi. Amina” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW