Sekou Toure ilivyopambana kupunguza vifo vya uzazi

June 13, 2022 1:47 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Robert Gabriel (kushoto) baada ya kutembelea jengo la mama na mtoto lililokamilika kwa asilimia 97 katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure. Picha| Mariam John.


  • Ni hospitali ya Sekou Toure ambayo imeboresha huduma zake.
  • Mwaka 2021 ilirekodi vifo nane tu kutoka 18 vya mwaka 2017.

Mwanza. Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure imefanikiwa kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi hadi nane mwaka 2021 kutokana na kuimarisha huduma za afya huku ikijenga jengo la kisasa kuhudumia wanawake wanaopelekwa kutibiwa hospitalini hapo. 

Kwa mujibu wa hospitali hiyo ambayo imekuwa ikihudumia watu wa Kanda ya Ziwa, mwaka 2017 ilirekodi vifo 18 vya mama na mtoto ambapo vimeshuka hadi nane mwaka jana.  

Hospitali imefanikiwa kupunguza vifo hivyo baada ya maboresho makubwa ya huduma za uzazi zinazotolewa hospitalini hapo ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu. 

“Jambo ambalo tungeweza kujivunia kama hospitali ni hili la kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini pia yapo mafanikio mengine ambayo hospitali imeyafikia lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Bahati Msaki. 

Kwa sasa, wajawazito 25 hadi 30 hujifungua kwa njia ya kawaida katika hospitali hiyo kwa siku huku watatu hadi 10 hujifungua kwa njia ya upasuaji. 


Zinazohusiana: 


Kuimarisha huduma

Ili kuimarisha huduma za uzazi, hospitali hiyo imezindua jengo la kisasa la mama na mtoto ambalo limekamilika kwa asilimia 97 na kugharimu zaidi ya Sh10.1 bilioni. 

Dk Msaki amesema hospitali hiyo pia ina mpango wa kuanzisha huduma ya tiba mtandao ambayo itaunganisha wataalam walioko katika hiyo na wale ambao wako nje ya hospitali hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel amewataka watoa huduma za afya kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, miiko na maadili ya utumishi wakati wa utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Amesema majengo haya yanayojengwa yanahitaji watoa huduma bora wa afya ili kuwavuta wananchi waendelee kwenda kupata huduma kwenye hospitali za Serikali.

Enable Notifications OK No thanks