Mchuano: Mauzo asali, nta ya Tanzania soko la kimataifa

June 20, 2022 10:44 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mauzo ya asali yashuka kwa miaka miwili mfululizo.
  • Nta yazidi kufanya vizuri kimataifa.
  • Serikali kuongeza uzalishaji, wakulima wanufaike na soko la kimataifa.

Dar es salaam.  Mauzo ya asali ya Tanzania nje ya nchi yameendelea kupungua kwa mwaka wa pili mfululizo hadi kufikia tani 1,201.9 mwaka 2021/22 huku mauzo ya nta yakizidi kuongezeka, jambo linalofungua fursa kwa Watanzania kuongeza uzalishaji na kufaidika na soko la kimataifa la mazao ya nyuki.

Mazao makuu ya nyuki ni pamoja na asali, nta, chavua, gundi ya nyuki na sumu ya nyuki. Asali hutengenezwa na nyuki na kutumika katika shughuli mbalimbali za chakula, urembo na matibabu. 

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2022/23 iliyowalishwa hivi karibuni bungeni na Waziri Balozi Pindi Chana, kwa miaka miwili mfululizo mauzo ya asali yamekuwa yakishuka kila mwaka. 

Hotuba hiyo inaonyesha kuwa mwaka 2019/20, Tanzania iliuza asali tani 2,032 nje ya nchi ambapo mwaka uliofuata mauzo yalishuka hadi kufikia tani 1,988 kabla hayajashuka zaidi hadi tani 1,201.9 mwaka huu wa 2021/22. 

Takwimu za mauzo ya asali za mwaka 2021/22 ni za hadi Aprili mwaka huu ambao unaisha Juni 30. 

Sambamba na hilo, thamani ya mauzo ya asali kwa mwaka mmoja uliopita yameshuka kutoka Sh19.8 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh12 bilioni mwaka huu.

Kupungua kwa thamani na mauzo ya asali nje ya nchi huenda kumesababishwa na kushuka kwa bei ya asali katika soko la dunia, licha ya kuwa uzalishaji wa bidhaa hiyo uko juu ikilinganishwa na kiasi kinachosafirishwa nje ya nchi kila mwaka.

Mathalan, mwaka 2020, tani 30,037 za asali zilizalishwa nchini kutoka tani 30,622 za mwaka 2019. 


soma zaidi


Nta yachuana na asali

Wakati mauzo ya asali yakishuka kwa miaka miwili mfululizo, nta imekuwa ikifanya vizuri sokoni licha ya uzalishaji wake kuwa wa kiwango cha chini.

Kwa mujibu wa hotuba ya wizara hiyo muhimu Tanzania, tangu mwaka 2019/20 mauzo ya nta nje ya nchi yamekuwa yakiongezeka mfululizo. Mwaka huo ziliuzwa tani 251 na mwaka uliofuta zikauzwa tani 393 kabla mauzo kupanda kwa kasi hadi tani 747.5 mwaka huu. 

Kuongezeka kwa zao hilo la nyuki pia kumechangia kuongezeka kwa thamani ya mauzo ya nta inayouzwa nje ya nchi ambapo katika mwaka wa fedha wa 2021/22 kiasi kilichouzwa kilikuwa na thamani ya Sh14.9 bilioni.

Serikali ilivyojipanga kuongeza uzalishaji

Balozi Dk Chana katika hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali itaendeleza viwanda vitatu vya nyuki na kutoa elimu kwa wafugaji nyuki 848 ili kuongeza uzalishaji.

“Vilevile, Wizara itatafsiri kwa lugha ya 129 Kiswahili na kusambaza miongozo mbalimbali ya Sekta ya Misitu na Ufugaji Nyuki ili kutoa uelewa mpana kwa umma kuhusu miongozo hiyo,” alisema Dk Chana.

Serikali inakusudia kuanzisha hifadhi za nyuki za vijiji vitano, kutoa mafunzo ya mbinu bora za ufugaji nyuki kwa vikundi vitano vya wafugaji nyuki.

Pia itaandaa jukwaa la wataalam wa fani ya ufugaji nyuki, na kuwezesha vyama vya ushirika wa wafugaji nyuki kuandaa mikataba ya ufugaji nyuki katika maeneo ya hifadhi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW