Fursa kwa wafugaji wa nyuki mikoa saba Tanzania
- Serikali yapokea Sh27 bilioni kuendeleza sekta ya nyuki nchini.
- Fedha hizo zitaekelezwa katika programu ya kuimarisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini.
- Zitasaidia kuongezeka thamani ya mazao ya nyuki na kutanua wigo wa masoko ya kimataifa.
Dar es Salaam. Wafugaji wa nyuki katika mikoa saba ya Tanzania ukiwemo Mkoa wa Kigoma wana kila sababu ya kutabasamu kwa sababu siku chache zijazo wanaweza kuongeza uzalishaji wa mazao yao baada ya Serikali kuandaa mpango kabambe kwa ajili yao.
Mazao ya nyuki ni pamoja na asali na nta ambavyo hutumika katika shughuli mbalimbali na hivyo kuwapatia kipato wafugaji.
Hata hivyo, matumizi ya teknolojia duni yamekuwa yakizuia wafugaji wa wadudu hao ambao hutumika kuchavusha maua kutonufaika kikamilifu.
Kwa kutambua hilo, Serikali ya Tanzania imepokea Sh27 bilioni kupitia programu ya kuwezesha mnyororo wa thamani wa ufugaji nyuki iliyofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).
Programu hiyo itanufaisha wananchi wa mikoa saba ya Tabora, Kigoma, Katavi, Singida, Shinyanga, Mkoa wa Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.
Akizindua Programu hiyo Februari 21 jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema Serikali inafanya uchambuzi wa kitaalamu kubaini wilaya na vijiji vilivyomo ndani ya mikoa hiyo ambapo mradi huu utatekelezwa.
Programu hiyo itamarisha mifumo ya uzalishaji wa mazao ya nyuki, kuwezesha maeneo ya uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya nyuki katika maeneo husika.
Masanja amesisita ushirikiano kati ya viongozi na wananchi wa mikoa hiyo katika kutekeleza malengo ya programu hiyo.
“Nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote walio katika mikoa husika kushiriki katika kutekeleza programu hii ili iweze kuleta matokeo chanya yanayotarajia,’’ amesema Naibu Waziri Masanja.
Soma zaidi:
- Usafirishaji mazao ya misitu ya kupandwa sasa kuwa usiku na mchana
- Sababu kuu za kuhifadhi rasimali misitu, nyuki
Programu hiyo pia, itaiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Nyuki ipate vitendea kazi katika maabara ya utafiti iliyopo Njiro mkoani Arusha na kuweka mfumo thabiti utakaowezesha ufanyaji wa biashara ya mazao ya nyuki.
Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020, tani 30,037 za asali zilizalishwa mwaka juzi ikilinganishwa na tani 30,622 mwaka 2019, sawa na upungufu wa asilimia 1.9.
Kati ya hizo, tani 2,032.4 zenye thamani ya Sh13.4 bilioni ziliuzwa nje ya nchi ikilinganishwa na tani 607.6 zenye thamani ya Sh4.8 bilioni mwaka 2019.
Maagizo kwa watendaji
Aidha, naibu waziri huyo amewataka viongozi wa wizara washirikiane na Ofisi ya Rais-Tamisemi kutenga maeneo yatakayotangazwa kuwa hifadhi za nyuki ili wananchi na wawekezaji waweze kuyatumia kufuga nyuki kibiashara.
Vilevile, ameelekeza maafisa wa nyuki wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoa mafunzo na huduma za ugani kwa wafugaji nyuki walio katika maeneo mbalimbali hapa nchini pamoja na wizara kuweka mazingira ya kukusanya takwimu za sekta ya ufugaji nyuki.
Balozi wa Ubeliji nchini Tanzania, Peter Van Acker amesema Umoja wa Ulaya umetoa ufadhili huo ili kuisaidia Tanzania kutumia fursa ya soko la asali lililoko katika nchi za Umoja huo.
” Nchi za Ulaya zinazalisha asali inayotosheleza kwa asilimia 60 ya mahitaji, hivyo ni fursa kwa Tanzania kuchangamkia soko la Ulaya kwenye soko la asilimia 40 hasa ikizingatia Tanzania inashika nafasi ya pili Afrika katika uzalishaji mazao ya nyuki nyuma ya Ethiopia,” amesema Van Acker.
Programu hii itakayotekelezwa kwa miezi 72 inatarajiwa kuwezesha kufanya mapitio ya sera, sheria na kuimarisha mfumo wa udhibiti ubora wa mazao ya nyuki, kuimarisha kiwango cha uzalishaji wa mazao ya nyuki yenye ubora na kuboresha mifumo ya biashara.
Latest
