Mgao wa maji unavyowatesa wananchi Mwanza

July 12, 2022 11:22 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Maji yanatoka mara moja au mbili kwa wiki katika Manispaa ya Ilemela.
  • Ubovu na miundombinu wasababisha tatizo hilo.
  • Serikali yatafuna mfupa mdogo mdogo.

Mwanza. Ni takrbani mwezi mmoja sasa huduma ya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imekuwa ya kusuasua hali inayosababisha watu kuamka alfajiri kwenda kutafuta maji visimani.

Wakazi katika manispaa hiyo wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana mara moja kwa wiki na yanapotoka yanatoka kwa saa moja au nusu saa kisha yanakatika hali inayosababisha baadhi ya wapangaji kuhama maeneo hayo.

Licha ya changamoto hizo pia wakazi hao wameeleza kuwa bili za maji zilizotoka mwishoni mwa mwezi uliopita zilikuwa juu tofauti na bili za nyuma ambapo huduma ya maji ilikuwepo. 

“Tunajiuliza hii bili ya Sh40,000 imetoka wapi wakati maji yanakatika siku tatu na yanaporudi yanatoka kwa saa 1 au 2 kisha yanakatika tena, na tumejaribu kuuliza kwa mamlaka husika tunapokea majibu mepesi yasiyoridhisha, tunaomba Serikali itusaidie tunateseka kwa kukosa huduma hii,” amesema Padri Fabian Ngeleja wa Parokia ya Nyamanoro.

Mkazi mwingine Judith Ferdinand amedai kuwa mgawo wa maji umeanza muda mrefu ambapo mamlaka ilikuwa inasingizia kukatika kwa umeme kwenye chanzo cha maji na kufanya marekebisho ya mabomba ya maji.

Amesema kwa sasa maji yanatoka kwa mgawo na yakitoka yanakaa masaa mawili au matatu yanakatika na yanaweza kukatika hadi siku tatu hadi nne.

“Jamani kama ni ukatili basi Ilemela tunafanyiwa ukatili wa kukosa maji, tunaishi na wapangaji lakini wanalazimika kuhama na kwenda kutafuta sehemu ambako maji yanapatikana, akina mama ndoa zinavunjika kwa kuwa wanalazimika kuamka alfajiri kwenda kutafuta maji visimani,” amesema Anastazia Paul, mkazi wa Kangae.

Mbunge wa jimbo la Ilemela, Angelina Mabula amekiri kuwepo kwa tatizo la mgawo wa maji na kueleza sababu ni miundombinu  iliyopo kuwa ya zamani, ubovu wa baadhi ya mitambo uliojitokeza pamoja na chanzo cha maji kilichopo kushindwa kusambaza maji kulingana ongezeko la  idadi ya watu iliyopo kwa sasa.

Amesema mahitaji ya maji kwa siku ni lita za ujazo 160 milioni, maji yanayozalishwa kwa siku ni lita za ujazo 90 milioni hivyo kuwa na upungufu wa lita za ujazo 70 milioni.

“Pamoja na upungufu huo lakini hivi karibuni kuna mota 2 na katika kutengeneza hawakupata mtu wa kutengeneza hivyo walilazimika kuzipeleka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matengenezo ingawa hawajafanikiwa hivyo kulazimika kuagiza mota zingine nje ya nchi ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo,” amesema Mabula.


Soma zaidi:


Amesema kilichofanyika hadi sasa wameandika mradi na wamepeleka Wizara ya Maji kuona kwa namna gani wanaweza kutatua suluhu ya tatizo hili.

“Nimemuomba Waziri wa Maji aje azungumze na wananchi eneo hili kabla sijaondoka ili aeleze kinagaubaga tatizo hili, lakini bado tatizo la maji ni kubwa hivyo niwaombe tuendelee kutumia njia mbadala wa hizi zilizopo wakati Serikali ikitafuta suluhu la maji,” amesema Mabula.

Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mohamed Seif amekiri kuwepo kwa upungufu wa maji hususan kwa maeneo ya pembezoni mwa jiji la Mwanza kutokana na hitilafu ya kuungua kwa mota mbili za kuendeshea mitambo ya kuzalisha na kusukuma maji.

Amesema hatua zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kubadili ratiba za mgawo ya maji ili kuhakikisha maeneo yote yanafikiwa na huduma kwa nyakati mbalimbali. 

“Lakini pia tumeagiza mota mpya ambazo tunatarajia zitafika hapa katika kipindi cha kuanzia wiki mbili zijazo, tunaomba radhi wateja wetu kwa usumbufu wanaopitia na pia tunawasihi kuhifadhi maji kila yanapotoka,” amesema Seif.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW