Mfahamu Mtanzania aliyeandika kitabu cha kwanza kwa mkono Afrika
Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Balozi Costarica Mahalu katikati akipokea nyaraka zilizoandikwa kwa mkono na Mtazania mzaliwa wa Ukerewe , Anicet Kitereza mwaka 1895 kutoka kwa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Colorado Denver cha Marekani. Nyaraka hizo zitatumika kama kumbukumbu chuoni hapo. Picha | Mariam John.
- Ni mzaliwa wa kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza, marehemu Aniceti Kitereza.
- Kitereza aliandika kitabu hicho kwa lugha ya Kikerewe mwaka 1895.
- Kitabu hicho kimeeleza kwa undani kuhusu kabila la Wakerewe.
Mwanza. Chuo kikuu cha Mtakatifu Olaf kilichopo Minnesota nchini Marekani kimetoa nyaraka zilizopo kwenye kitabu kwa mkono na mzaliwa wa kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza, Aniceti Kitereza huku nyaraka hizo zikidhaniwa kuwa za kwanza kuandikwa kwa mkonon chini na barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kukabidhi nyaraka hizo katika chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Colorado Denver cha Marekani, Profesa Charles Musiba amesema Kitereza aliandika kitabu hicho kwa lugha ya Kikerewe mwaka 1895.
Baadaye kilichukuliwa na Dk Gerald Hartwing ambaye alikitafasiri katika lugha sita ikiwemo Kifaransa na Kihispania.
Mbali na nyaraka hizo zinazojumuisha kitabu kilichoandikwa na mwandishi huyo kwa lugha ya Kikerewe chenye jina la’ Bwana Nyombekele na Bibi Bugonoka Ntulanalwona Bulihwali’ pia wamekabidhi barua za Kitereza alizokuwa anamwandikia ndugu yake mzaliwa wa Marekani, Gerald Hartwing amabaye pia ni mtafiti katika sayansi ya utamaduni (Anthropology).
Chuo hicho pia kimekabidhi ala za muziki wa kabila la Wakerewe, nanga, vifaa vya kuandalia chakula, vifaa vya kilimo kama jembe lililotengenezwa kwa kuyeyusha chuma kwa njia ya asili iliyotumiwa na kabila hilo.
Profesa Musiba amesema nyaraka hizo zilichukuliwa nchini na kuhifadhiwa na familia ya rafiki wa Kitereza Dk Hartwing na kwenda nazo nchini Marekani tangu mwaka 1968 ambako zilihifadhiwa nyumbani kwake kisha kuzipeleka katika Chuo cha Mtakatifu Olaf ambapo wasomi wa historia na utamaduni walizitumia kufanya tafiti zao.
Kwa mujibu wa Profesa Musiba familia ya Dk Hartwing kupitia kwa mkewe Shoonie Hartwing waliona ipo haja ya nyaraka hizo kurejeshwa nchini Tanzania ili zitumike katika taasisi za elimu na makumbusho nchini kuelezea historia ya utamaduni wa kabila la Wakerewe.
“Mwanzoni tulihitaji kuzikabidhi katika kitivo cha Historia kilichopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) lakini familia ya Dk Hartwing ikasema ni vyema zikahifadhiwa karibu na alipozaliwa na kuzikwa bwana Kitereza ndiyo maana tumeamua kuzihifadhi hapa,” amesema Profesa Musiba
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUTI) Profesa Costa Mahalu amesema licha ya kuhifadhi malikale hizo bado kuna umuhimu wa kutafuta kabuli lake ili kuweka historia itakayowasaidia watafiti kuandika historia yake.
“Mali kale hizi tutazitumia kuhamasisha wageni kutembelea kwenye chuo chetu cha SAUT kwa ajili ya kujifunza utamaduni wa kabila la Wakerewe na zitarahisisha wanafunzi wanaofanya utafiti kuhusu kabila la Wakerewe kupata taarifa,” amesema Profesa Mahalu.