Halmashauri 4 mtegoni ukusanyaji mapato kiduchu

August 2, 2022 1:11 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni halmashauri za Bumbuli, Kigoma, Buhigwe na Madaba.
  • Halmashauri hizo zimekuwa chini ya Sh1 bilioni.
  • Serikali yasema itachukua hatua.

Dar es Salaam. Viongozi wa halmashauri nne nchini Tanzania  ikiwemo ya Bumbuli mkoani Tanga huenda wakawa katika wakati mgumu baada ya kushika nafasi za mwisho katika ukusanyaji wa mapato katika robo ya nne ya 2021/22.

Robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2021/22 ilikuwa Aprili hadi Juni 2022.

Haya yamebainika leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Innocent Bashungwa akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka 2021/22.

Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imeshika nafasi ya mwisho katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kuliko halmashauri zote 124.

“Halmashauri nne zimekusanya chini ya bilioni moja mabapo halmashauri ya wilaya ya Bumbuli imekuwa ya mwisho kwa kukusanya Sh599.7 milioni,” amesema Waziri Bashungwa. 

Bumbuli ambayo Mbunge wake ni January Makamba, Waziri wa Nishati iko chini ya Halmashauri ya Wilaya Kigoma ya mkoani Kigoma ambayo katika kipindi hicho ilikusanya Sh692 milioni.

Juu ya Kigoma iko Halmashauri ya Wilaya ya Madaba (Ruvuma) iliyokusanya Sh792 milioni na Buhigwa (Kigoma) iliyokusanya Sh880 milioni.

Kwa takwimu hizo, Mkoa wa Kigoma ambao unasifika kwa kilimo cha michikichi na mashamba yaliyopimwa umeingiza halmashauri mbili katika orodha hiyo ya aibu. 

Bashungwa amesema licha ya halmashauri hizo nne kushika mkia bado  zimekusanya zaidi mapato kwa mwaka 2021/22 ukilinganisha na miaka mingine, sambamba na hilo halmashauri zote zitaangaliwa kwa upya kuona namna ya kuweza kuongeza mapato.

Wengine ni kicheko

Wakati wengine wakilia, watendaji wa halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Kinondoni na Dodoma watalala na tabasamu leo kwa sababu halmashauri zimekuwa vinara katika ukusanyaji wa mapato. 

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeshika nafasi ya kwanza kwa kukusanya Sh75.3 bilioni ikifuatiwa na Kinondoni na Dodoma. 

“Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekusanya Sh47.3 bilioni na Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekusanya Sh45.1 bilioni,” amesema  Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amesema kwa robo ya nne ya mwaka 2021/2022, ukusanyaji wa mapato nchini umevuka lengo kwa asilimia 103, ambazo hazijawahi kufikiwa tangu mwaka 2012/2013.

“Hakuna mwaka ambao halmashauri zimewahi kukusanya asilimia zaidi ya 94, wahiyo mwaka huu kuufunga tukiwa tumefika  asilimia 103 ya lengo kwa kweli niwapongeze watendaji wote,” amesema Bashungwa.


soma zaidi


Bashungwa ataka uchunguzi 

Kufuatia agizo la Rais Samia Suluhu alilolitoa kwenye hafla ya kuwaapisha  makatibu tawala wa mikoa na wakuu wa mikoa Agosti 1, 2022 Ikulu jijini Dar es salaam la kuhakikisha mianya ya upotevu wa mapato inazibwa katika halmashauri, Waziri Bashungwa ameagiza kuundwa timu ya kuzuia upotevu wa mapato 

“Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya mapato kupotea nimemuelekeza  Katibu wa Mkuu wa Tamisemi kuunda timu ambayo itafanya uchunguzi ili kuhakikisha chain (mnyororo) ya upotevu wa mapato tunaikomesha,” amesema Bashungwa.

Pia amewataka wakuu wa mikoa kuhuisha leseni za biashara kwenye halmashauri za mikoa ili kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani.

Sambamba na hilo amezitaka halmashauri kuhuisha bajeti zo ili kuendana na hali halisi ya mapato yanayokusanya.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW