Kamati ya ulinzi na usalama kufanya tathimini ajali ya moto hoteli Mwanza
- Ni baada ya kasino iliyopo katika jengo la hotelki hiyo kuteketea kwa moto.
- Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.
- Uchunguzi unaendelea.
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo itaketi kesho Septemba 2 kufanya tathimini ya ajali ya moto iliyotokea jana na kuteketeza jengo la kasino iliyopo karibu na hoteli ya Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 1, Malima amesema analipongeza jeshi la zimamoto kufanikisha kuzima moto huo bila kusababisha madhara yoyote kwa binadamu na hata kwenye majengo mengine kama jengo la benki ya NMB, hoteli ya Pizzaria na maduka mengine yanayozunguka eneo hilo.
“Kesho tutaketi na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuangalia tathimini ya ajali hiyo, lakini pamoja na tathimini hiyo niwaombe wananchi waendelee kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki ambapo kuna matumizi makubwa ya gesi za kupikia majumbani,” amesema Malima.
Awali, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Mwanza, Kamila Labani amesema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto uliounguza kasino iliyopo kwenye jengo la Mwanza hoteli.
Moto huo uliozuka jana majira ya saa 2 usiku ulisababisha sehemu ya kasino na mali zilizokuwemo kuteketea.
“Mpaka sasa hatujabaini chanzo cha moto huo, tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo, tayari taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya moto zikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wako hapa kufanya uchunguzi,” amesema Labani.
Sehemu ya kasino iliyopo kwenye jengo la hoteli ya Mwanza iliyoteketea kwa moto. Picha | Mariam John.
Amesema pamoja na kwamba hotel hiyo kuwa katikati ya mjini na imepakana na maduka mengi ikiwemo jengo la zamani la benki kuu, benki ya NMB, Hotel ya Pizzaria na maduka mengine, lakini walifanikiwa kuuzima na haukuleta madhara kwenye maeneo mengine.
“Hakuna madhara kwenye maeneo mengine isipokuwa kwenye kasino pekee ambapo eneo lote na mali zilizokuwepo ziliteketea,” amesema Labani
Hatahivyo amewataka wamiliki wa majengo ya biashara kuhakikisha wanafunga mfumo wa maji wa zimamoto ili zinapotokea ajali kama hizi iwe rahisi kuuzima na usisababishe madhara makubwa.
“Tunakushukuru kwamba mfumo wa maji kwa upande wa jengo la benki kuu ulikuwa wazi na ndio ulisaidia katika kuzima moto ingawa mfumo uliopo ndani ya jengo hili ulikuwa umefungwa hivyo ni vyema kila mmiliki kuhakikisha anafunga mfumo huo kwa ajili ya dharura kama hizi,” amesema Labani.
Awali Mmiliki wa jengo la Mwanza hoteli ambaye pia ni Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Pamba, Christopher Gachuma amesema jengo hilo lina sehemu mbili na iliyoathirika zaidi ni ile ya nyuma ambapo shughuli za klabu, kumbi za sherehe na kasino hufanyika.
Amesema sehemu hiyo hukodishwa na kwamba hawezi kuzungumzia thamani ya mali zilizokuwemo mpaka muhusika atakapozungumza.
Amesema hoteli ipo salama na shughuli zinaendelea na kwamba anasubiri uchunguzi ufanyike ambapo tayari watu wa Tanesco, Zimamoto na bima za majengo wako hapo kubaini chanzo cha moto huo na kufanya tathimini.