Jinsi ya kuepuka habari za uzushi

September 28, 2022 1:01 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Chukua muda kuisoma kila habari unayopokea.
  • Fanya maamuzi kutoka kwenye vyanzo vya habari vinavyoaminika.         

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kupambana na Uviko-19, ina kibarua kingine cha kudhibiti kuenea kwa habari za uzushi au uongo ambazo ni zao la ugonjwa huo.

Habari hizo ambazo zimekuwa zikitengenezwa na watu wenye nia mbaya zimekuwa zikizidisha athari za ugonjwa huo ikiwemo kiafya na kiuchumi.

Hata hivyo, jukumu la kukabiliana na habari hizo ni la kila mtu duniani. Ufanye nini basi kutambua au kujiepusha na habari ya uzushi endapo itakufikia kwenye simu yako au wakati unatumia mtandao wa intaneti?

Ithibitishe kwanza

Kila upokeapo habari yoyote, kabla ya kuitumia ifanyie tathmni ya kina kwa sababu wanaosambaza habari hizo huzitengeneza kwa namna ambayo inakuwa ni ngumu kutilia mashaka kwa mtu wa kawaida. 

Habari za uongo hujitokeza ambapo msomaji hawezi kuthibitisha madai ya habari hiyo, taarifa hulenga kuvuta hisia ili kupunguza kiu ya kutaka kuutafuta ukweli.

Waandishi wake si wanataaluma, pia habari hizo haziwezi kupatikana mahali pengine na huchapishwa kwenye tovuti ghushi.

Kuna habari gani za uongo?

Takribani miaka miwili iliyopita hadi hivi sasa habari nyingi zinazopotosha zinatungwa kukosoa taratibu za kisasa za matibabu, husasan baada ya kuzuka kwa janga la Uviko-19.

Baadhi ya tovuti hutafsiri vibaya ukweli au kupotosha data, na taarifa katika mitandao ya kijamii zinazoweza kuwa sahihi kwa kiasi fulani lakini hutumia kichwa cha uongo ili kuvutia umakini wako.

Kichwa cha habari kisikufanye uamini habari bali isome kwa makini kujua kama iko sahihi. 


Soma pia

Jinsi ya kuangalia ukweli wa habari kama mtaalamu

Zingatia utambulisho, hakikisha mwandishi na vigezo na uzoefu wa mada inayoelezewa, au anafanya kazi katika tasnia ya habari. Hii inasaidia kupata taarifa sahihi kutoka kwa wahusika wenye mamlaka.

Angalia kama kuna upendeleo, kagua picha, viunganishi vya mtandao na maudhui ya taarifa kujiepusha na kuegemea upande fulani wa maoni kwa kuwa habari za aina hiyo hazikupi ukweli halisi.

Kagua vyanzo, endapo taarifa inataja mhusika ni vema kumfuatilia kwa undani. Wakati mwingine vyama rasmi vya kutoa sauti huwa vinaegemea upande fulani au vinawakilisha maoni potofu ya kundi kubwa la watu.

Zingatia tarehe, baadhi ya habari zinaweza kuisha muda wake na kutoa taarifa zisizo na maslahi kwa wakati uliopo, muda mwingi tumia taarifa mpya zaidi kutoka vyanzo vya kuaminika.

Chunguza taarifa kwa makini, ikiwa ukweli katika mada yako inaonekana kutiwa chumvi, ya kustaajabisha na kutoaminika kwa urahisi, au inayolenga kuteka zaidi hisia. 

Unaweza kutumia Google kufuatilia kama tovuti nyingine zinazoheshimika zinaripoti juu ya kitu kimoja.

Pata Habari kutoka kwa vyanzo rasmi, tovuti kama Reuters na Nukta TV. Njia hii ni rahisi kuingia katika mtego wa habari za uzushi.

Tofautisha Maoni na Ukweli

Unaweza kukubaliana na maoni yanayowasilishwa, au yanaweza kukuletea muktadha wa ukweli kwa njia inayoeleweka kupitia tahariri, barua kwa Mhariri, maoni na uchambuzi. 

Hata hivyo, tambua kuwa wanawasilisha ukweli kwa njia inayokidhi ajenda zao na ujifikirie mwenyewe na kujiuliza Je, “upande wa pili” unawezaje kuwasilisha ukweli huu huu? 


Madhara ya habari za uzushi

Unaweza kukabiliwa na makosa ya kisheria kwa kusambaza taarifa za uongo, zaidi unakosa haki yako ya msingi unapopokea taarifa za aina hiyo.

Habari za uwongo zinaharibu uaminifu wako, ikiwa hoja zako zimejengwa juu ya habari ghushi, itakuwa vigumu zaidi kwa watu kukuamini katika siku zijazo.

Zinaweza kukuumiza wewe na watu wengine wengi, hususan wasambazaji wa ushauri wa matibabu ya uongo wanaoendeleza mashauri potofu kwa watu, mfano madhara mabaya yatokanayo na chanjo ya  Uviko-19. 

Madhara hayo unaweza kuyaepuka kwa kujenga uwezo wa kuhakiki taarifa kwa usahihi na kuongeza faida upande wako, ikiwa unataka kununua hisa katika kampuni, unataka kusoma makala sahihi kuhusu kampuni hiyo ili uweze kuwekeza kwa busara.

Kwa wanahabari, Habari za uwongo hazitakusaidia kupata pesa au kufanya ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi, lakini habari za kweli zinaweza.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW