Nukta Africa, Unesco yawanoa wanahabari uandishi wa takwimu
- Ni mafunzo ya siku tatu yaliyoanza leo.
- Watajengewa uwezo wa kuripoti kwa usahihi habari za takwimu.
Dar es Salaam. Awamu ya pili ya mafunzo kuhusu uandishi wa habari za takwimu kwa wanahabari wa Tanzania yanayoendeshwa na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa yameanza leo kwa njia ya mtandao.
Mafunzo hayo yanayofadhidhiliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) yanafanyika kwa siku tatu kuanza leo Oktoba 3 hadi 5, 2022.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari kutumia takwimu na kutafuta na kutengeneza habari zenye manufaa kwa jamii.
“Uandishi wa habari za data ni mafunzo yanayosisitizwa sana kutokana na mabadiliko ya kidigitali…teknolojia inafanya wananchi wa kawaida waweze kutoa taarifa.
“Mafunzo haya yatasaidia kuongeza thamani ya maudhui yetu,” Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen.
Mafunzo haya yanawezeshwa na Programu ya Kimataifa ya Maendeleo katika Mawasiliano chini ya UNESCO ambapo ni sehemu ya mafunzo ya miezi mitatu yanayotolewa kwa awamu tatu.
Mafunzo yaliyoanza leo ni muendelezo wa mafunzo ya awali yaliyolenga kuwajengea uwezo wanahabari kutumia zana za kidijitali kuandika habari kwa ustadi wa hali ya juu (Multimedia Storytelling’ wiki iliyopita) ambapo wanufaika walikuwa 33.
Soma pia
Faida za uandishi wa habari wa data
Kuongeza msukumo wa uwazi na uwajibikaji, kusaidia wanajamii kufanya maamuzi sahihi zaidi kulingana na takwimu na kuwawezesha wanahabri kutayarisha maudhui ya yenye ushindani katika soko.
Dausen amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kufanyia mazoezi mara kwa mara ya wanachojifunza, ili kuzidi kupanua uelewa wao wa uchambuzi wa data.
Baada ya kukamilika kwa muda wa mafunzo hayo Wanahabari watakuwa na uwezo mkubwa katika mambo muhimu matatu ambayo ni ‘multimedia storytelling’, kuchambua takwimu na mbinu za uthibitishaji wa habari.