Nukta Afrika, TMF wazindua mafunzo ya uthibitishaji taarifa mtandaoni

November 25, 2020 12:47 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa kuthibitisha habari.
  • Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika kwa siku tatu kwa wanahabari 10.
  • Yatawasaidia wanahabari hao kuwa mabalozi dhidi ya habari za uzushi.

Dar es Salaam. Waandishi wa habari wa Tanzania wametakiwa kuchangamkia fursa za mafunzo yakiwemo ya uthibitishaji habari, yatakayowasaidia kuongeza ubunifu na uvumbuzi katika kazi zao ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya upashanaji habari. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya habari ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema ubunifu na uvumbuzi huo ni pamoja na kujifunza zana za kidijitali zinazowezesha kuthibitisha habari (Fact check) wanazoandaa au kupokea kutoka vyanzo mbalimbali. 

Dausen alikua akizungumza katika mafunzo maalum ya mtandaoni ya siku tatu ya uthibitishaji habari leo Novemba 25, 2020 yaliyoandaliwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa kushirikiana  na taasisi ya DW Academie na Nukta Africa. 

Amesema kutokana na kuongezeka kwa mitandao ya kijamii, watu wenye nia ovu wamekuwa wakisambaza habari za uzushi ambazo zimekuwa na madhara makubwa kwenye jamii.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari wa kuthibitisha habari. Picha| Nukta Africa.

“Unaweza ukapata habari kwenye mtandao wa WhatsaApp inayosema kitu fulani kimetokea na kwa sisi waandishi wa habari ukaona habari hiyo inastahili kuchapishwa haraka iwezekanavyo, baadaye baada ya kuichapisha, unakuja kujua ni famba. 

“Mwisho, chombo chako cha habari kinafungiwa,” amesema Dausen.

Dausen ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Nukta Afrika amesema zana mbalimbali za kidijitali ambazo zinaweza kutumiwa na kuwalinda wanahabari na changamoto ya kueneza habari za uzushi.

Mafunzo hayo yaliyopo chini ya mradi wa “TMF Makini Lab Fact-Checking Program”  yanahusisha wanahabari 10 kutoka vyombo vya habari Tanzania yakiwa na lengo la kukabiliana na habari za uzushi zinazosambaa kwa kasi ulimwenguni.


Soma zaidi:


Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Fausta Msokwa aliyekua akizindua mafunzo hayo amesema Tanzania inahitaji waandishi wa habari wanaozingatia ukweli kwa manufaa ya umma.

“Tunahimiza uvumbuzi na ubunifu miongoni mwa waandishi wa habari ili kujenga waandishi wa habari wanaoandaa habari zilizo na maslahi ya umma,” amesema Msokwa.

Mkurugenzi huyo amesema, kila siku kuna mambo mapya na teknolojia mpya za habari zinazovumbuliwa na waandishi wa habari hawatakiwi kubaki nyuma. 

Amesema mafunzo hayo ya siku tatu ni miongoni mwa jitihada za wadau wa habari kuwawezesha wanahabari kupata muamka wa kujifunza ili kukabiliana na habari za uzushi katika maeneo yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW