Watatu wafariki dunia ajali ya ndege Ziwa Victoria, 26 wakiokolewa
- Precision Air yaeleza kuwa ndege zake nyingine zipo salama na zinaendelea na safari kama kawaida
- Kati ya waliookolewa 17 ni wanaume na tisa ni wanawake.
Dar es Salaam. Watu watatu wamepoteza maisha baada ya ndege ya Shirika la ndege la Precision Air kupata ajali katika Ziwa Victoria wakati ikitua katika uwanja wa ndege wa Bukoba huku vikosi vya ukoaji vikifanikiwa kuwaokoa watu 26.
Ndege hiyo yenye namba PW 494 ilikuwa imetokea jijini Dar es Salaam ikiwa na watu 43 wakiwemo abiria 39, wahudumu wawili na marubani wawili.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Issessanda Kaniki amewaambia wanahabari kuwa wamepokea miili ya watu watatu wakiwa wamepoteza maisha.
“Tumewapokea ndugu zetu watatu wakiwa wamefariki ambao ni wanaume wawili na mwanamke mmoja, uokoaji unaendelea kwa wale walio hai huduma zinaendelea kutolewa na wanaendelea vizuri,” amesema Dk Kaniki.
Dk Kaniki amesema kati ya watu 26 waliookolewa kutoka katika ndege hiyo, 17 ni wanaume na tisa ni wanawake.
Soma Zaidi
Watu 26 kati ya 43 waokolewa ajali ya ndege ya Precision Air
Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Precision Air, Patrick Mwanri amesema wanaendelea kushirikiana na mamlaka katika jitihada za uokoaji na tayari wameanzisha vituo viwili vya kutoa msaada kwa familia za walioathirika katika ajali hiyo.
Mwanri amesema mbali na ndege hiyo iliyopata ajali, ndege zake nyingine zinaendelea na safari kama kawaida ingawa huenda kukawa na mabadiliko ya ratiba ili kumudu mabadiliko yaliyotokea.
“Ndege zetu nyingine zote zipo salam ,kila kitu kinaenda vizuri kwenye ndege nyingine, kutakuwa na mabadiliko kidogo ya ratiba leo mchana na kesho asubuhi kutokana na tatizo lililotokea,” amesema Mwanri alionekana kuwa katika masikitiko.
Kauli hiyo ya mkurugenzi inakuja mara baada ya kuibuka kwa wasiwasi kuwa huenda safari nyingine za ndege za kampuni hiyo zikasimama kutoa huduma kutokana na ajali hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa Precision Air umeahidi kuendelea kutoa taarifa mara kwa mara kupitia kwa vyombo vya habari na kupitia vituo maalumu vilivyotengwa katika hoteli ya Blue Saphire iliyopo Vingunguti jijini Dar es salaam na hoteli ya ELCT mjini Bukoba.
Katika mkutano huo na wanahabari, Precision Air haikuruhusu maswali ikieleza kuwa itafanya hivyo katika mkutano ujao.
Latest