Takriban watu 11 kwa kila 100,000 hujiua kila mwaka Afrika
- Kiwango hicho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani cha kimataifa ambacho ni watu 9 kwa kila watu 100,000.
- Sababu ni matatizo ya afya ya akili na ugumu wa maisha.
- Hujiua kwa kujinyonga, kunywa sumu, kujitosa majini, kutumia bunduki, kujirusha kutoka ghorofani.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema tatizo la watu kujiua barani Afrika ni kubwa ambapo karibu watu 11 katika kila watu 100,000 wanakufa kila mwaka kwa kujiua barani humo, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko wastani wa kimataifa.
Katika takwimu zake zilizotolewa jana Oktoba 7, 2022 mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo, WHO imesema kiwango hicho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha wastani ulimwenguni ambacho ni watu tisa kwa kila watu 100,000.
“Hali hii inatokana kwa kiasi kikubwa kwa kutochukuliwa hatua za kushughulikia na kuzuia sababu za hatari ikiwemo hali ya matatizo ya afya ya akili ambayo kwa sasa inaathiri watu milioni 116 likiwa ni ongezeko kubwa kutoka watu milioni 53 mwaka 1990,” imesema WHO.
Hali halisi ya kujiua barani Afrika
WHO katika taarifa hiyo iliyotolewa jana imesema “Kanda ya Afrika ni maskani ya nchi 6 kati ya 10 zilizo na viwango vya juu vya watu kujiua ulimwenguni.”
Njia zinatotumika zaidi kujiua katika bara hilo ni kujinyonga, kunywa sumu na kwa kiasi kidogo kujitosa majini na kuzama, kutumia bunduki, kujirusha kutoka ghorofani au kumeza madawa kuzidi kiwango.
Uchunguzi unaonesha kuwa barani Afrika kwa kila mtu anayefanikiwa kujiua, kuna takriban watu wengine 20 waliojaribu kujiua.
Soma zaidi:
-
Zifahamu sababu zinazowafanya vijana kujiua duniani
-
Kila sekunde 40 mtu mmoja anapoteza uhai kwa kujiua-WHO
“Kujiua ni tatizo kubwa la afya ya umma na kila kifo cha kujiua ni janga. Kwa bahati mbaya, hatua za kuzuia kujiua ni mara chache sana kuwa kipaumbele katika programu za afya za kitaifa.
“Uwekezaji mkubwa lazima ufanywe ili kukabiliana na mzigo unaoongezeka kwa Afrika wa magonjwa sugu na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile matatizo ya akili ambayo yanaweza kuchangia kujiua,” amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika.
Kwa mujibu wa WHO matatizo ya afya ya akili huchangia hadi asilimia 11 ya sababu za hatari zinazohusiana na kujiua.
Barani Afrika, uwekezaji duni unaofanywa na serikali ndiyo changamoto kuu ya utoaji wa huduma za afya ya akili. Kwa wastani serikali hutenga chini ya senti 50 za Marekani kwa kila mtu kwa ajili ya afya ya akili.
“Ingawa ni uboreshaji kutoka senti 10 za Marekani mwaka 2017, bado iko chini ya dola 2 (Sh4,663) zilizopendekezwa kwa kila mtu kwa nchi zenye kipato cha chini. Zaidi ya hayo, huduma ya afya ya akili kwa ujumla hazijajumuishwa katika mipango ya kitaifa ya bima ya afya.”
Tangazo:
WHO yazindua kampeni
Kutokana na hali hiyo, WHO imezindua kampeni kupitia mitandao ya kijamii, inayolenga kufikia watu milioni 10 kote kanda ya Afrika ili kuhamasisha umma na kuhamasisha uungwaji mkono wa serikali na watunga sera kwa ajili ya kuongeza umakini na ufadhili wa programu za afya ya akili, pamoja na juhudi za kuzuia watu kujiua.
Juhudi hizo ni pamoja na kuwawezesha wahudumu wa afya kusaidia zaidi wale wanaokabiliana na fikra za kujiua, kuwaelimisha watu ambao wanaweza kupata fikra hizo juu ya wapi pa kupata usaidizi.
Pia kuhamasisha umma jinsi ya kutambua na kusaidia wale wanaohitaji msaada na kusaidia kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na afya ya akili na kujiua, kifafa, matatizo ya afya ya akili na matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya.
Uwekezaji duni
Kutokana na uwekezaji mdogo katika huduma za afya ya akili, Afrika ina daktari mmoja wa magonjwa wa akili kwa kila wakazi 500,000, ambayo ni mara 100 chini ya mapendekezo ya WHO. Zaidi ya hayo, wahudumu wa afya ya akili wako wengi katika maeneo ya mijini, huku vituo vya afya vya msingi na vya jamii vikiwa na vichache.
WHO inaunga mkono nchi kuongeza huduma za afya ya akili katika eneo hilo.
Latest