Tanzania itakavyofaidika ujio wa kombe la dunia
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akipokea Kombe la Dunia kutoka kwa Balozi wa Kombe hilo kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil Juliano Belletti. Picha| Ikulu.
- Litachangia kuitangaza nchi na vivutio vya utalii.
- Kuongeza chachu ya kushiriki mashindano hayo makubwa duniani.
Dar es salaam. Baada ya miaka nane kupita, Tanzania imepata tena bahati ya kuwa mwenyeji wa ziara ya kombe la dunia barani Afrika ikiwa miongoni mwa nchi tisa ambazo kombe hilo litapita.
Kombe hilo ambalo limeingia Tanzania leo Mei 31, 2022 litaambatana na fursa mbalimbali kibiashara na utalii.
Mara baada ya kuwasili nchini, kombe hilo lilipelekwa ikulu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan pekee ndiye alilishika kama sheria zinavyotaka kisha akatoa hotuba fupi ambapo ameelezea namna Tanzania itakavyonufaika na ujio wa kombe hilo nchini ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii na kuamsha chachu ya kufanya vizuri zaidi katika michezo.
“Mchango wake kiuchumi na kijamii una umuhimu wa kipekee kwa fursa zinazoweza kupatikana lakini kubwa kuitangaza nchi yetu… kwa hiyo ningependa kombe hili pia litoe hamasa kwetu tuweze kuitumia nafasi hii kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema Rais.
Hii ni mara ya nne kwa Kombe la Dunia kufika nchini Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza lilifika nchini mwaka 2006 na kupokelewa na hayati Benjamin Mkapa na mara ya mwisho liliwasili nchini mwaka 2013 na kupokelewa Jijini Mwanza na Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.
Soma zaidi:
Manufaa mengine ya kombe hilo
Ali Luambano ni mchambuzi wa masuala ya michezo nchini, akiwa mkoani Iringa ameiambia Nukta habari www.nukta.co.tz kuwa ujio wa kombe hilo una faida kubwa kwani utaitangaza nchi kimataifa lakini pia viongozi wa michezo nchini watapata fursa ya kubadilishana ujuzi na wageni waliosindikiza kombe hilo akiwemo gwiji wa zamani wa soka David Trezeguet.
“Ni fursa nzuri kwa viongozi wa shirikisho kupata ujuzi na kubadilishana uzoefu na watendaji kutoka shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA) ,jambo ambalo linaweza kuongeza kitu kwenye soka letu lakini pia Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache ambazo kombe hili litapita kutaitangaza Tanzania kimataifa na kusapoti jitihada za filamu ya “Royal Tour” kutangaza utalii,” amesema Luambano.
Kombe la dunia siku ya kesho yaani Juni mosi litapelekwa katika uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ikiwa ndiyo siku ya mwisho wa ziara hiyo.
“Kombe hili litupe uamsho kuwatayarisha watoto wetu vizuri zaidi, waweze kufanya vizuri zaidi, si kwa kutetema na kunyunyiza bali ufundi zaidi…. kwa ufundi na kuweza kujua pale uwanjani kinatakiwa nini kwa hiyo tujitahidi sana…,” ameongeza Rais Samia.
Sifa ya kombe hilo
Kombe hili limeundwa kwa dhahabu yenye uzito wa kilo 6 iliyotengenezwa kama muundo wa watu wawili wanaoshikilia ulimwengu juu yao. Muundo wa sasa wa kombe Halisi ni wa mwaka 1974 na ni moja ya alama za michezo zinazotambulika zaidi duniani.
Fainali za kombe la dunia hufanyika kila baada ya miaka minne na mwaka huu zitafanyika nchini Quatar ambapo mataifa 54 kugombania kikombe hicho kikubwa kabisa duniani ambapo Afrika itawakilishwa na Senegal,Tunisia, Morocco, Ivory Coast na Cameroon.
Latest
