Tanzania inavyojinadi kimataifa maonyesho ya Dubai Expo 2020
- Yafungua banda lenye bidhaa za Tanzania.
- Watendaji wa Serikali wayatumia kuvutia wawekezaji na watalii.
- Rais Samia kuongeza nguvu Februari 27.
Dar es Salaam. Huenda Tanzania ikafaidika maradufu na fursa za uwekezaji na utalii duniani baada ya Serikali kufungua milango kwa taasisi zake ushiriki maonyesho ya kimataifa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro ameungana na Mawaziri wengine kutoka Tanzania kushiriki katika maonyesho makubwa ya dunia ya Expo 2020 Dubai kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushiriki ikiwa ni jitihada za kuinadi Tanzania katika nyanja mbalimbali za uwekezaji na utalii
Dk Ndumbaro aliyekuwa akizungumza Dubai Februari mara baada ya kutembelea banda la Tanzania katika maonyesho hayo amesema muonekano wa kipekee (Branding) uliopo katika banda la Tanzania ni mkakati wa kuinadi Tanzania katika fursa za uwekezaji, kilimo, utalii, viwanda na biashara.
”Mimi na mawaziri wenzangu tumekuja kuongeza nguvu kuhakikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania zinajulikana dunia kote ambapo katika maonyesho hayo zaidi ya nchi 192 zinashiriki hivyo ni fursa kwetu kama nchi kunadi utajiri wetu ili kuvutia wawekezaji,” amesema Dk Ndumbaro.
Dk Ndumbaro amesema picha na maudhui ya video za vivutio vya utalii viilivyopo katika banda hilo vimekuwa chachu kwa wageni kuendelea kumiminika kutembelea banda hilo.
“Hii inaonesha jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji katika nyanja mbalimbali. Imeongeza muitikio chanya kwa wageni kuja na wanapofika hapa wana vitu mbalimbali vya kuona katika banda letu ambalo lina upekee na picha zenye uhalisia,’’ amefafanua.
Soma zaidi:
-
Tanzania kuinadi kahawa yake katika maonyesho ya kimataifa
-
Tanzania yapata heshima ya kushiriki maonyesho ya biashara China
Aidha,Tanzania imejipanga kutumia vyema ushiriki katika jukwaa hilo ambapo Februari 27, 2022 itakuwa Siku ya Tanzania (Tanzania Day) katika maonyesho hayo, hivyo imejipanga kuinadi Tanzania katika sekta ya Utalii kwa mafanikio makubwa ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kufuatia uwepo wa Siku hiyo, Diaspora, wafanyabiashara wakubwa, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali na wadau wa utalii kutoka kona mbalilmbali za dunia watashiriki katika siku hiyo kwa lengo la kuwashawishi wawekezaji kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali.
Katika maonesho hayo Mawaziri wengine waliowasili nchi Dubai kwa ajili ya kunadi fursa za uwekeaji zilizopo Tanzania ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Miongoni mwa taasisi za Tanzania zinazoshiriki maonyesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS).
Maonyesho hayo ya kimataifa yaliyoanza Oktoba 1 mwaka jana yanaendelea hadi Machi 31, 2022.
Latest