Rais Samia asisitiza siasa za maridhiano kongamano la Bawacha
- Asema bila maelewano hakuna maendeleo.
- Aahidi kusongesha mbele ajenda ya Katiba Mpya.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema siasa za kistaarabu na za maelewano baina ya vyama vya siasa vilivyopo nchini ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa Taifa la Tanzania.
Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lilioandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufanyika leo Machi 8, 2023 katika Ukumbi wa Kuringe, Mkoa wa Kilimanjaro amesisitiza umuhimu wa mazungumzo kwenye kutatua migogoro.
“Panapotokea hoja tukae tuzungumze na siyo kukaa kwenye majukwaa na kuanza kulumbana, hapana tusirudi kule tulikotoka.
“Ikitokea hoja viongozi wetu wapo kaeni zungumzeni kwanini hili limetokea liwekwe sawa tuendelee,” amesema Rais Samia.
Akiwa kwenye kongamano hilo amewataka viongozi na wanachama wa vyama siasa kuiga mfano wa vyama vingine kutoka mataifa yaliyoendelea ambayo huheshimu demokrasia na mabadilishano ya madaraka.
“Hata wale wanaotufundisha demokrasia mambo yale tuliyokuwa tunafanya hayapo, wakimaliza chaguzi zao sijui nani kapata kimya wanaendelea na yao,” ameongeza Rais na kusisitiza kuwa,
“Lengo kubwa ni kujenga amani na utulivu ili Taifa letu lipate maendeleo.wote tunajua bila amani na utulivu hakuna maendeleo.”
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amewahakikishia viongozi na wahudhuriaji wa kongamano hilo zaidi ya 3,000 kuwa mageuzi ya makubwa ya kisiasa yanakuja nchini.
“Taifa la Tanzania lenye ushindani wa kisiasa bila vurugu huku ndipo tunapokwenda,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi
-
Mfumo dume chanzo ushiriki mdogo wa wanawake sekta ya sayansi, teknolojia
-
Sababu zinazochangia watoto wadogo kupoteza hamu ya kula
Changamoto za kufanyiwa kazi
Katika kongamano hilo Rais Samia ameahidi kufanyia kazi baadhi ya changamoto zilizoibuliwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakati wakihutubia kwenye ukumbi huo.
Baadhi ya mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na kuharakishwa kwa mchakato wa katiba mpya, kupanda kwa gharama za maisha, malimbikizo ya tozo pamoja na uonevu unaofanywa na vyombo vya usalama ikiwemo polisi.
“Nawasihi sana msipuuzie Katiba Mpya, kauli hii muichukue kwa uzito mkubwa, kwani ni sauti ya wananchi,” amesema Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe aliyekuwa akihutubia kwenye kongamano hilo.
Maombi hayo ya kuharakisha mchakato wa katiba yaliyotolewa na kiongozi huyo wa Chadema yalijibiwa kwa Raisi Samia alipoahidi kuundwa kwa kamati itakayohusisha vyama vingine vya upinzani.
“Suala la katiba hakuna anayelikataa, hata chama changu kimesema twende kwenye mabadiliko ya Katiba…mambo ni mengi ndani ya nchi hii lakini niwaahidi muda si mrefu tutatangaza kamati,” amesema Rais.
Mbali na Katiba Mpya Rais Samia aliahidi utekelezwaji wa changamoto nyingine zote zilizioibuliwa na wanachama wa chama hicho cha upinzani.
“Yote yaliyodaiwa hapa yatafanyika hakuna gumu yote yatafanika lakini kwanza tujenge amani,” amesema Samia akihitimisha hotuba yake.