Mfumo dume chanzo ushiriki mdogo wa wanawake sekta ya sayansi, teknolojia

Lucy Samson 0715Hrs   Machi 07, 2023 Habari
  • Asilimia 19 tu ya wanawake ndiyo wameunganishwa mtandaoni.
  • Viongozi wa Umoja wa Mataifa wasema akili bandia inaweza kuleta suluhu.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema mfumo dume ni moja kati ya sababu inayorudisha nyuma maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa wanawake wengi duniani.

Kauli hiyo ya Guterres imekuja wakati ambao dunia ikielekea kuazimisha siku ya wanawake duniani ambayo kilele chake huadhimishwa  Machi 8 kila mwaka, huku kukiwa na pengo kubwa la kijinsia katika matumizi ya sayansi na teknolojia.

Guterres aliyekuwa akihutubia  ufunguzi wa mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani (CSW) uliofanyika jijini New York, Marekani jana Machi 6, 2023 amesema mkutano huo umelenga kuongeza usawa na ujumuishi wa wanawake na wasichana kwenye sayansi na teknolojia.

“Watu bilioni 3 bado hawajaunganishwa kwenye huduma ya intaneti na wengi wao ni wanawake na wasichana katika nchi zinazoendelea, katika nchi zenye uchumi duni  asilimia 19 tu ndio wameunganishwa mtandaoni,” amesema Gutterres.

Hali ni mbaya zaidi kwa wasichana na wanawake wanaosoma masomo ya sayansi, teknolojia uhandisi na hisabati (STEM). Ni theluthi moja pekee  waliopata nafasi ya kusoma masomo hayo.


Soma zaidi:


Akili bandia (AI) kuleta kuleta nafuu

Hotuba hiyo ya  Guterres imeungwa mkono na viongozi mbalimbali akiwemo  Rais wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi, ambaye amezungumzia matumaini mapya yatakayoletwa na akili bandia.

“Kujifunza mtandaoni katika baadhi ya maeneo kunapunguza pengo la usawa kijinsia, kuwaandaa wanawake kwaajili ya kupata kazi kidijitali na kuwaunganisha wanawake na fursa za kufanya kazi,” amesema Kőrösi.

Mbali na kupunguza pengo la usawa kijinsia matumizi ya akili bandia  yataimarisha uchumi wa wanawake na kufuta kabisa ubaguzi uliopo.

Kwa mwaka 2023 siku hii muhimu ya wanawake ina kauli mbiu isemayo Dijitali: Uvumbuzi na Teknolojia kwa Usawa wa Jinsia.” ikilenga kuongeza usawa katika matumizi ya teknolojia kwa wanawake.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Wanawake (UN Women) ni asilimia 22 tu ya wanawake wote ulimwenguni wanaofanya kazi kwenye mashirika ya akili bandia.

Related Post