Simulizi ya mamba wanavyokatisha maisha ya watu Ziwa Victoria
- Kuoga na kuchota maji ya kutumia majumbani katika ziwa hilo kwa changia.
- Ndani ya miaka miwili, watu 10 wameuwawa na mamba Kanda ya Ziwa.
- Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari, Serikali ikijenga vizuizi kuwakinga.
Mwanza. Ni siku isiyosahaulika kwa familia ya Protus Tibiabo, mkazi wa Kijiji cha Izidabo katika kisiwa cha Kome wilayani Sengerema baada ya kupokea taarifa ya mkewe Bintliver Evarist (56) kufariki dunia kwa kushambuliwa na mamba.
Tukio la mwanamke huyo wa mkoani Mwanza lilitokea Machi 9 saa 6 mchana wakati marehemu alipokuwa anaoga kando ya Ziwa Victoria.
Mme wa Marehemu, Protus Tibiabo anasema kabla ya tukio hilo walikuwa shamba wakipanda mpunga kwenye majaruba ambayo yapo karibu na ziwa hilo.
“Baadaye nilianza kujisikia vibaya kichwa kikawa kinanisumbua ikanilazimu kurudi nyumbani kupumzika nikamwacha yeye na kijana wetu mmoja wakiendelea kulima na baada ya kutoka shamba kijana alirudi nyumbani na kumwacha mama,” anasema Tibiabo.
Ilipofika saa nane mchana alipokea taarifa za mkewe kufariki dunia kwa kushambuliwa na mamba wakati alipokuwa akioga ziwani.
“Taarifa hizo zilishtua sana hasa ukizingatia wote tulikuwa shamba muda mfupi uliopita,” anasema Tibiabo.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya mashuhuda ambao walikua ziwani wakitega samaki ziwani wanasema walimuona mama huyo akioga na mita chache alikuwepo mamba.
“Tulimshtua kuwa pembeni yake kuna mamba hivyo achukue tahadhari akiwa anajiandaa kutoka gafla mamba alimrukia naye akarukia nchi kavu ambapo aliteleza na kuanguka,” anasema mmoja wa mashuhuda hao, John Chocho.
Baada ya kuteleza alilala kwenye mchanga kwa muda mrefu ndipo mamba huyo alienda na kumng’ata kumvutia majini.
Hata wakati mashuhuda hao wanafika eneo la tukio tayari marehemu alikuwa ameng’atwa sehemu mbalimbali za mwili wake na baadaye alipoteza maisha.
Bintliver ni mongoni mwa watu watano wilayani Sengerema mkoani hapa ambao waliuwawa na mamba kati ya Agosti 2022 hadi Machi 2023.
Vifo hivyo, vimezua taharuki na hofu kwa wakazi wa Mwanza hasa wanaotumia Ziwa Victoria kwa shughuli mbalimbali ikiwemo uvuvi.
Baadhi ya wananchi katika kisiwa cha Kome wilayani Sengerema wakishuhudia mamba wawili waliouawa na askari wa Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), ambapo mamba hao wanasadikika kujeruhi na kuua raia. Picha | Mariam John.
Sababu mamba kushambulia watu
Nukta habari imetembelea baadhi ya wathirika wa walioshambuliwa na mamba katika Kijiji cha Izidabo ambapo wameeleza sababu zinazochangia wanyamapori hao kuwadhuru watu kuwa ni ukosefu wa visima vya maji hali inayosababisha shughuli zote kufanyikia ziwani.
Mpimba Kamwanda (50) ni majeruhi ambaye alishambuliwa na mamba kwenye mguu wake wa kushoto wakati akiruka kutoka majini alipokuwa anaoga majira ya saa 11 jioni Disemba 13, 2022.
“Nilihisi kama kuna kitu kinaning’ata kwenye mguu nikakurupuka kukimbilia nchi kavu na baada ya kufika hapo nikagundua kuwa tayari nilikuwa nimeng’atwa kwakua damu zilikuwa zinanitoka kwa wingi,” anasema Kamwanda.
Huenda asingeng’atwa kwa kuwa alikuwa anaona uvivu kuoga lakini jirani yake ambaye walienda wote kuteka maji alimsisitiza aoge tu ndipo akaona bora aoge.
“Kumbe nilikuwa nimefuata matatizo nilipoingia tu ziwani napaka sabuni kichwani nikahisi nang’atwa na kitu mguuni kutoka nikakuta kweli nimeng’atwa,” anasema Kamwanda.
Mbali na mama huyo, mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Lugaka, Jackson Method naye alishambuliwa na mamba alipokuwa amesimama wakati walipokuwa wanatoka kuvua samaki.
Method anasema walienda mwaloni na baba yake kwa shughuli za uvuvi, muda mfupi baada ya kushuka kwenye mtumbwi gafla alishtukia mamba akimng’ata kwenye makalio.
“Ilitokea kwa haraka sana na sikuwa na fahamu kama eneo nililosimama kuna mamba nilishtukia tu navutwa majini zaidi hadi pale baba na watu wengine waliokuwa hapo walipokuja kunisaidia,” anasema Method.
Ni miezi mitatu sasa toka tukio hilo litokee ambapo ilikuwa siku chache tu kabla shule kufunguliwa.
Ndani ya robo ya kwanza ya mwaka 2023, Method ameitumia nyumbani kuuguza majeraha aliyoshambuliwa na mnyama huyo.
“Hali ilikuwa mbaya kwani hakuweza kukaa alikuwa ni wa kubeba hata anapotaka kwenda kujisaidia, ila angalau sasa anaendelea vizuri,” anasema Florida Mayala, mama mzazi wa Jackson.
Licha ya kijiji hicho kuzungukwa na ziwa, wakazi katika eneo hilo wanasema wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ya kutumia katika shughuli za nyumbani.
Mpimba anasema katika kijiji hicho kuna kisima kimoja cha maji kwa ajili ya kunywa huku shughuli nyingine kama kupikia, kuoga na kufulia huchotwa ziwani.
Kutokana na changamoto hiyo, wakazi hao hulazimika kwenda kuoga ziwani kisha kuteka maji kwa ajili ya kupikia pekee.
“Kisima cha maji ya kunywa kipo mbali hivyo tunalazimika kwenda ziwani kuchota kwa ajili ya kupikia lakini kuoga na kufua hufanyika huko huko ziwani,” anasema Mpimba.
Soma zaidi:
- Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 1
-
Simulizi ya mcheza ngoma aliyeng’atwa na nyoka zaidi ya mara 10
- Simulizi ya mwanamke aliyenusurika kifo na kupoteza watoto watatu baharini
Mamba walikuwepo lakini siyo kama miaka ya hivi karibuni
Penina Mayengela, mkazi wa kijiji hicho anasema zamani tatizo hili la mamba halikuwa kama ilivyo sasa ambapo kila baada ya muda mfupi linatokea.
Wanaoathirika zaidi hapo ni wanawake na wavuvi ambao shughuli nyingi hufanyikia ziwani.
“Tunashambuliwa na wanyama hao kwa kuwa sisi ndiyo tunateka maji ziwani mara kwa mara na ndiyo maana tunashambuliwa zaidi na wanyama hao,” anasema Mayengela.
Penina amesema miaka nyuma wanyama hao walikuwa wachache na walikuwa wanafanya shughuli zao vizuri lakini hivi sasa hofu imetanda zaidi kwa kuwa kila kukicha matukio zaidi yanaongezeka.
Mtendaji wa Kata ya Lugata katika kisiwa cha Kome, Fred Nyangole anasema kwa muda wa hivi karibuni kumeripotiwa matukio mengi ya watu kushambuliwa na mamba hali inayosababisha kuzorotesha shughuli za maendeleo ikiwemo uvuvi.
“Wavuvi wanaogopa kuingia ziwani kuvua na hata wananchi wanaogopa kwenda kufuata maji ziwani,” anasema Nyangole.
Wanafanya nini kupunguza tatizo?
Mwenyekiti wa Kijiji cha Izidabo, Stephano Tungalaza anasema katika Kijiji hicho pekee kwa muda wa miaka miwili tayari watu watano wamefariki dunia kwa kung’atwa na mamba huku watatu wakijeruhiwa.
Tungalaza anasema kwa sasa wameweka sheria itakayosaidia kupunguza matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuzuia uoagaji ziwani huku wavuvi kutotembea majini bali wawe wanapanda mitumbwi.
“Tatizo lililoko kwenye Kijiji hiki ni la toka kizazi na kizazi toka enzi za mababu ambapo shughuli zote zilikuwa zinafanyikia ziwani hivyo pamoja na kuweka sheria hizo lakini hazisaidii,” anasema mwenyekiti huyo.
Anasema kijiji hicho kina vitongoji vitano na kwamba kuna visima vitatu vya kuchota maji ingawa kinachotumika ni kimoja tu huku akiiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi hao kujikinga na wanyama hao wakali.
Kuongezeka kwa mamba Ziwa Victoria kumesababisha wananchi wanaotumia ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali kuishi kwa hofu kwa sababu wamekuwa wakivamiwa mara kwa mara. Picha | Mariam John.
Mwanga kidogo waonekana
Kutokana na changamoto hizo, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) wameanza kufanya Msako kwenye maeneo yanayokumbwa na tatizo hilo ambapo hadi sasa mamba wawili wameuawa.
Afisa Wanyamapori Msaidizi wa Tawa Kanda ya Ziwa, Mohamed Mpoto anawataka wananchi kuchukua tahadhari ya kuepuka wanyama hao ikiwa ni pamoja na kuacha kuteka maji ziwani.
Anasema hadi sasa wamefanikiwa kujenga wigo kwenye moja ya mwalo ambao wananchi huenda kuteka maji ili kusaidia kuzuia mamba wasiingie kwenye eneo hilo kirahisi.
Pamoja na kutoa elimu hiyo lakini pia Tawa wamefanikiwa kuua mamba wawili katika Kijiji cha Izidabo ambao wadaiwa kuua watu.
“Niwaombe wananchi muendelee kuchukua tahadhari kwa kuwa hivi sasa samaki wamepungua ziwani huku wanyama hao wakiongezeka kwa wingi,” anasema Mpoto.
Afisa Uhusiano wa Jamii kutoka Tawa Kanda ya Ziwa, Omary Mhando anasema baada ya kupata taarifa hizo walienda kwenye eneo hilo kwa ajili ya kufanya msako lakini pia kutoa elimu namna ya kudhibiti wanyama hao.
Mpaka sasa wametembelea vijiji tisa vilivyoko kwenye kata nne za kisiwa hicho cha Kome kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na wanyama hao lakini pia kutembela familia zilizoathirika aidha kwa kuuliwa au kushambuliwa na mamba.
Mhando anasema zaidi ya vifo 10 vimetokea katika kipindi cha miaka miwili iliyopita huku idadi ya majeruhi ikiongezeka kila kukicha.
Matukio haya yanatokea kwa kuwa wakazi wanaoishi kwenye kisiwa hicho mara nyingi shughuli zote hufanyikia ziwani hivyo kutengeneza uwanda mpana wa wao kushambuliwa na mamba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Yanga Makanga amekiri kuwepo kwa matukio hayo na kueleza kuwa halmashauri hiyo itatenga fedha katika mwaka wa fedha ujao wa 2023/24 kwa ajili ya kujenga uzio kwenye mialo ambayo wananchi huchota maji.
Anasema zoezi hilo limeanza kutekelezwa kwa baadhi ya kata ambazo zinaishi karibu na ziwa kwa kujenga wigo ili kuwakinga na wanyama hao wakali.
Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana katika hotuba ya bajeti kwa wizara yake ya mwaka 2022/23 alisema Serikali inaendelea kuvuna mamba kwenye mikoa ambayo imekumbwa na matukio mengi ya wananchi kushambuliwa na wanyama hao.
“Wizara imetoa mafunzo ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo katika wilaya 21 na kujenga vizimba viwili (2) vya mamba Ziwa Rukwa katika Wilaya ya Songwe kwa ajili ya kuwakinga wananchi na madhara ya mamba,” alisema Dk Chana.
Pia wizara hiyo imeanzisha utaratibu wa mawasiliano wa namba za simu za kiganjani za bure kwenye kanda ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za wanyamapori wakali na waharibifu kwa ajili ya kupata msaada wa haraka inapotokea matukio.
Latest