Ndani mtiti, nje mtiti: Harufu ya dagaa, uduvi inavyowaathiri wakazi Mwanza

June 13, 2023 4:36 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Harufu kali huzalizwa na wanaoanika dagaa, uduvi katika mtaa wa Mswahili jijini Mwanza
  • Baadhi ya wakazi wasema hukumbwa na kichefuchefu na kutapika mara kwa mara

Mwanza. Miaka minne iliyopita maisha ya Editha Msafiri na wakazi wenzie wa Mtaa wa Mswahili jijini Mwanza yalikuwa ni ya kawaida tu na yenye furaha. 

Wakazi hao wanaokaa mita chache kutoka Ziwa Victoria walikuwa wakifurahia upepo mwanana wa ziwani na hawakuwahi kuwaza siku moja kuishi katika mtaa huo ingekuwa ni “mateso na karaha”. 

“Yaani unavaa vizuri unaweka na manukato yako vizuri lakini unapofika hapo unakutana na harufu kali mpaka unajiuliza hivi mimi nakaa hapa kwa sababu sina hela au nini?” anasema Editha. 

Mtaa anaokaa Editha na familia yake umebadilika ndani ya miaka mitatu iliyopita,kutokana na harufu kali inayosababishwa na kuvunda kwa dagaa na samaki wadogo maarufu kama uduvi wanaoanikwa na wafanyabiashara karibu na makazi yao. 

Wakazi hao wanaishi mita chache tu kutoka eneo ambapo wachuuzi wa dagaa na uduvi hao huanikia dagaa wao lakini pia ni mita chache kutoka mwalo wa dagaa wa Mswahili.

Shughuli kuu inayofanyika hapo ni uvuvi wa dagaa na samaki lakini pia wachuuzi hutumia eneo lilipo nje karibu na barabara kuu ya Mwanza- Shinyanga kuanikia uduvi, konokono na dagaa. 

Editha anasema kabla ya wachuuzi hao kuhamishiwa hapo miaka mitatu iliyopita hakukuwa na kero ya harufu ya aina yoyote, hali ilianza tu pale wafanyabiashara hao wa uduvi na dagaa kuanza kuanikia mazao yao.

Anasema harufu kali huzalishwa zaidi pale mazao hayo ya samaki yanaposhindwa kukauka vema. 

“Kwa kweli mimi sijisikii vizuri yaani unavaa vizuri ili utoke nyumbani, ukitoka tu ndani kwenda kupanda daladala harufu inayokupokea mpaka unajiuliza kwa nini nakaa hapa si bora tu ningehama nikaenda kutafuta sehemu nyingine,” anasema Editha.

Ndani harufu, nje harufu

Harufu hii haishii kuwatesa wakazi hao wanapotoka nje pekee. Lucia Samsoni anasema harufu hiyo huingia ndani kiasi cha kuwakwaza wengi na kusababisha washindwe kula vyema msosi.

“Kuna wakati unapatwa na kichefuchefu cha kutapika na unashindwa hata kula,” anasema Lucia akieleza kuna baadhi wameshahama eneo hilo. 

Mbali na harufu hiyo, Lucia anasema kwenye eneo hilo pia kuna funza na ikitokea umepita kwa bahati mbaya karibu na wanapoanikia dagaa hao wadudu huwapanda miguuni.

Hata Hivyo, wakazi hao wanaishauri Serikali kutafuta sehemu nyingine ya kuwapeleka wafanyabiashara hao kulinda amani na afya ya wakazi hao.

Kujaa kina cha Ziwa Victoria kulivyoharibu mambo

Wachuuzi wanaoanika bidhaa zao katika eneo hilo la makazi katika mtaa wa Mswahili wanasema hawakuhamia hapo kwa bahati mbaya. 

Zuena Hussein, mmoja ya wafanyabiashara hao anasema baada ya mvua kubwa kunyesha mwaka 2018/19 na 2020 na kusababisha kina cha Ziwa kujaa hali ilibadilika na kusababisha mamlaka kuwafukuza katika sehemu waliyotumia kuanikia. 

Ndani ya miaka minne iliyopita maziwa makubwa nchini yaani Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa nyakati tofauti yaliongezeka kina cha maji kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kusababisha madhara makubwa kwa wakazi wa pembezoni.  

Eneo la awali, Zuena anasema, lilijengwa vibanda ambavyo vilipangishwa kwa wachuuzi wengine.

Kutokana na uamuzi huo, Zuena anasema iliwalazimu kuhamia nje ya mwalo na kuendeleza kazi hiyo ambayo huwaingizia kipato cha kuhudumia familia na kupeleka watoto shule.

Mfanyabiashara akianika dagaa katika eneo la Mswahili jijini Mwanza, PichalMariam John/Nukta

“Tunachukiwa na kila mtu”

“Kifupi tunateseka hatuna sehemu maalum ya kuanikia, wananchi wanaopita barabarani na hata wanaokaa karibu na eneo hili wanatuchukia, muda wote wanatutaka tutafute eneo la kuanikia lakini tutaenda wapi na hapa ndio tuliona kuna afadhali,” anasema Zuena ambaye aliiomba serikali kuwatafutia sehemu nyingine.

Harufu hiyo haiwatesi tu wakazi wa eneo hilo bali hata wafanyabiashara wenyewe. 

Gaetruda Yusuph, mjasiriamali wa kuanika uduvi na dagaa, anasema watu wanaopita hapo huziba pua na kutema mate huku wengine wakiwataka kuhama eneo hilo.

 “Tunakutana na kero sana sasa tutafanye tunavumilia kwa kuwa ndiyo kazi tuliyoichagua na hatuna sehemu nyingine ya kuanikia,” anasema Getruda. 

Mjasiriamali huyo, mama wa watoto wanne, amekuwa akifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 10 sasa na imesaidia katika kujikwamua kimaisha.

“Tumekopa kwenye vikundi hatuwezi kukaa tu na kusikiliza malalamiko ya wananchi tunalazimika kuendelea na kazi yetu ili tupate fedha ya marejesho na kuhudumia familia,” anasema Getruda. 

Matumaini ya wafanyabiashara hao kuhama eneo hilo ni finyu jambo linalozidi kuwatesa wakazi wa eneo hilo la Mswahili.

Wafanyabiashara zaidi ya 100 huanika dagaa, uduvi

“Hapa tupo wajasiriamali wengi zaidi ya 100 na miezi miwili iliyopita viongozi wa mwalo walipita kutuandika majina ili kujua idadi yetu na walituahidi kutuhamisha hapa lakini hadi sasa kimya hatuoni kinachoendelea,” amesema Anna Daniel mjasiriamali wa konokono. 

Amesema kabla ya kuhamia hapo walikuwa wanaanika chini ya mwalo lakini walihamishwa ili kuwapisha wajasirimali wengine wenye vichanja ambao serikali huchukua mapato.

“Sasa sisi ambao hatutoi chochote ndio tukahamishiwa huku na wakati huo huo kwa sasa tunaona imeanza kujengwa reli ya kisasa (SGR) wakatuambia tupishe ingawa baadae walituachia kaeneo kadogo ambapo huwa tunajibana kuanika ambako hakawezi kuanika hata gunia labda debe 2 au 3,” anasema Anna.  

Anna na wachuuzi wengine wanaiomba serikali kuwapatia eneo la kudumu la kuanikia litakalosaidia kuondoa kero wanazokutana nazo kutoka kwa wananchi.


Soma zaidi


Harufu kali ina madhara kisaikolojia, kiafya

Uzalishaji wa harufu kali ni miongoni mwa uchafuzi wa hewa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na usipodhibitiwa jarida la utafiti wa masuala ya mazingira la Environmental Research lilidokeza Machi 2022 kuwa huwa na athari kwa binadamu yakiwemo maudhi madogo madogo ya kichefuchefu, kutapika na kuathiri mapafu. 

mujibu wa “Japo harufu kali huenda ikaleta usumbufu kwa watu kuliko masuala ya kiafya ila kuwepo kwenye eneo lenye harufu kali kwa muda mrefu yenye mchanganyiko na kemikali nyingine kunaweza kuleta hatari ya maradhi mengine kama Pumu (Asthma), maradhi ya ngozi (atopic dermatitis) na athari katika ubongo (neurologic damage),” inasomeka sehemu ya utafiti uliochapishwa kwenye jarida hilo wenye kichwa cha habari ‘Uzalishaji wa harufu: Jambo linalogusa umma na hatarishi kiafya.’ 

Wataalamu wa ndani wanasema hakuna madhara ya moja kwa moja  yanayosababishwa na harufu kali inayosababishwa na uchafu au harufu mbaya ya kitu kilichooza isipokuwa labda tumbo kujaa gesi.

Mratibu wa Elimu ya Afya kwa umma kutoka Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, (Sekouture) Renard Mlyakado aliiambia Nukta Habari kuwa hakuna madhara ya moja kwa moja kiafya isipokuwa kisaikolojia.

Dk Mlyakado anasema ingekuwa ni harufu inayotoka kwenye kiwanda ambayo imechanganyikana na kemikali ingeleta madhara makubwa zaidi.

Serikali ya mtaa njiapanda

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kang’anga maarufu kama Mswahili, Zuberi Khamisi amesema wamekuwa wakipokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wakitaka kuwafukuza wajasiriamali hao katika eneo hilo. 

“Ni kweli tunakereka lakini ilikuwa ni njia yao kujikwamua kimaisha kwa sababu kuwaondoa pale ni sawa na kukaribisha vibaka na wizi mtaani kwa kuwa shughuli hiyo inasaidia wananchi kujikwamua na akina mama kujitafutatia ridhiki,” anasema Khamisi.  

Zaidi ya wanawake 160 hujishughulisha na kazi ya kuanika uduvi, dagaa na konokono kwenye eneo hilo na kabla ya kuanza kuanika sehemu hiyo, anasema wachuuzi hao walikuwa wanaanika ndani ya mwalo na hakukuwa na harufu yoyote iliyokera wakazi.

Khamis anasema serikali ya mtaa kwa kushirikiana na wadau wa uvuvi waliwatoa wafanyabiashara hao huko ziwani na kuwaleta nje ya mwalo ili waweze kuanika bidhaa zao vizuri.

‘Wavumiliane kwa sasa’

Anasema waliamua kuwaacha hapo kutokana na mazingira ya mtaa kuzungukwa na milima ambayo sio rafiki kwa kuanikia dagaa. 

“Kitendo hicho kilikuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo ingawa tuliendelea kuwaelimisha na kuwasihi wavumiliane wakati wakitafuta sehemu ya kuanikia,” anasema Khamisi na kuongeza kwa sasa hawawezi kuwahamisha kwa kuwa biashara hiyo inawakwamua wengi kimaisha. 

Anataja shughuli kuu inayofanyika hapo ni kuanika uduvi, konokono na dagaa wachafu kwa ajili ya chakula cha kuku, bata na nguruwe.

Serikali kujenga soko, mwalo wa kisasa

Kutokana na malalamiko hayo, Serikali imekuja na mpango wa kupanua mwalo uwe wa kisasa pamoja na kujenga soko kubwa la kisasa ili kuondoa adha hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi aliiambia Nukta Habari kuwa wako mbioni kujenga soko la kisasa ambalo litakuwa na chanja zitakazotumika kuanikia dagaa na kuachana na teknolojia duni inayotumika sasa na wajasiriamali hao kuanikia.

Hatua hiyo, iwapo itatekelezwa ipasavyo, itasaidia kutokomeza harufu kali inayowakumba wakazi wa Mswahili kama Editha. 

Mkuu huyo wa wilaya amekiri kuwa kwa sasa wafanyabiashara hao wanaanikia chini na wengine kwenye neti kitendo ambacho si kizuri hasa kwa upande wa dagaa ambao unaweza kuwa na mchanga mwingi ambao ni hatari kwa afya.

“Baada tu ya soko hilo kukamilika wafanyabiashara watahamishwa hapo na kuhamia ndani ya soko hilo, tayari usanifu ushafanyika na mkandarasi ameshapewa tenda ya kujenga na kinachosubiriwa ni kuidhinishwa kwa fedha ili kazi ianze,” anasema Makilagi.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
5 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
5 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV